Habari za Punde

Rais Dk Shein aweka msimamo kuhusu uchimbaji mchanga

Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 18.02.2019
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema azma ya Serikali kusimamisha uchimbaji wa Mchanga imelenga kutafuta njia nzuri ya kuitumia Rasilimali hiyo chache iliyobaki kwa faida ya kizazi kilichopo na kijacho.
Dk. Shein ameyasema hayo alipofanya ziara katika maeneo yaliyokuwa yakitumika kuchimba mchanga ya Donge Chechele, Pangatupu na Kiomba Mvua ikiwa ni katika mwendelezo wa ziara zake za kukagua shughuli za Chama na Serikali.
Amesema tayari ameunda Tume inayojumuisha Mawaziri na Makatibu Wakuu ambao watakuwa na jukumu la kufikiria namna bora ya kuchimba mchanga uliobaki ili uwasaidie Wananchi wanyonge badala ya kununuliwa na Wafanyabiashara wa Viwanda vya Matofali pekee.
Kwa sasa shughuli nyingi za ujenzi zimesimama ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar ZURA  baada ya maamuzi ya Serikali kusitisha uchimbaji mchanga katika maeneo yanayochimbwa.
Dk. Shein ameelezea masikitiko yake na kusema kuwa kukosekana kwa mchanga kumechangiwa na baadhi ya Wananchi, Wafanyabiashara na baadhi ya watendaji wa Serikali kushindwa kuitumia vyema rasilimali hiyo.
Amefahamisha kuwa wapo baadhi ya Wafayabiashara waliibuka na kuanza kuuficha mchanga tani kwa tani katika maeneo yao na hivyo kuutumia kwa kuanzisha Viwanda vya Matofali.
Amefahamisha kuwa maamuzi ya kuzuia kuchimbwa mchanga yamekuja baada ya kuona mchanga unamalizwa na Wafanyabishara wasiowaaminifu wanaoununua kwa wingi na kuuficha ili kuufanya biashara.
“Hivyo tumesimamisha tupange vizuri, mchanga unamalizwa, hawa wananchi wanyonge nao wakitaka kujenga nyumba zao wataupata vipi? Nimeunda kamati ya Mawaziri na Makatibu wao ili watushauri namna nzuri ya kuutumia huo uliobaki na taarifa tutawapa wananchi wetu,” Alisema Dk. Shein.
Amesema yapo baadhi ya maeneo Zanzibar ambayo mchanga upo lakini yanatumika kwa shughuli za kilimo hivyo kunahitajika uamuzi wa busara kuchagua lipi lifanywe kwa faida ya Wananchi.
Kuhusu Mapato ameipongeza Serikali ya Wilaya ya Kaskazini B kwa kukusanya mapato vizuri kutoka Milioni 500 hadi Bilioni moja kwa mwaka jambo ambalo linapaswa kuigwa.
Dk. Shein alieleza kwamba Serikali imeanza ujenzi wa Bandari ya Mafuta na Gesi katika eneo la Mangapwani ili Meli zitakazoshusha na kupakia Mafuta na Gesi zifanye shughuli zake huko.
Amesema tayari pesa ya kutekelezea Mradi huo zipo na miundombinu imeshapangwa ambapo Wanakijiji cha Dundua, kilichopo eneo linalopakana na Bandari hiyo, wameshaanza kulipwa fidia ili kupisha Mradi huo.
Akizungumzia changamoto ya Elimu katika Mkoa huo Dk. Shein amewataka Viongozi wa Mkoa na Wilaya kukaa pamoja kutafuta mbinu za kupandisha ufaulu katika Mkoa wao.
Akizungumzia kuhusu maendeleo ya Chama Dk. Shein ameelezea kufurahishwa na mashirkiano yaliyopo kati ya Viongozi wa Chama na Serikali hali inayoashiria ushindi mkubwa katika Uchanguzi mkuu unaokoja.
Hata hivyo ameelezea  kusikitishwa na baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanaotoa kauli zinazoharibu taswira ya Chama na Viongozi wao.
“Wajumbe wa Baraza niwakumbushe tu hata kama kuna mtu hataki tena kugombea katika Uchaguzi unaokuja si vyema kusema maneno ya kuharibu taswira ya Chama, wao ni binaadam inawezekana mawazo yao yakabadilika wakataka tena kugombea wakati walishakichafua Chama, Siasa za Chama cha Labour cha Uengereza zinatofautiana na CCM” Alitanabahisha Dk. Shein.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Juma Abdallah Sadala amepongeza hatua zinazofanywa na Serikali kutekeleza vyema Ilani ya CCM ambapo kwa siku za nyuma utekelezaji wake ulikuwa zaidi ya asilimia 87%.
Kuhusu kuimarisha Chama ameishukuru Wilaya kwa kuweza kuhuisha Chama na kufanya Vikao katika ngazi ya Mashina hali ambayo imesaidia kuwa na ongezeko la Wanachama wapya 5,000.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B Rajab Ali Rajab wakati akielezea maendeleo ya Wilaya yake amesema Wilaya yake imechukua juhudi mbali mbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuwabunia Mradi wa kuwaajiri Vijana kupitia Kilimo cha Miwa na Ufugaji.
Dk Shein anaendelea na ziara yake ya kukagua shughuli Chama na Serikali ambapo amehitimisha kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na kesho anatarajiwa kuaza ziara Mkoa wa kusini Unguja. IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.