Habari za Punde

Dk Mabodi ataka Muungano kuenziwa kwa vitendo

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi akishangiliwa na Wanafunzi wa Skuli ya Kidagoni ya wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.
 WANAFUNZI wa Skuli ya Maandalizi,Msingi na Kati ya Kidagoni Wilaya ya Kaskazini ‘A’  wakiwa katika skuli hiyo kwa ajili ya hafla ya kukabidhiwa vifaa vya wanafunzi zikiwemo sale,viatu,mikoba ya kuhifadhi madaftari pamoja na mabembea na Jumuya ya Vijana wapenda maendeleo ya CCM Zanzibar.
  NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Kidagoni mara baada ya kukabidhi vifaa na zawadi mbali mbali kwa wanafunzi wa skuli ya Kidagoni.
 MWENYEKITI wa Jumuiya ya Vijana wapenda maendeleo Mwinyi Ahmed Mwinyi (wa kulia wa mwanzo aliyenyanyua shungi la sale ya wanafunzi wa kike) akikabidhi vitu mbali mbali vilivyotolewa na jumuiya hiyo kwa uongozi wa skuli hiyo.
VIONGOZI wa Jumuiya ya Vijana wapenda maendeleo pamoja na Walimu wa Skuli ya Kidagoni na wanafunzi wa maandalizi wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kupokea vifaa vya skuli zikiwemo Sale,viatu na mikoba ya kuhifadhi madaftari.By Haji Mohd
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi amesema muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni tunu ya taifa inayotakiwa kuenziwa kwa vitendo na wananchi kutokana na kuimarika kwa nyanja za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kimaendeleo.
Rai hiyo ameitoa  katika hafla ya kutoa vifaa vya skuli kwa wanafunzi wa skuli ya Kidagoni Wilaya ya Kaskazini 'A'  Unguja vilivyotolewa na Jumuiya ya Vijana wapenda maendeleo wa CCM, amesema muungano huo licha ya kuunganisha nchi mbili umeenda mbali zaidi na kuwaunganisha watu wa pande zote mbili kiundugu, kidamu na kijamii.
Alisema hakuna kiongozi, taasisi wala mtu wa kuvunja muungano huo uliodumu kwa miaka 55 toka kuasisiwa kwake.
Alieleza kwamba wapo baadhi ya viongozi wa kisiasa wamekuwa na kauli zisizofaa za kubeza tunu hiyo iliyowaunganisha wananchi wa nchi mbili na kuishi kwa amani na utulivu.
Alisema wakati umefika wa wananchi wa wilaya hiyo ya Kaskazini 'A' hasa shehia ya Kidoti na vitongoji vyake kupuuza maneno ya ulaghai yanayotolewa na vyama vya upinzani na badala yake kuthamini juhudi za kimaendeleo zinazotekelezwa na Serikali chini ya usimamizi wa CCM.
Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 alisema Chama Cha Mapinduzi kimeendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa mijini na vijijini ili wanufaike na Sera imara zinazosimamiwa na CCM.
Katika maelezo yake Dk.Mabodi alifafanua kwamba maendeleo yaliyofikiwa nchini yametokama na misingi imara ya kiuongozi, kiitikadi na kimfumo iliyoasisiwa na waasisi wa Mapinduzi ya 1964,Muungano 1964 pamoja na waasisi wa TANU na ASP.
Katika hafla hiyo ya ugawaji wa vifaa kwa wanafunzi wa skuli hiyo Dk. Mabodi amesema CCM itatoa itatoa mabati ya kuezeka Kituo cha Afya cha Ndagoni pamoja na ujenzi wa choo, kuchangia shilingi milioni 2.5 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa madarasa matano ya skuli hiyo ya mandalizi, msingi na kati pamoja na vifaa mbali mbali vya kutumia maskulini kwa wanafunzi watakaofaulu michipuo.
Aidha aliongeza kuwa ataikumbusha Serikali kuu pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini 'A'  kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la ukosefu wa barabara, umeme na umaliziaji wa kituo cha Afya.
"CCM inapoahidi inatekeleza kwa wakati na hakuna jambo lolote lililowahi kushindikana mbele yetu, nakuombeni muendelew kuwa pamoja na Chama Cha Mapinduzi kwani ndio taasisi pekee inayozunguka usiku na mchana kuratibu matatizo yenu na kuyatatua kwa wakati", alisema Dk. Mabodi.
Pamoja na hayo aliongeza kwamba kwa mujibu CCM ilivyotekeleza Ilani yake visiwani humo, hakuna mtu yeyote wa kuzuia ushindi wa kishindo wa CCM  mwaka 2020 kama ilivyosisitizwa katika ibara ya Tano ya Katiba ya Chama ya mwaka 1977.
Akizungumza Mwenyekiti wa Jumuiya ya   Vijana wapenda maendeleo ya CCM Mwinyi Ahmed Mwinyi alisema lengo la kutoa vifaa hivyo kwa wanafunzi ni kuunga mkono juhudu za Serikali na CCM katika kuisaidia jamii ya wananchi wa kijiji cha Ndagoni.
Alisema fedha za kununua vifaa hivyo zumetokana na michango mbali mbali ya vijana wazalendo wa CCM ambao ni wanachama waliounda jumuiya hiyo kwa kutoa fedha za mishahara yao ili isaidie jamii katika masuala ya elimu.
Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni sale za wanafunzi wa ngazi zote za skuli hiyo, viatu, mikoba, mabati, mabembea ya kisasa kwa ajili ya wanafunzi wa maandalizi pamoja na mabati ya kuezekea majengo ya skuli hiyo.
Katika risala ya skuli hiyo iliyosomwa na Mwl. Neema Othman Khamis aliishukru Jumuiya hiyo kwa maamuzi yake ya kuwasaidia vifaa wanafunzi wa skuli hiyo na kueleza kuwa wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa na jumuiya zingine nchini.
Alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni upungufu wa madarasa, ukosefu wa barabara, ukosefu wa vifaa vya masomo ya ICT zikiwemo komputa.
Naye Mwakilishi wa Jimbo Mhe. Ame Haji Ali alisema ametekeleza masuala mbali mbali ya kimaendeleo katika kijiji hicho na vijiji jirani vikiwemo kuimarisha huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama, huduma za Afya, vikundi vya ujasiriamali zikiwemo Sacoss kwa ajili ya akina mama pamoja na kuimarisha sekta ya michezo kuwapatia vijana vifaa vya michezo katika ligi mbali mbali za jimbo hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.