Habari za Punde

Wafanyabiashara Mkoani Tanga Watakiwa Kuacha Kupandisha Bei za Bidhaa Katika Kipindi Hichi Cha Mwezi wa Ramadhani

WAFANYABIASHARA mkoani Tanga wametakiwa kuacha kupandisha bei za bidhaa hususani za vyakula kwenye kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani ikiwemo kuwa na moyo wa huruma kwa wale watakaofunga kwani ni mwezi wa toba ambao waumini hujinyima kwaajili ya watu wengine.
Hayo yalisemwa na Katibu wa Hamasa na Chipukizi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoani Tanga Waziri Mohamed wakati akizungumza na waandishi wa habari kipindi hiki cha mfungo mtukufu wa mwezi wa ramadhani.
Alisema kuwa mwezi wa ramadhani ni kipindi ambacho waumini humrudia Mwenyezi Mungu kwa nguvu zote hivyo sio kipindi cha wafanyabiashara hao kujinufaisha kwa watu wanaofunga kwani waumini wamekuwa wakijidunduliza ili kusaidia wasiojiweza lakini wafanyabiashara hao wanaona ni fursa ya kujinufaisha.
 “Hiki ni kipindi ambacho wanawasaidia watu mbalimbali kwa nguvu zao zote, sasa akamsaidie mtu mwingine na wakati huo huo akusaidie wewe ambaye unataka kujinufaisha kwa manufaa yako mwenyewe ukijua kabisa kwamba hiki ni kipindi maalum cha kumrudia Mwenyezi Mungu lakini pia ndugu zangu kwenye tuongeze ibada,tupendane ikiwemo kutembelea wagonjwa“Alisema
Katibu huyo aliwasihi wafanyabiashara kuacha kuongeza bei bei ya vyakula mbalimbali huku akiwaomba ikiwezekana washushe bei za vyakula ili kuweza kupata thawabu kwenye kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtufuku wa ramadhani.
Aidha aliwatakia mfungo mwema wa mwezi wa Ramadhani Waislamu wote Tanzania pamoja na wale waumini wa dini mbalimbali watakaosindikiza mwezi huo na kumuomba mwenyezi Mungu atupe baraka kutokana na mwezi huo ndani ya Mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla.
Hata hivyo pia aliwataka makatibu wote wa hamasa na chipukizi wilaya za mkoa huo kuendelela kushikamana ikiwemo kuchangamkia fursa za kimaendeleo zilizopo kwenye maeneo yao ili ziweze kuwa na tija kwao na jamii zinazowazunguka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.