Habari za Punde

Dk Shein: Ujenzi wa Bandari ya Mafuta na Gesi Mangapwani umeanza


 STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                   18, February, 2019

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kazi za ujenzi wa Bandari ya Mafuta na Gesi katika eneo la Mangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja, zimeanza.

Amesema ujenzi huo utakaofanyika katika eneo lenye ukubwa wa kilomita sita pia utahusisha ujenzi wa matangi ya kuhifadhia mafuta, sambamba na ujenzi wa barabara pana kuelekea eneo la bandari ili kuziwezesha gari kupita vizuri.

Dk. Shein  amesema hayo katika Hoteli ya Sea Cliff Mangapwani, alipozungumza na Kamati za Siasa za Wilaya Kaskazini 'B' Unguja pamoja na  viongozi wa ngazi mbali mbali wa chama wa Wilaya hiyo, ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kutembelea Wilaya zote za Unguja na Pemba, kukaguwa miradi  ya maendeleo na utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Aidha, katika mkutano huo Dk. Shein alifanya majumuisho ya ziara yake hiyo na kutoa nasaha kwa wanachama hao.

Alisema ujenzi huo umeanza baada ya kukamilika hatua zote za kulipa fidia  vipando vya  wananchi wa eneo hilo la Dundua, kuku hatua za kuwahamishia katika makaazi mapya zikichukuliwa.

Amesema wawekezaji wa mradi huo tayari wamekabidhiwa eneo kwa ajili ya ujenzi wa matangi ya mafuta na kubainisha kuwa matangi yaliopo Mtoni hivi sasa yatahamishiwa huko.

Dk. Shein alisema miundombinu  ya umeme nayo tayari imeshawekwa katika eneo la mradi.

Katika hatua nyengine Dk. Shein alisema ameridhishwa na taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Wilaya hiyo, na kuagiza kuainishwa idadi ya vikao vilivyofanyika kupitia ngazi za shina na Matawi, kwa kigezo kuwa ndiko iliko nguvu ya Chama hicho.

"Nimevutiwa sana jinsi mlivyoweka muhtasari wa utekelezaji wa Ilani............nimeridhika vipi mnavyoshirikiana kati ya viongozi wa Serikali na wale wa Chama", alisema.

Akigusia tatizo la uhaba wa ardhi linalokikabili Kiwanda cha Sukari Mahonda, Dk. Shein alisema Serikali imekipatia kiwanda hicho eneo la ardhi huko Kichwele ili kuendelea na uzalishaji wa miwa, baada ya eneo lake kuvamiwa an wananachi kwa shughuli za kilimo.

Alisema pamoja na hatua hiyo, bado Menejmeneti ya kiwanda hicho inadai eka 3,000 ambazo zilichukuliwa na wananchi.

Dk. Shein aliwataka wazee wa Wilaya hiyo kufahamu sababu  hasa zilizopelekea Serikali kutoa eneo hilo la Kichwele kwa Mwekezaji huyo.

Akigusia suala la uimarishaji wa maji safi na salama katika Wilaya hiyo, Dk. Shein alipongeza juhudi zilizochukuliwa na Uongozi wa Wilaya hiyo hadi huduma hiyo kupatikana kwa asilimia 70, na kutaka juhudi zaidi zifanyike kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo ili zifikie asilimia mia moja, kabla ya mwaka 2020.

Alisema tatizo la upatikanaji wa maji katika maeneo mbali mbali ya Wilaya hiyo, ikiwemo Misufini na Bumbwini itaimarika pale visima vilivyochimbwa kwa ufadhili wa Serikali ya Ras el Hemma vitakapounganishwa.

Aidha, Dk. Shein alisema tatizo la Barabara za Matetema hadi Kazole, Mangapwani na Zingwezingwe zitashughulikiwa katika kipindi hiki, mara baada ya vifaa vya ujenzi vilivyoagizwa na Serikali kuwasili baadae mwaka huu.

Kuhusiana na changamoto ya elimu katika Wilaya hiyo na Mkoa wa Kaskazini kwa ujumla, Dk. Shein aliutaka uongozi wa Mkoa huo na  Wilaya kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuona  mikakati ipi ifanyike kuimarisha kiwango cha elimu na ufaulu kwa wanafunzi wa mkoa huo.

Aidha, aliipongeza Wilaya hiyo kwa makusanyo bora ya mapato na kuvuka kiwango kilichowekwa kwa zaidi ya asilimia mia 200.

Dk. Shein Shein ambae pia ni Mkaamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, alisema CCM imebeba dhima kubwa ya kuwatumikia wananchi, akibai isha kazi hiyo kuanza kufanyika vizuri, huku akiwaonya  baadhi ya viongozi Wilaya hiyo kwa kutofanya  vizuri.

Dk. Shein aliwataka viongozi ambao kwa namna moja au nyengine bado hawajetekeleza ahadi walizotowa kwa wananchi wakati wa kampeni kutumia kipindi kilichobaki kukamilisha ahadi zao.

Vile vile akasisitiza dhana ya kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya chama hicho, mbali na kuwepo kwa Demokrasia katika utoaji wa maoni.

Mapema, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Juma Abdalla Sadala, alizipongeza Kamatiza Siasa katika ngazi mbali mbali Wilayani humo kwa kuwafikia wanachama walio chini na kushajihisha uingizaji wa wanachama wapya.

Hata hivyo,alisema juhudi za kufanya vikao kupitia ngazi za mashina na matawi zinahitajika, hususan wakati huu kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa 2020.

Aidha,  alisema bado kuna changamoto kwa baadhi ya viongozi wa Majimbo (wabunge na Wawakilishi) Wilayani humo, kushindwa kutekeleza kikamilifu ahadi walizoweka wakati wa kampeni za uchaguzi.

Dk. Juma alisema suala la mazingira nalo ni changamoto nyengine inayoikabili Wilaya hiyo.

Nae, Mkuu wa Wilaya Kaskazini 'B' Unguja, Rajab Ali Rajab alisema Uongozi wa Wilaya kwa kushirikiana na kamati ya Ulinzi na Usalama imefanya juhudi ya kuimarisha ulinzi ili kutoa fursa kwa wananchi kutekeleza ipasavyo shughuli zao kiuchumi.

Alisema Wilaya hiyo imeimarisha huduma za kijamii kwa kuwapatia wazee 729 shilingi 5,000 kila mmoja kwa kila mwezi, sambamba na kusimamia upatikanaji wa pensheni jamii, ambapo wazee 1940 wamenufaika.

Aidha, alisema kutokana na juhudi za Uongozi wa Wilaya hiyo wananchi wamepata mwamko wa  kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji, hivyo kiwango cha uhalifu huo kushuka na kubainisha kuwa katika mwaka 2018 kesi 65 ziliripotiwa, wakati ambapo hadi hivi sasa ni kesi 7 pekee zilizoripotiwa.

Vile vile Mkuu huyo wa Wilaya, alisema kutokana na juhudi zilizochukuliwa, ukusanyaji wa mapato kupitia Halmashauri umeongezeka na kuvuka malengo ya Serikali, akibainisha katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 shilingi Bilioni 1.2 zilikusanywa, wakati ambapo katika mwaka wa fedha wa 2018/19 , hadi kufikia sasa zaidi ya shilingi Milioni 711 zimeshakusanywa.


Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.