Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi, Afanya Ziara Kukagua Ujenzi wa Daraja la Mwanakwerekwe Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikagua harakati za ujenzi wa Mtaro wa kupitishia maji ya Mvua yanayoingia katika Bwawa la Mwanakwerekwe.




Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alionya kwamba Serikali haitasita kumnyima kazi moja kwa moja Mkandarasi ye yote atakayeshindwa kutekeleza mradi aliyokabidhiwa ambao utakuwa haukufikia kiwango bora kinachokubalika.
Alisema kuanzia sasa Kampuni inayopewa jukumu baada ya kufanikiwa katika mchakato wa maombi ya kutekeleza Mradi wowote lazima iwe makini katika kazi hiyo.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo wakati alipofanya ziara fupi ya kuangalia harakati za ujenzi wa Mtaro wa kupitishia Maji ya Mvua yanayotoka katika maeneo mbali mbali na kuingia katika Bwawa la Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharibi “B” Mkoa Mjini Magharibi.
Alisema zipo Kampuni zilizopewa jukumu la ujenzi wa Majengo Mpya ya Skuli katika sehemu tofauti hapa Nchini  na kuyakabidhi baada ya ukamilishaji wake, lakini ndani ya kipindi kifupi majengo hayo huleta athari tofauti ikiwemo matatizo ya kuvuja kwa Majengo hayo.
Balozi Seif alitahadharisha kwamba uzembe kama huo hautavumiwa tena kwa vile unailetea hasara kubwa Serikali iliyoaminiwa na Wananchi katika kuwaletea maendeleo kupitia Miundombinu mbali mbali.
Mapema  Mhandisi Mshauri wa Mradi wa ujenzi wa  mtaro huo wa bara bara ya Mwanakwerekwe Nd. John Nyakoro alisema kutokana na kasi kubwa ya maji yanayotitirika kuingia katika bwawa hilo Wahandisi wamelazimika kujenga Makalavati Manne yatakayokidhi kukabiliala na kasi hiyo.
Mhandisi John alimueleza Balozi Seif  kwamba kwa vile Bara bara hiyo imenyanyuliwa kwa kiwango kikubwa baada ya utafiti wa kina itakuwa na uwezo wa kutumia katika misimu yote hata ule wa mvua kubwa za masika.
Alisema Kalavati hizo Nne zitakuwa na uqwezo kamili wa kupitisha maji ya mvua kwa asilimia 20/% wakati ile asilimia nyengine iliyobakia ya 86 ya Maji ya Mvua itatiririka katika mitaro mengine iliyokamilika kujengwa kwa kupelekwa maji hayo baharini.
Mhandisi John Nyakoro alifahamisha kwamba hivi sasa wanamalizia ujenzi wa kalavati ya Nne wakiwa na matumaini ya kazi hiyo kumalizika ndani ya miezi miwili iliyobakia.
Alieleza kwamba Wahandisi wa Ujenzi huo walifanikiwa kukirejesha kifusi kilichokuwa juu ya Makalavati kufuatia mvua zilizonyesa zilizonyesha jana asubuhi ambayo hazikuletaathari yoyote ile.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na Balozi Mdogo ya India aliyepo Zanzibar Bwana T C. Barual ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo yao Balozi Seif ameishukuru na kuipongeza Serikai ya India kwa jitihada zake za kusaidia harakati za Maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Balozi Seif alisema miradi ya Maji safi na Salama inayoendelea kuwekewa miundombinu wakati huo ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi kwa kuungwa mkono ya Serikali ya India, huduma za Afya, Elimu na Kilimo imeleta ustawi kwa Wananchi walio wqengi Visiwani Zanzibar.
Alitolea mfano wa Sekta ya Afya ilivyoongeza chachu ya uhusiano na Ushirikiano kati ya Zanzibar na India ambapo idadi kubwa Wagonjwa wa Zanzibar wamekuwa wakipata huduma za Afya katika Hospitali tofauti Nchini India.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba UbaloziMdogo wa India hapa Zanzibar kupitia Balozi wake kuandaa mpango Maalum wa kuwapatia Mafunzo Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na Maafisa wao.
Alisema Mpango huo endapo unaweza kusimama utawasaidia kuwajengea uwezo zaidi wa uwajibikaji Viongozi hao katika kuwatumikia vyema Wananchi katika misingi ya uwelewa mpana.
Naye Balozi Mdogo wa India aliyepo Zanzibar Bwana T.C. Barual alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba wazo lake litafanyiwa.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza kasi ya uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo baina ya India na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.