Habari za Punde

BOT kula sahani moja na wanaozitumia fedha kama mapambo


NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.

BENK Kuu ya Tanzania (BOT) imesema kuwa inakusudia kupeleka sheria bungeni, ili kuweza kuwekea thamani zaidi fedha ya Tanzania, ambayo kwa sasa imekuwa ikitumiwa vibaya katika mashuhuli.

Akifungua mkutano wasiku moja uliowashirikisha masheha, madiwani na kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kaskazini Pemba, Afisa Mdhamini Wizara ya Fedha na Mipango Pemba, Ibrahim Sale Juma alisema sheria hiyo itaweza kumbana mtu yoyote atakaeweza kuitumia vibaya fedha hiyo.

Alisema Mtindo wa fedha kutumika katika maholi ya sherehe kama mapambo, mavazi mwilini, kuzikanyaga chini ni uvunjifu wa sheria, kwani sheria zipo na zinaongoza na kuelekeza namna gani ya kuzitumia fedha hizo.

“Kumekuwa na mtindo siku hizi wananchi kuzitumia wanavyotaka fedha zetu, sasa sheria ikipita basi mtu asije akaona anaonewa pale itakapomtia hatiani, asije akasema ameonewa lengo ni kuiwekea ulinzi zaidi na heshima fedha yetu ambayo ni tunu pekee ya Taifa”alisema.

Mdhamini Ibrahim alisema BOT haijatoa ruhusa ya fedha, kuzitumia kama kuzivaa mwilini au kuzikanyaga au kutengeneza shati na koti, kwani kufanya hivyo ni kuivunjia hadhi na heshma fedha ya taifa.

Aidha alisema kuwa fedha inavyotumika vibaya hupelekea uharibifu wa kutokutumika tena fedha hizo, kuingia sokoni na kuweza kuingia katika mzunguruko wa fedha na kupelekea, kuitia hasara BOT katika kuchapisha fedha nyengine mpya.

“Elimu hii ya matumizi na umuhimu wa kuitunza fedha zetu ni jambo zuri kupatiwa, tunaishukuru SMT na SMZ kwa maamuzi yake na leo tunapewa elimu, jumuku letu sasa kuitunza na kuilinda fedha yetu”alieleza.

Aidha aliwataka wananchi kuhakikisha wanazilinda na kuzitunza fedha hizo, masheha ndio wenye wananchi aliwataka kuhakikisha,  wanatoa elimu kwa wananchi wao pale wanapowapa vibali vya kufanya sherehe juu ya matumizi ya fedha.

Meneja msaidizi idara ya mawasiliano kwa umma kutoka BOT, Victoria Msima alisema bot inajukumu la kutekeleza sera ya fedha na kusimamia masoko yote ya fedha nchini na taasisi za kifedha, ikiwemo kuchapisha na kusambaza fedha.
Alisema haipendezi kuona wananchi wanazitumia fedha vibaya, kwa kuzitengenezea mapambo, nguo, kuzikanyaga chini, kufanya hivyo ni kuishushia hadhi fedha ya taifa.

“Fedha ni tunu ya taifa kama ilivyo bendera ya nchi, huwezi kuifanya vyovyote na kuitumia vibaya bendera ni kosa la jinai sawa sawa na fedha, wajibu wetu kuwa makini katika matumizi ya fedha zetu”alisema.

Aidha aliwataka wananchi kuhakikisha wanazitunza noti za 
Taifa, kwani BOT sasa imeanza kufuatilia matumizi yote ya fedha, ikiwemo wanaozitumia vibaya ili kuwatia hatiani na kuwa fundisho kwa wengine.

Akiwasilisha mada ya sarafu afisa kutoka BOT Restituta Magnus, alisema benk inafanya kazi kubwa ya kusambaza fedha zote, kwa kushirikiana na benk za biashara zilizopo nchini.

Alisema tayari elimu ya matumizi ya fedha hizo na ugunduzi wa fedha ambazo sio halali, tayari imeshatolewa kwa wananchi wote wakiwemo makundi maalumu ya watu wenye ulemavu.

Wakichangia katika kikao hicho Zulfa Abdalla Said, alisema wanawake wa mkoa wakaskazini Pemba wanalaani Vikali kitendo kilichofanywa na wanawake wenzao, kuzitumia fedha kama mapambo katika shuhuli mbali mbali.

Alisema wakati umefika kwa viongozi wakamati ya Ulinzi na usalama Zanzibar, kufanya uchunguzi juu ya tukio lililotokea na kuenea katika mitandao ya kijamii, kutumika fedha kama nguo na muhusika kumchukulia hatua za kisheria, ili kuwa fundisho kwa wengine, kwa lengo la kuiwekea heshima fedha ya Tanzania.

Sheha wa selimu Ali Khatib Chwaya, aliitaka BOT kuandaa sheria kali kwa wale wote watakaobainika kuitumia vyeba fedha ya taifa na kuweza kuwatia hatiani, pale watakapobainika kwani fedha ndio alama tosha kwa taifa lolote duniani.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.