Habari za Punde

Balozi Seif afanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Watu wa Cuba

 Naibu Waziri wa Kilimo wa Cuba Bwana Jose Migvel De Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika Nyumbani kwake Bara bara ya Haile Selassie Jijini Dar es salaam kwa mazungumzo.
 Balozi Seif wa Pili kutoka Kulia akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Naibu Waziri wa Kilimo wa Cuba Bwana Jose Migvel De Numbani kwake Dar es salaam.
Wa kwanza kulia ni Balozi wa Cuba Nchini Tanzania Dr. Lucas Domingo na Kulia ya Naibu Waziri wa Kilimo wa Cuba Bwana Jose  ni Afisa wa Ubalozi wa Cuba Dar es salaam Bwana Sultan.
 Bwana Jose Migvel De wa Pili kutoka Kushoto akisisitiza umuhimu wa Nchi yake kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika sekta za Maendeleo.

 Msaidizi wa Balozi wa Cuba Nchini Tanzania Bibi Meylin Suarez  akiwa makini kufuatilia mazungumzo ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Bwana Jose Migvel De yake.
Balozi Seif akiagana na Mtoto wa Balozi wa Cuba Nchini Tnaznia mara baada ya mazungumzo na Bwana Jose Migvel De.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika sasa  wa kufikia makubaliano ya kuanzisha ushirikiano wa karibu wa uendeshaji wa Miji ya Asili ya Havana Nchini Cuba na Mji Mkongwe wa Zanzibar katika azma ya kulinda Historia muhimu iliyomo ndani ya Miji hiyo Mikongwe Duniani.
Alisema licha ya uwepo wa uhusiano wa muda mrefu wa Viongozi Wakuu, Watendaji na Watumishi wa Umma wa pande hizo mbili kwa mfumo wa kutembeleana katika ziara za Kikazi lakini pia ipo haja ya kuwekeza kwenye eneo hilo la Historia kwa Maslahi ya Kizazi kipya.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa Kauli hiyo Nyumbani kwake Bara bara ya Haile Selassie Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na Naibu Waziri wa Kilimo wa Jamuhuri ya Watu wa Cuba Bwana Jose Migvel De aliyepo Nchini Tanzania kwa ziara ya Wiki Moja.
Alisema Mji ya Havana na Mji Mkongwe wa Zanzibar ina Historia kubwa katika masuala ya Biashara, Siasa, Uchumi, Utamaduni pamoja na Ukarimu wa Watu wake inayopaswa kulindwa na kuendelezwa na Wakaazi wake licha ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni {UNESCO} kuiingiza katika Urithi wa Kimataifa.
Balozi Seif alimueleza Naibu Waziri wa Kilimo  wa Cuba Bwana Jose Migvel De kwamba Zanzibar itaendelea kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na Ndugu zao wa Cuba hasa katika Sekta za Afya na Kilimo ambazo tayari zimeshaleta mabadiliko makubwa.
Alitolea mfano wa jitihada za Serikali ya Cuba ya kuanzisha Chuo cha Madaktari kilichozalisha Madaktari Wazalendo 50 kwa mkupuo Mmoja jambo ambalo ni faraja kwa Zanzibar kutokana na Sera zake za kuimarisha Sekta ya Afya kwa kuweka huduma zake si zaidi ya Kilomita Tano.
“ Ni faraja iliyoje hivi sasa muona  Cuba inaendelea kusomesha Madaktari 15 waliopata mafunzo kupitia Mpango huo ulioasisiwa kufuatia wazo la Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein wakati akiwa Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alipotembelea Cuba Mwishoni mwa Miaka ya 2000”. Alisisitiza Balozi Seif.
Akizungumzia Sekta ya Utalii inayoonekena kuchukuwa nafasi kubwa katika Uchumi wa Dunia Balozi Seif alisema kwa vile Cuba imeshatanua Wigo wa Ushirikiano uliolenga kuimarisha Uhusiano wake na Tanzania, upo umuhimu wa kuiangalia Sekta hii katika nia ya kuimarisha Mapato ya Taifa.
Alisema wakati Zanzibar inajitahidi kuendeleza Sekta hiyo kwa kuimarisha Uchumi wake, Cuba imeshapiga hatua kubwa inayopaswa kuiunga mkono Zanzibar kuelekea kwenye mafanikio zaidi.
Balozi Seif  alimueleza Bwana Jose kwamba Zanzibar imelenga kupokea Watalii zaidi ya Laki 500,000 ifikapo Mwaka 2020 babala ya ile iliyopo hivi sasa ya idadi ya Watalii wanaoingia Nchini zaidi ya Laki Nne na Nusu.
Mapema Naibu Waziri wa Kilimo wa Cuba Bwana Jose Migvel De alisema ziara yake Visiwani Zanzibar imemuwezesha kujifunza mambo mengi  hasa Bidhaa za Viungo pamoja na Historia ya Mji Mkongwe wa Zanzibar yatakayoendelea kubakia katika Historia ya Maisha yake.
Bwana Jose alisema Zanzibar imefanikiwa kuwa na Hazina kubwa ya Historia inayotokana na Rasilmali ya Mji wake ambayo Walimwengu wana kila sababu ya kujifunza ili kujua ladha ya kilichomo ambacho ni adimu kupatikana katika maeneo mengi Duniani.
Akigusia Sekta ya Kilimo Naibu Waziri huyo wa Kilimo wa Cuba alisema kuanzishwa kwa Kiwanda kitakachozalisha Dawa kwa ajili ya kuua Majani yanayozalisha Mbu Mkoani Kibaha ni muendelezo wa Uhusiano mwema wa muda mrefu uliopo kati ya Cuba na Tanzania.
Bwana Jose alisema Kiwanda hicho kitakapokamilika ujenzi wake kitaweza kusaidia kupunguza gharama za matumizi ya fedha nyingi za Kigeni zinazotumika kuagiza Dawa hizo Nje ya Nchi.
Alisema ziara yake Nchini Tanzania imemuwezesha kukutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Wizara inayohusika na Kilimo Nchi Tanzania na kufikia uwamuzi wa kutaka kusaini Mkataba wa Ushirikiano kwa hatua za hapo baadae.
Pamoja na mambo mengine Naibu Waziri huyo wa Kilimo Nchini Cuba aliishukuru na kuipongeza Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msimamo wake wa kuendelea kuiunga Mkono Cuba katika changamoto zake inazopitia Kimataifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.