Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Aridhishwa na Utendaji Mambo ya Nje.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Dkt. Damas .D.Ndumbaro, alipofika Ikulu kujitambulisha na kufanya mazungumzo Ikulu Zanzibar.

WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepongezwa kwa kufanya kazi zake vyema katika kipindi cha miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhusiano na ushirikiano ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  alitoa pongezi hizo leo wakati alipofanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Damas Daniel Ndumbaro aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya mazungumzo pamoja na kujitambulisha kwa Rais.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alieleza kuwa licha ya kubadilishwa jina la Wizara hiyo mara kwa mara lakini bado imekuwa ikifanya kazi zake vyema na kuonesha ushirikiano mzuri wa pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hata nje ya Tanzania.

Hivyo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuendeleza uhusiano na mashirikiano hayo mema na Idara yake iliopo hapa Zanzibar ili mafanikio zaidi yaweze kupatikana kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hasa ikizingatiwa kuwa Wizara hiyo ni ya Muungano.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Wizara hiyo ina historia nzuri na tayari imejijengea heshima  na sifa kubwa ndani na nje ya Tanzania, hivyo kuna haja ya kuiimarisha kwa lengo la  kupata mafanikio zaidi.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Naibu Waziri wa Wizara hiyo kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo na kuweza kuukubali uteuzi wake huo ambao utamuwezesha kutekeleza vyema majukumu aliyopewa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Rais Dk. Shein aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi  ya Zanzibar itaendelea kuiunga mkono na kuipa ushirikiano wa aina zote Wizara hiyo kama ilivyo kwa Wizara nyengine zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa aliyonayo kutokana na uongozi na utendaji kazi wa Naibu Waziri huyo katika Wizara hiyo ambayo ni kubwa kutokana na umuhimu wake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nje ya Tanzania.

Nae Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Damas Ndumbaro alieleza kuwa Wizara hiyo ina umuhimu mkubwa sana katika kuimarisha Muungano uliopo sambamba na kuimarisha masuala  yote ya kiitifaki.

Aidha, Naibu Waziri huyo nae alieleza matumaini yake makubwa kutokana na utumishi uliotukuka wa Rais Dk. Shein katika uongozi wake hali itakayompelekea kufanya kazi zake vyema na kuweza kutekeleza lengo lililokusudiwa kwa mafanikio ya pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sambamba na hayo, Naibu Waziri huyo alimueleza Dk. Shein kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wanaridhika na utendaji mkubwa wa kazi anazozifanya Dk. Shein katika kuwatumikia wananchi wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla na kutumia fursa hiyo kumpongeza kwa juhudi zake hizo.

Hivyo, Naibu Waziri huyo alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa amepokea maelekezo na ushauri aliopewa na Rais na kumuahidi kuwa atayafanyia kazi mambo yote huku akisisitiza kuwa kipindi kirefu atajitadi kufanya kazi zake hapa Zanzibar kwa azma ya kustawisha Wizara hiyo kupitia Idara yake ya uratibu ya hapa Zanzibar.

Dk. Damas  Daniel Ndumbaro ambaye ni Mbunge wa Songea Mjini katika Mkoa wa Ruvuma aliteuliwa kushika wadhifa huo Septemba 26 mwaka jana 2018 akichukua nafasi ya Dk. Suzan Alphonce Kolimba ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Joseph Magufuli.

Rajab Mkasaba, Ikulu
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.