Habari za Punde

Waziri Mahmoud aahidi kutatua kero jimboni kwake

Na Khadija  Khamis –Maelezo  Zanzibar 
Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki Mahmoud Thabit Kombo ameahidi kuziondoa kero zinazoikabili shehia mpya ya Mombasa jimboni humo ikiwemo Gari la kutupia taka taka, Vifaa na Sare za Walinzi shirikishi.
Ahadi hiyo ameitoa katika kikao cha uongozi wa Shehia ya Mombasa na uongozi wa Jimbo la Kiembesamaki huko kilichofanyika katika kijiji cha kulelea watoto SOS Mombasa.
Mahmoud ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya kale alisema Viongozi wa Jimbo hilo watashirikiana kwa pamoja na uongozi wa shehia ya Mombasa kujadili changamoto zilizopo na kuhakikisha  zinapatiwa ufumbuzi kwa lengo la kuiletea maendeleo shehia hiyo.
Aliwapongeza wananchi wa shehia hiyo kwa kujipanga vizuri kudhibiti uhalifu ikiwemo uporaji na wizi ili usitokee katika maeneo yao kutokana na ulinzi shirikishi uliopo.
Hivyo amewataka kuorodhesha mahitaji ya sare na vifaa vya ulinzi wanavyohitaji ili kuwasaidia Walinzi hao kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Nae Mbunge wa Jimbo la Kiembe samaki Ibrahim Raza aliitaka kamati ya Jimbo itafute Eneo kwa ajili ya kujengewa Kituo cha afya katika shehia hiyo ili kuwaondoshea usumbufu wananchi wa shehia hiyo.
Alisema katika mipango ya utekelezaji Viongozi wamejipanga vizuri na Serikali tayari imeshaanza ugatuzi katika wizara zake tatu ikiwemo afya, elimu na kilimo hivyo wananchi wasitie wasiwasi kupatiwa huduma hiyo.
Alifahamisha kuwa katika changamoto zilizopo ni pamoja na Madimbwi yanayotuwama maji katika eneo hilo hivyo Mbunge huyo ameahidi kumwaga kifusi katika eneo lote la Mombasa.
“Hatutokuwa wazito kuwachangia wananchi wetu kwani wao ndio waliotuweka madarakani wafanye idadi rasmi ya bajeti yao ya mahitaji ili tuifanyie kazi Mbunge nipo na Mwakilishi yupo kwa ajili yenu”, alisema Raza.
Kuhusu suala la Gari la Taka katika shehia ya Mombasa Mbunge Raza alisema watafanya mazungumzo na Baraza la Manispaa ili kama wanalo Gari wafanye makubaliano ya kuweza kulinunua kuhakikisha tatizo hilo linaondoka katika eneo hilo.
Kwa upande wake Katibu wa Fedha na Uchumi wa Kamati ya Shehia ya Mombasa Abdul Sleiman Mohamed alisema iwapo watapatiwa gari la taka taka katika shehiya hiyo wanaweza kuingiza fedha na kujipatia maendeleo bila ya kutegemea kuomba kwa viongozi wao.
Aidha amesema kupitia Gari hilo pia litawasaidia kudhibiti taka taka zisikae kwa muda mrefu na kufanya uchafu ambao utasababisha maradhi ya miripuko.
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Idrisa Abeid Shamte alisema kuwepo kwa ulinzi kunasaidia usalama wa watu na mali zao na kutembea bila ya hofu.
Alisema jumla ya Walinzi 24 hulinda katika shehia hiyo ili kupunguza vitendo vya uhalifu huku Walinzi hao wakikabiliwa na mazingira magumu ya kazi yao ikiwemo vitendea kazi na ofisi ya kudumu.  
Katika kukabiliana na changamoto ya Kodi ya ofisi ya ulinzi shirikishi Viongozi hao wa jimbo la Kiembe samaki walitoa pesa taslimu shillingi laki sita za kodi ya chumba hicho ili walinzi wafanye kazi zao kwa ufanisi.
Shehia hii mpya ya Mombasa awali ilikuwa shehia mchanganyiko ilikuwa shehia ya Michungwani baada ya ugatuzi imeundwa shehia mpya ya Mombasa.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.