Habari za Punde

Kamati ya Kukabiliana na Maafa Waklutana.

Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar imekutana kutafakari hali halisi ya Mvua za masika zinazoendelea kunyesha Nchini na kuleta athari chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabilana na Maafa Zanzibar Nd. Makame Khatib Makame Akitoa Taarifa ya awali juu ya athari za Mvua za masika zilizonyesha siku tatu mfululizo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed akichangia Taarifa kwenye Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar.
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud akichangia Taarifa kwenye Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar.
Mkurugenbzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar Mohamed Ngwali akitoa taarifa ya hali ya mvua za masika zinazoendelea kunyesha Nchini.
Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mh. Mahmoud Thabit Kombo akichangia Taarifa kwenye Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar.

Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar wamekutana leo kutafakari hali halisi ya Mvua za masika zinazoendelea kunyesha Nchini ambazo tayari zimeshaleta maafa kwa baadhi ya Wananch hasa wale wanaoishi katika maeneo hatarishi.
Kikao hicho kilikutana chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na kufanyika katika Ukumbi wa Ofisi yake uliopo Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Akitoa Taarifa ya awali juu ya athari za Mvua hizo Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabilana na Maafa Zanzibar Nd. Makame Khatib Makame alisema Nyumba elfu 2,120 zimeathirika kutokana na Mvua na upepo mkali Unguja na Pemba.
Nd. Makame alisema athari hizo zimesababisha kujeruhiwa kwa Wananchi Watatu ambapo Wawili kati yao waliongukiwa na ukuta wa nyumba huko Chuwini Wilaya ya Magharibi  na Mmoja kuangukiwa na Mnazi baada ya kung’oka kufuatia upepo mkali huko Makoongwe Wilaya ya Mkoani Kisiwani Pemba.
Alisema athari zilizojitokeza kufuatia tathmini hiyo ni pamoja na upotevu wa mali za Wananchi, kujaa kwa maji na kusababisha wananchi husika kuhifadhiwa na Jamaa zao, kufurika kwa Makaro  ya Maji machafu, kutomoka kwa mashimo pamoja na kubomoka kwa miundombinu ya bara bara.
Akitoa taarifa ya hali ya mvua za masika zinazoendelea kunyesha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar Mohamed Ngwali alisema kiwango cha Mvua kilichonyesha Tarehe 5 Mei  katika uwanja wa ndege wa Zanzibar pekee kilifikia Milimita 167.2 kwa saa 24.
Nd. Ngwali alisema kiwango hicho ni kikubwa ikilinganishwa na mvua ya Milimita 115.3 iliyoripotiwa Mwezi mei mwaka 2018 wakati kwa upande wa kisiwa cha Pemba kiwango cha mvua cha Tarehe 5 mei kilifikia milimita 105.3 kilichoripotiwa katika uwanja wa ndege wa chake chake.
Mkurugenbzi Mkuu huyo wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar aliwaeleza Wajumbe wa Kamati hiyo kwamba kikawaida mvua zinapopindukia milimita 50 kwa saa 24 mara nyingi huleta athari.
Wakichangia taarifa hizo Wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar walizikumbusha taasisi zinazohusika kuchukuwa hatua ya kuyahifadhi maeneo hatarishi yakiwemo mabonde na njia za asili kama ilivyoshauriwa na Kamati ta Sekriterieti ya Kukabiliana na Maafa.
Wajumbe hao walisema Taarifa zinapaswa kutolewa katika kipindi hichi zikiwemo kuwanasihi Wananchi wazingatie ushauri wa wataalamu wa afya katika dhana nzima ya kujiepusha na maradhi ya kuambukiza kutokana na kuvurugika kwa miundombinu mbali mbali ikiwemo ile ya maji.
Walisema pamoja na mambo mengine ni jambo la msingi kuwafariji Wananchi waliojitolea kuwahifadhi Jamaa zao waliopatwa na athari kutokana na Makaazi yao kukumbwa na maafa ya mafuriko.
Hata hivyo wajumbe hao walisisitiza umuhimu wa Kamati za Maafa ya Shehia na Wilaya kuendelea kutoa elimu kwa Wananchi kuyakimbia maeneo hatarishi ambayo bado yanaonekana kutoa muelekeo wa athari zaidi za maafa endapo Mvua zitaendelea kunyesha katika kipindi hichi.
Akiahirisha Kikao hicho Mwenyekiti wa  Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwaagiza Viongozi wa Wilaya na Halmashauri za Wilaya kuwazuia Wananchi kutojenga katika maeneo ya wazi na yale hatarishi ili kujiepusha mapema na matatizo ya maafa.
Balozi Seif alionya kwamba ipo tabia ya baadhi ya viongozi wanashuhudia hatua za baadhi ya Wananchi kujenga maeneo hayo bila ya kuchukuwa hatua zozote za kisheria na matokeo yake kuibebesha mzigo Serikali wa kulipa fidia jambo ambalo halitavumiliwa kwa sasa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Serikali inazingatia njia muwafaka za kuchukuwa katika kukabiliana na maafa yatakayotokezea iwapo mvua za masika zitaendelea kunyesha la kuleta athari zaidi.
Kikao hicho  cha Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar kilikuwa cha dharura kutokana na hali halisi iliyojitokeza kutokana na siku Tatu mfululizo za mvua kubwa ya Masika zilizonyesha na kuleta athari kubwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.