Habari za Punde

Tatizo la Maji Dar kuwa Historia Ifikapo 2020


Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) imesema kuwa Serikali  imejipanga kumaliza tatizo la maji katika jiji la Dar es Salaam ifikapo mwaka 2020. Ambapo upatikanaji wa huduma za maji utakuwa asilimia 95 kwa maji safi na asilimia 30 kwa majitaka.
Akizungumza  na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam, kuhusu mafanikio ya Taasisi hiyo katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja alisema kuwa tatizo la maji katika jiji la Dar es Salaam litaisha ifikapo mwaka 2020 kwa kuwa Serikali imeandaa mfumo mpya utakaosadia wananchi kupata huduma ya maji kwa uhakika.
“Katika mradi wa mfumo wa usambazaji wa majisafi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam mpaka Bagamoyo ambapo  mabomba yenye urefu wa Kilomita 1,426 yatalazwa na wateja wapya zaidi ya 300,000 wataunganishwa”
Mhandisi  Luhemeja, aliongeza kuwa  “vilevile mradi wa mifumo midogo midogo inayojitegemea ya usambazaji maji kwenye maeneo yasio na mtandao (off grid water supply schemes) ambapo kutakuwa na maunganisho ya wateja wapya 100,000 yatasaidia kumaliza tatizo hilo”
Aidha, alitaja mikakati mingine ambayo Serikali imeiweka kwa ajili ya  Jiji la Dar es Salaam kuwa ni kuimarisha mifumo ya usambazaji wa majisafi maeneo ya kusini mwa Dar es Salaam (Part 4D na 4E) ambapo mabomba yenye urefu wa Kilomita 400 yatalazwa na wateja wapya zaidi ya 71,600 wataunganishwa, ikiwa ni sambamba na mradi wa kudhibiti upotevu wa maji.
Pia, alisema mafanikio ya Serikali katika kipindi cha miaka mitatu ni pamoja na   miradi ya ujenzi wa mifumo mipya ya majitaka na mitambo ya kisasa ya kuchakata majitaka katika maeneo ya Jangwani, Kurasini na Mbezi Beach, ikiwa ni pamoja na kumalizia uchimbaji wa visima vya Kimbiji na Mpera na kujenga mifumo ya usambazaji maji .Pamoja na kujenga  bwawa la Kidunda ili kuwa na uhakika wa maji kwenye mto Ruvu katika kipindi chote cha mwaka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.