Rais wac Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akiongazana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa na Idara Maalum za SMZ,Mhe.Haji Omar Kheri, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.Mhe.Vuai Mwinyi, wakitembelea eneo la Uchimbaji wa Mchanga Pangatupu Wilaya ya Kaskazini B, Unguja,wakati wa ziara yake kuangalia eneo hilo la uchimgaji wa mchanga Jimbo la Bumbwini Shehia ya Kidazini.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amewataka wananchi
watambue kuwa kuna uhaba mkubwa wa mchanga hivi sasa hapa Zanzibar kutokana na uchimbaji
mbaya wa rasilimali hiyo unaofanyika.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo katika ziara yake ya Wilaya ya Kaskazini B Unguja wakati alipotembelea
maeneo yanayochimbwa mchanga huko Pangatupu, Chechele na Kiombamvua na kujionea
jinsi maeneo hayo yalivyoathirika kutokana na rasilimali hiyo kuanza kumalizika
kabisa.
Katika ziara hiyo
ambapo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd na Mama Mwanamwema Shein
walishiriki kikamilifu, Rais Dk. Shein aliwataka wananchi wajue uhaba uliopo wa
rasilimali hiyo ya mchanga.
Akiwa katika eneo la
Pangatupu na Chechele, Rais Dk. Shein alieleza kuwa rasilimali ya mchanga hapa
Zanzibar imeanza kutoweka na haipo hivyo kuna haja ya kuweka mikakati maalum ya
kunusuru huo mchache uliobakia ambapo tayari Serikali anayoiongoza imeshaanza
kazi hiyo.
Alieleza kuwa tayari
ameshawapa kazi Mawaziri wake watatu pamoja na Kamati yao ya Makatibu Wakuu
kufuatilia hali hiyo kwani tayari kwa upande wake hivi karibuni aliagiza
shughuli za uchimbaji wa mchanga kusisitiswa.
Aliongeza kuwa
Serikali imefanya hivyo si kama inawakomoa wananchi wake bali inatafuta
utaratibu wa kufanya ili rasilimali hiyo iwasaidie wananchi wote kwani tayari
kuna wafanyabiashara wameshahodhi mchanga katika maeneo yao ya biashara hasa
wale wanaofanya biashara ya matofali.
Rais Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kuwataka waandishi wa habari waliokuwepo katika eneo hilo
na wale waliokuwa hawapo katika ziara yake hiyo kuwaeleza wananchi ukweli juu
ya uhaba wa rasilimali hiyo ambayo wao wenyewe hali hiyo wameiona.
Akiwa katika eneo la
Kiombamvua, Dk. Shein alipata maelezo kutoka kwa uongozi wa Wizara ya Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi pamoja na kutoka kwa Sheha wa Shehia ya Kiombamvua
Mohamed Ali Ame ambaye aliomba aondolewe mchanga uliokusanyika kondeni kwake
ili aendelee na kilimo ambapo mchanga ulipelekwa na maji na jumla ya tani 2,020
zilichukuliwa na Kampuni ya CRJ kwa ajili ya matumizi ya mradi wa ujenzi wa
misingi ya maji ya mvua.
Katika majumuisho yaliokwenda
sambamba na mazungumzo na viongozi wa CCM wa Wilaya hiyo huko katika hoteli ya
“SeaCliff” Kama Wilaya ya Kaskazini B, Dk. Shein alisema kuwa wapo
wafanyabiashara wa matofali wameuficha mchanga kwenye maeneo yao hali ambayo imekuwa
usumbufu kwa wananchi wanaotaka kujenga.
Akieleza historia ya
uuzaji wa mchanga, udongo, mawe na kifusi ulivyokuwa hapo zamani, Dk. Shein
alisema kuwa kunatofauti kubwa na biashara hiyo inavyofanywa hivi sasa hali
ambayo inachangia uhaba wa rasilimali hiyo.
Alisema kuwa katika
shimo la mchanga la Pangatupu mchanga umemaliza na zimebaki tani 50,000 tu za
mchanga ambao haufiki hata miezi miwili ambapo mchanga wa CheChele nao umebaki
tani 2000 tu ambao umewekwa kwa ajili ya miradi ya Serikali.
Alisema kuwa jengo la
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) limesita
ujenzi wake kutokana na ukosefu wa mchanga na kupelekea mafundi wa ujenzi kutoka
kampuni ya Hainan International kutoka China kukaa bila ya kazi.
Alieleza kuwa licha ya
Serikali kusimamia rasilimali hiyo hivi sasa ambapo hatua hizo zilianza mnamo
mwezi Machi na Novemba mwaka jana 2017 bado kumetokea wananchi ambao wanahoji na
kusema kuwa Serikali inawachukulia mchanga wao.
Alisisitiza kuwa ni
vyema wananchi wakaelewa kuwa ardhi yote ya Zanzibar ni mali ya Serikali hivyo
rasilimali ya mchanga yote ni mali ya Serikali kwa mujibu wa Sheria na Katiba
ya nchi na yeye ndie msimamizi wa ardhi hiyo.
Pia, alieleza kuwa
jambo jengine lililochangia kwa kiasi kikubwa kutokea uhaba wa rasilimali hiyo
ni pamoja na kutofuatwa kwa sheria za nchi kwani tayari kila kitu kina sheria
yake huku akieleza kuwa baadhi wa viongozi na wananachi wa Wilaya hiyo
wamechangia kutokea kwa athari hiyo iliyopelekea uhaba wa mchanga.
Rais Dk. Shein
alieleza kuwa juhudi za makusudi zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kuzungumza na
wananchi wa maeneo yanayochimbwa mchanga yakiwemo maeneo ya Donge ambapo
aliwatuma Mawaziri wake waende kuzungumza nao ili watambue hali iliyopo hivi
sasa.
Dk. Shein alisema kuwa
Serikali imo katika kufanya utaratibu ili mchanga mchache uliopo uweze kutumika
vizuri na uwafae wananchi wote na wala haikusudii kuwasumbua wananchi wake juu
ya matumizi ya rasilimali hiyo hapa Zanzibar.
Aidha, alisema kuwa
Serikali ina kazi kubwa ya kuwaelimisha na kuwaeleza wananchi juu ya hali ya
mchanga ilivyo hivi sasa hapa Zanzibar.
Alisema kuwa wapo
baadhi ya wafanyabiashara walitaka kuruhusiwa waagize rasilimali hiyo kutoka
Tanzania Bara lakini Serikali imekataa huku akisisitiza kuwa kwa upande wa
kisiwa cha Pemba rasilimali hiyo ipo lakini bado inatosheleza kwa wananchi wa
kisiwa hicho.
Nae Katibu Mkuu wa
Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mariam Juma Abdalla Sadalla
alieleza kuwa uchimbaji chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Serikali ulianza
katika mwezi Machi 2017 katika eneo la Donge Chechele na baadae mnamo mwezi wa
Novemba 2017 kuhamia eneo la Pangatupu ambalo lilikuwa shamba la miwa chini ya
Kiwanda cha Sukari Mahonda.
Alieleza kuwa eneo la
Pangatupu lenye hekta 64 limebaki tani 50,000 tu za mchanga huku akieleza kuwa
baada ya Wizara hiyo kusimamia kiasi cha TZS Bilioni 11 zimepatika ambazo
hugaiwa kwa Halmashauri,Wizara na Hazina.
Katibu Mariam alieleza
kuwa jitihada imekuwa ikifanyika ya kupanda miti ikiwemo mikeshia na mihojoro
ambapo tayari hekta 56 zimepandwa miti ipatayo 2000 kuanzia mwaka 2016 hadi
mwaka huu wa 2019 na kueleza kuwa eneo hilo limetoa ajira 700 ambalo lina
Jumuiya mbili ikiwemo ya Madereva na Jumuiya ya Wapakizi.
Rajab
Mkasaba, Ikulu
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment