Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima (wa pili
kutoka kushoto) akimsikiliza Mratibu wa Kanda kutoka Baraza la Taifa Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira Bw. Godlove Mwamsojo mara baada ya kutembelea dampo lililopo
katika Kata ya Saja, Kijiji cha Itengelo Wilaya ya Wanging’ombe. Naibu Waziri
Sima ameagiza kufungwa kwa dampo hilo na kuteketeza taka zote zilizopo.
Sehemu
ya wananchi ambao wamekutwa wakiendelea na shughuli za
kutafuta bidhaa kwa ajili ya kurejereza
katika dampo lililopo katika Kata ya Saja, Kijiji cha Itengelo
Wilaya ya Wanging’ombe bila kujali madhara yao kiafya. Naibu Waziri Sima
amepiga marufuku wananchi kuingia kiholela katika dampo hilo na kumwagiza
Mkurugenzi wa Mji wa Makambako kufunga dampo hilo na kuteketeza taka zote ndani
ya siku sitini.
Na
Lulu Mussa.-Njombe
Halmashauri ya Mji wa
Makambako Wilayani Njombe imeagizwa kusitisha mara moja utupaji wa taka ngumu
katika dampo lililopo katika Kata ya Saja, Kijiji cha Itengelo Wilaya ya
Wanging’ombe kutokana na kutokidhi matakwa ya Sheria ya Mazingira na malalamiko
yaliyotolewa na wananchi katika vijiji vya jirani.
Agizo hilo limetolewa hii
leo Mkoani Njombe na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira
Mhe. Mussa Sima mara baada ya kufanya ziara ya kikazi na kumuagiza Kaimu Mkurugenzi
wa Mji wa Makambako Bw. Rashid Hozi kutafuta eneo maalumu litakalokidhi
mahitaji husika ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya athari kwa mazingira
Akiwa katika eneo hilo la
dampo la Makambako ambalo kwa hivi sasa liko katika Wilaya ya Wanging’ombe, Mhe
Sima ameshuhudia wananchi wakiingia kiholela katika dampo hilo kwa ajili ya
kuokota bidhaa mfano chupa za plastiki kwa ajili ya kuziuza.
“Serikali inatumia pesa
nyingi katika huduma za afya ni wakati sasa tupunguze mzigo huu kwa magonjwa
yanayoweza kuepukika kwa kuwa na mazingira safi na salama. Kuanzia sasa ni
marufuku wananchi kuingia dampo kuokota chupa za plastiki, hii inahatarisha
afya zao wenyewe, hivyo utaratibu wa kutenganisha taka uanzie katika vyanzo vya
uzalishaji” Sima alisisitiza.
Awali Mratibu wa Kanda wa Baraza
la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira
(NEMC) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Bw. Godlove Mwamsojo amesema kuwa
Baraza limetoa notisi ya siku sitini (60) kuanzia tarehe 01/02/2019 kwa
Halmashauri hiyo ya kusitisha utupaji wa taka katika eneo hilo na kuwaagiza
kuteketeza taka zote zilizopo katika kipindi kilichotajwa.
Bw. Mwamsojo amesema kuwa
Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, kifungu cha 119 kinazitaka Mamlaka za
Serikali za Mitaa kutafuta namna bora ya kuteketeza taka ngumu katika maeneo
yao na kuainisha kuwa dampo hilo kwa sasa liko katika eneo la mwinuko hivyo
kipindi cha mvua hutiririsha maji ambayo si salama kwa wakazi wa maeneo ya
chini.
Wakati huo huo, Naibu
Waziri Sima pia amemuagiza Mratibu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi
wa Mazingira (NEMC) kuhakikisha anafuatilia utekelezaji wa agizo hilo na endapo
Halmashauri haitatekeleza agizo hilo hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi
yao .
Kwa upande wake Kaimu
Mkurugenzi wa Mji wa Makambako Bw. Rashid Hozi amekiri kupokea barua ya Baraza
la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira na kuahidi kutekeleza maagizo
yaliyotolewa kwa muda muafaka.
Naibu Waziri Mussa Sima,
yuko katika ziara ya kikazi katika mikoa ya Nyanda za juu Kusini kuainisha
changamoto za kimazingira katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kukagua mitambo ya kuteketeza taka hatarishi
katika Hospitali, kujionea hali ya madampo katika mikoa husika endapo utaratibu
wa kutenganisha taka unazingatiwa ili kuzuia wananchi kuzifuata baadhi ya
bidhaa zinazo rejerezeka katika maeneo ya dampo kwa lengo la kudhibiti milipuko
ya magonjwa.
Katika
Mikoa ya Njombe, Mbeya na Iringa Mheshimiwa Sima pia atapata fursa ya kuembelea
kwenye ikolojia ya vyanzo vya maji vinavyo changia
maji katika bonde la Rufiji.
No comments:
Post a Comment