Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Mama Mwanamwema Shein na kulia Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibaer Mhe. Riziki Pembe Juma, wakipiga makofi baada ya kuondoa kipazia kuashiria kuweka Jiwe la Msingi la Skuli ya Ng'ambwa leo , akiwa katika ziara yake Wilaya ya Kati Unguja.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amesema kuwa si muda
mrefu kisiwa cha Uzi kitafumbuka kwani Serikali anayoiongoza itahakikisha
inaimarisha huduma za maendeleo ikiwemo kujenga barabara na daraja kutoka
Unguja Ukuu Kaepwani hadi Uzi.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo katika ziara yake ya Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja wakati
alipotembelea kisiwa cha Uzi na kuweka jiwe la Msingi katika Skuli ya Maandalizi
na Msingi ya Ng’ambwa na baadae kuwahutubia wananchi wa Uzi.
Katika maelezo yake
Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina mipango
kabambe ya kuhakikisha wananchi wa Kisiwa cha Uzi wanapata huduma zote muhimu
kwa uhakika ikiwemo usafiri wa barabara, Skuli ya Sekondari pamoja na
kuimarisha huduma za masi safi na salama.
Alieleza kuwa barabara
ya Kutoka Unguja Ukuu Kaepwani hadi Uzi kwa kujengwa daraja linalokadiriwa kuwa
na urefu wa mita 400 inawezekana kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imeshatekeleza miradi mikubwa kuliko huo.
Rais Dk. Shein
aliwataka wananchi wa kisiwa hicho kufanya subira kwani Serikali itajenga
daraja hilo kuelekea usawa wa bahari hatua ambayo itawaondoshea wananchi wa
kisiwa hicho usumbufu wa usafiri wa barabara.
Aliongeza kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzbar inampango wa kukopa fedha kutoka Benki ya
Maendeleo ya ya Afria AfDB kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji katika
kisiwa hicho cha Uzi ambao utaondoa kabisa uhaba wa huduma hiyo.
Akieleza kuhusu azma
ya Serikali kuimarisha sekta ya elimu katika kisiwa hicho cha Uzi, Rais Dk.
Shein ameeleza kuwa Serikali anayoiongoza itahakikisha inajenga Skuli ya
Sekondari ya Uzi Ng’ambwa pamoja na kupeleka samani.
Aidha, Rais Dk. Shein
aliwaelezea wananchi wa kisiwa hicho juu ya suala zima la magendo
linavyofanyika katika eneo hilo alisema kuwa Serikali kupitia Kikosi chake cha
KMKM kiko macho kupambana na wale wote wanaofanya magendo.
Rais Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kukipongeza kikosi hicho cha KMKM kwa kazi nzuri inayofanya
kwani watu wamekuwa wakifanya makosa kwa kusafirisha bidhaa kama vile
unga,mchele, sukari na mafuta bila ya kufuata taratibu na sheria za nchi.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein aliwaahidi wanaCCM wa Uzi kuwa tawi lao atalizindua na kuliweka jiwe
la msingi baada ya kumaliza ujenzi wake kwa hoihoi na nderemo huku akiwataka wananchi
wa Uzi kutogombana wala kutohasimiana kwa sababu ya vyama vya siasa kwani wao
wote ni ndugu wa asili moja.
Alisema kuwa kuwepo
kwa mfumo wa vyama vingi kunatokana na mujibu wa sheria na taratibu kutokana na
Katiba ya mwaka 1984 hivyo hakuna haja ya kugombana wao wenyewe kwa wenyewe na
kuwataka wapendane na waishi kwa amani na utulivu.
Aliwaeleza wananchi
hao kuwa kisiwa cha Uzi kitapiga hatua kubwa za maendeleo iwapo wataendeleza amani na utulivu sambamba
na kuimarisha umoja wao kwani siasa ni mpito lakini damu na uasilia bado
unabaki pale pale. Aliwataka kufanya siasa bila ya kubughudhiana na kutukanana.
Mapema Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma alipongeza juhudi za Rais Dk. Shein
katika kuimarisha sekta ya elimu nchini.
Akiwa huko Uzi Rais
Dk. Shein alimtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) Mussa Ramadhan
Haji kueleza mikakati ya Serikali iliyoiweka katika kuimarisha huduma ya maji
safi na salama ambapo alieleza kuwa Mamlaka yake inachukua hatua za dharura
hivi sasa ikiwa ni pamoja na kulifanyia ukarabati tangi lililopo kwa kuliziba
ili lisipoteze maji.
Aidha, alisema
kuwa ZAWA inampango wa kuongeza
uzalishaji wa maji kwa kuongeza idadi ya visima kwani vipo baadhi ya visima
ambavyo vimeshachimbwa na vinaweza kutumika kuzalisha maji ili kusaidiana na
kisima kiliopo na kusaidia kupeleka huduma hiyo huko Uzi pamoja na kuweka
mtandao mpya wa maji katika kisiwa hicho.
Kwa upande wa Wizara
ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Mustafa
Aboud Jumbe alisema kuwa sehemu ya barabara inayotoka Unguja Ukuu
Kaepwani hadi Kisiwa cha Uzi ina urefu wa km 2 na inapita kwenye bahari ya
Hindi ambapo hali yake si nzuri.
Aliongeza kuwa
kutokana na Wizara kuliona hilo imepanga kutafuta Mshauri Mwelekezi kwa ajili
ya kulipatia ufumbuzi suala hilo ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kujenga
daraja kwenye eneo ambalo nguzo za umeme zimewekwa ambalo linakadiriwa kuwa na
urefu wa mita 400 tu kutoka kisiwa cha Uzi hadi Unguja Ukuu Kaepwani.
Alisema kuwa Wizara
imekusudia kumpatia kazi za ziada Mshauri Mwelekezi Kampuni ya Dar Al Handasah
ya Misri inayoendelea na kazi za upembuzi yakinifu, sanifu na kuandaa zabuni ya
barabara ya Tunguu-Makunduchi, Fumba-Kisauni na Mkoani Chake Chake ambapo makisio
ya kitaalamu ya gharama za ujenzi wa daraja na barabara yatajulikana baada ya
Mshauri Mwelekezi kukamilisha michoro yake.
Akiwa katika
majumuisho ya ziara yake hiyo pamoja na mazungumzo na viongozi wa CCM wa Wilaya
hiyo huko katika ukumbi wa Hoteli ya Coconut Tree, Marumbi, Wilaya ya Kati
Unguja, Rais Dk. Shein aliupongeza uongozi wa Wilaya hiyo kwa kutoa ripoti
nzuri ambayo imemridhisha.
Aliwasisitiza viongozi
wa Wilaya hiyo kuzigeuza changamoto chache zilizopo kuwa mafanikio kwa kufanya
kazi kwa pamoja na kwa mashirikiano huku akitumia fursa hiyo kupongeza
mashirikiano yaliopo kati ya uongozi wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais Dk. Shein ambaye
pia, ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar aliipongeza Wilaya hiyo ya Kati kwa
kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kupitia Wizara zote 14 za Serikali huku
akieleza azma ya Serikali ya kuzijenga barabara za Jumbi hadi Koani, Dole-Kizimbani-Miwani
hadi Kiboje, Tunguu-Ndijani na Jozani Charawe- Ukongoroni ambazo zote
zitajenwga kwa kiwango cha lami.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza changamoto ya wizi wa mazao, wizi wa kuvunja nyumba ambao alisema
ni miongoni mwa maombo ya uhalifu yaliyomo katika Wilaya hiyo ambayo yanahitaji
kukomeshwa.
Nae Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheir alieleza
hatua zitakazochukuliwa katika kuajiri wafanyakazi katika sekta ya kilimo,
elimu na afya ambapo ajira zitazingatia mahitaji ya maeneo maalum.
Rajab
Mkasaba, Ikulu
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment