Habari za Punde

Wananchi wa Kijiji cha Uzini Waiomba Serikali Imruhusu Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Atekeleze Ahadi Yake.

Na. Mwandishi Wetu.
WANANCHI wa kijiji cha Umbuji jimbo la Uzini wameiomba serikali imruhusu Mwakilishi wa jimbo la Uzini, Mohamed Raza Dharamsi, atekeleze ahadi yake ya kujenga kituo cha afya katika jimbo hilo, ili kiwasaidie wananchi.
Mmoja ya wananchi,Ndg.Kheri Omar Hamdan kwa niaba ya wenzake, akizungumza kwenye kikao cha watendaji wa TAMWA, WAHAMAZA na asasi ya mtandao wa wanawake, alisema kama kweli mwakilishi huyo ameshindwa kutekeleza ahadi hiyo aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa uwakilishi Februari 2012 kwa sababu ya kuzuiwa na serikali, ipo haja ya kufikiria kumruhusu ili atekeleza ahadi hiyo.
Raza, Mfanyabiashara maarufu nchini na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alichaguliwa tena katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Wananchi wengi tuna shida na kupata huduma za afya hasa akina mama wa vijijini kwa hivyo tunaiomba serikali imruhusu Raza atekeleze ahadi yake aliyoitoa kwenye uchanguzi kwa sababu atakuwa anatekeleza ilani ya chama chetu,” alisema mwananchi huyo.

Wizara ya Afya iliahidi kujenga kituo hicho kwa ufadhili wa shirika binafsi la Korea Kusini lakini hadi sasa utekelezaji bado haujafanyika.
Kwa sasa huduma ya tiba kwa wananchi wa kijiji cha Umbuji inatolewa na kituo cha kuhudumia akinamama na watoto kilichojengwa mwaka huu kijijini hapo na mfadhili binafsi.
Hata hivyo, kituo hicho hakitoi huduma za dharura kwa mama wajawazito.Katika hatua nyengine uongozi wa hospitali ya Makunduchi, umeimarisha utoaji huduma kwa mama wajawazito katika mazingira rafiki.
Taarifa hiyo imetolewa hivi karibuni mbele ya viongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Kusini na wawakilishi wa asasi za kiraia zinazoshirikiana na watekelezaji wa mradi wa kuinua uwajibikaji Zanzibar (PAZA), unaofadhiliwa na taasisi ya kusaidia asasi za kiraia za Zanzibar (ZANSASP).
Akizungumza kwenye kikao cha kubadilishana mawazo kuhusu ufuatiliaji wa malalamiko ya wananchi, kati ya maofisa wa halmashauri ya wilayani Kusini na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kwenye ukumbi wa halmashauri uliopo Kitogani, kiongozi wa mtandao wa Taarifa na Maarifa, Mussa Hassan Mussa, alisema huduma za uzazi zinazotolewa ni rafiki kwa wajawazito na wananchi wanafurahia mpango huo.
Kikao hicho kiliratibiwa na ofisa ufuatiliaji na tathmini wa Tamwa hapa Zanzibar na kuwashirikisha maofisa mbali mbali wa serikali za mitaa na wana asasi wakiwemo wana mitandao.
Awali kulikuwa na malalamiko kuwa huduma za uzazi ikiwemo kujua kiwango cha mimba mpaka kujifungua pamoja na huduma ya uzazi wa mpango zilikuwa zikitolewa kwa kuchangia.
“Tunafurahia huduma zinazotolewa, hakuna michango yoyote inayotozwa kwa wajawazito,” alisema mama mmoja aliejitambulisha kwa jina la Siti Abdalla.
Habari hiyo iligundulika kupitia utafiti mdogo uliofanywa na waandishi wa habari waandamizi waliodhaminiwa na Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA) kufuatilia huduma za kijamii katika vijiji mbali mbali Unguja na Pemba.
Wahamaza ambayo ni asasi ya kiraia inayoshirikiana na TAMWA pamoja na jumuiya ya hifadhi ya msitu wa Ngezi (NGENARECO) ya Pemba, ilituma timu ya waandishi kwa lengo la kubaini changamoto zinazowakabili wananchi katika kupata huduma za jamii ngazi ya halmashauri zikiwemo pia masuala ya elimu na maendeleo ya jinsia.
Utafiti huo mdogo uliendeshwa pia wilaya ya Kati na Kaskazini Unguja pamoja na wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.