Habari za Punde

Watanzania Waombwa Kushirikiana na Taasisi ya VPN Kusaidia Vijana Kupata Elimu.


Mwenyekiti wa Vipaji Promotion Network (VPN), Haji is Mrisho (kulia) akimkabidhi zawadi ya saa Naibu Meya wa Temeke, Juma Rashid wakati wa hafla hiyo. 
Sehemu ya watoto wanaofadhiliwa na Vipaji Promotion Network (VPN) wakifuatilia matukio yaliyokuwa yakiendelea katika hafla  fupi iliyoandaliwa na taasisi  ya Vipaji Promotion Network (VPN) kwa lengo la kuchangia vijana wenye vipaji ili kuwawezesha kusoma, ambayo iliambatana na tukio la kufutarisha lilifanyika Mei 25, 2019 jijini Dar es Salaam.


 Mmoja wa kinamama washiriki wa hafla hiyo akitoa mchango wake wa mawazo ili kuboresha taasisi hiyo ili iwe na uwezo wa kusaidia vijana wengi zaidi.Na. Mbaraka Kambona,
Mwenyekiti wa Mtandao huru (VPN) wa kubaini na kuwafadhili vijana wenye vipaji  lakini familia zao hazimudu kuwasomesha, Haji Mrisho amewaomba watanzania kuunga mkono jitihada za taasisi hiyo ili kusaidia vijana hao kupata elimu  nchini.

Mrisho alitoa wito huo Mei 25, 2019 jijini Dar es Salaam katika hafla  fupi iliyoandaliwa na taasisi hiyo ya Vipaji Promotion Network (VPN) kwa lengo la kuchangia vijana wenye vipaji ili kuwawezesha kusoma, ambayo iliambatana na tukio la kufutarisha.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2015 mpaka sasa wameshafanikiwa kuwapeleka shule watoto tisini na nne (94) ambao wako katika shule zilizopo mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Kigoma na Tabora.

Mrisho aliendelea kusema kuwa  lengo la taasisi hiyo ni kupeleka shule watoto Mia moja (100) kila mwaka, hivyo alitoa wito kwa watanzania wenye mapenzi ya kusaidia watoto kusoma wajitokeze kuunga juhudi zilizoanzishwa na VPN.

“Serikali peke yake haiwezi kufanya kila kitu, niwaombe ndugu zangu watanzania wajitoe na kuungana na sisi katika harakati hizi za kumkomboa kijana, kwani kijana akiachwa tu mtaani bila kusaidiwa anaweza kujiingiza katika makundi yasiyofaa na ikawa ni hasara kwa jamii na taifa pia”, alisema Mrisho

“Lakini vijana pia wanaopata fursa hii ya kusoma wahakikishe wanaitumia vyema kwa manufaa yao na kwa taifa, wajue kuwa  hili ni deni kwao kwa kuwa jamii inajitolea rasilimali zao ili wao wasome na kuja kuiendeleza nchi yao”, aliongeza Mwenyekiti huyo

Pamoja na mafanikio hayo waliyofikia mpaka sasa, Mrisho hakusita kueleza changamoto wanazopata ikiwa ni pamoja na ufinyu wa bajeti, na pia taasisi hiyo kutofahamika vizuri  kwa watanzania walio wengi kwa  kuwa bado ni changa.

Katika hatua nyingine, Naibu Meya wa Halmashauri ya Temeke, Juma Rashid  Mkenka  ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi akimuwakilisha Meya wa Temeke alisema kuwa  kazi inayofanywa na taasisi hiyo ni kubwa sana hivyo wasiifanye peke yao peke yao, wapanue wigo kwa kushirikisha wadau wengi zaidi ili wapate uwezo wa kusaidia vijana wengi.

“Tanzania kuna wadau wengi sana wanaopenda kusaidia katika eneo la elimu, hivyo mfanye jitihada za kuimarisha ushirikiano na wadau hao ikiwemo Serikali ili muweze kupanua wigo wa kuwasaidia vijana wengi zaidi nchini”, alisema Naibu Meya huyo

Aidha, Mwenyekiti wa VPN alisema kuwa mipango yao ya baadae ni kuwa na uwezo wa kuchukua vijana wenye vipaji nje ya masomo ifikapo mwaka 2020, pia kuwa na shule ya sekondari ya VPN ifikapo mwaka 2025 na kuwa na chuo kikuu ifikapo 2035.

Vipaji Promotion Network (VPN) ni Mtandao huru unaojiendesha bila faida ambao ulioanzishwa  mwaka 2015 na vijana wa kitanzania kwa  lengo la kuwabaini na kuwafadhili vijana wenye vipaji lakini familia zao hazimudu kuwasomesha vijana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.