Habari za Punde

Wazazi wahimizwa kupeleka watoto wao Madrasa

Na. Husna Sheha,Zanzibar.
WAZAZI na walezi wametakiwa kuwahimiza watoto wao kwenda madrasa, ili kupata elimu ya duniani na akhera.
Wito huo umetolewa na Ukhty Zuleikha Khamis Kombo, katika mashindano ya kuhifadhi qur-an yaliofanyika katika ukumbi wa Majid  Kiembesamaki, Zanzibar.
Alisema iwapo watoto watajikita zaidi kuisoma na kuifahamu elimu ya qur-an, wataweza kujiepusha  na  mambo machafu, hivyo ni vyema  wazazi kuwasimamia ili kuachana na vishawishi ili kuwajengea mustakbali mwema wa maisha yao.
Hata hivyo, aliwasihi walimu kuzidisha jitihada ya kuwafundisha wanafunzi wao kuhifadhi Qur-an ili kuweza kuiendeleza dini ya kiislamu, kwani ndio muongozo hapa duniani na kesho akhera .
“Qur-an  huwatoa watu katika kiza na kuwaweka katika muangaza, hivyo wazazi  wasiwe nyuma katika kuwahimiza watoto wao kuhudhuria katika madrasa naipongeza Jumuiya ilianzisha mashindano haya” alisema .
Nae, Ukhti Mwanakhamis Ahmada Said, amesikitishwa na changamoto ya baadhi ya matajiri kushindwa kuchangia katika mashindano hayo na amewataka kujitokeza kutoa sadaka, ili kuweza kuendeleza mbele mashindano hayo.
Pia amewapongeza washiriki wa mashindano hayo, kwa kuweza kuhifadhi Qur-an katika vifua vyao na kuisoma na  amewataka  waendelee kujifunza na kuipenda, ili kuweza kuzipata fadhila wao pamoja na wazazi wao kwani mwenye kuipenda anaibeba  bendera  ya uislamu.
Nae, Msimamizi wa Mkuu wa Kamati ya kuhifadhisha Qur-an Zanzibar, Ukhti Saada Muhammad Nassor , amesema kuwa   lengo kuu la Jumuiya hiyo ni kuijenga jamii katika kuhifadhi Qur-an na  kuitumikia dini ipasavyo, ambao ndio mwenendo wa mtume wetu Muhammad (S.A.W ),ili waifuate sunna ya mtume huyo.
Amesema mashindano ya kuhifadhi Qur-an yameanzishwa mwaka 1992 na kuasisiwa rasmin 2003, hadi sasa imetimiza miaka 27, tangu kuanzishwa mashindano hayo, ambapo jumuiya imeweza kupata fursa ya kushiriki katika mashindano mbali mbali ya kuhifadhi Qur-an ndani ya nchi na kutoka nje ikiwemo    Saudia rabia.
Amesema kuna mpango wakuyaimarisha zaidi kwa mwaka ujao ili kufikia hatua ya kuhifadhi Msahafu mzima, kwani hivi sasa imefanikiwa kuwakuza wanafuzi 200 ambapo wameingia katika mashindano kwa mwaka huu.
Hata hivyo Ukhti Saada amesikitishwa na hali ya mahudhurio ya watu katika mashindano hayo, kuwa wanashiriki watu wachache na amewataka kujitokeza kwa wingi.
Jumla ya wanafunzi 12 wa juzuu 10 walishiriki, ambapo mwanafunzi  Asila Mwalim Said mwenye umri wa miaka 14 kutoka Zanzibar, ameshinda nafasi ya kwanza na amepata alama 99.5 na kupewa zawadi ya fedha shilingi 250,000 taslim, na vitu vyengine mbali mbali.
Mshindi wa pili ni Aisha Suleiman Ali, mwenye umri wa miaka 16  kutoka Zanzibar, ambae alipata alama 99 ,na kupewa  shilingi 200,000 taslim na vitu vyengine, na mshindi wa tatu  Idhat Omar Ali, mwenye umri wa miaka (9) kutoka Zanzibar  alipata alama  98.5 na alizawadiwa  fedha shilingi 150,000 taslim na vitu mbali mbali.
Juzuu 20 mshindi wa kwanza ni Mwaine Ali Hamad, mwenye umri wa miaka 16 ambae alipata alama 99.8 , alizawadiwa fedha taslim shilingi 350,000 na vitu mbali mbali,  mshindi wa pili  ni Rahma Salum Juma mwenye umri wa miaka 13 kutoka Zanzibar alipata alama 99.5 alizawadiwa fedha shilingi 300,000 taslim na vitu mbali mbali.
Mshindi wa tatu  Sumaiyya Said Hamad mwenye umri wa miaka 14  kutoka Zanzibar, ambae alipata alama 97.5  alizawadiwa fedha shilingi 250,000 taslim pamojana vitu mbali mbali.
Upande wa juzuu 30, mshindi wa mwanzo Bimkubwa Kassim Mohammed, mwenye umri wa miaka 14 kutoka Zanzibar ambae alipata alama 100 alizawadiwa fedha shilingi 700,000 taslim pamoja na vitu vyengine.
Nafasi ya pili ni Sara Yussuf Ali, mwenye umri wa miaka 12 kutoka Zanzibar  ambae alipata alama 99.8  amezawadiwa fedha shilingi 600,000 taslim na vitu mbali mbali, na mshindi wa tatu Munawwara mkubwa Juma mwenye umri wa miaka 17 kutoka Zanzibar,  amezawadiwa  fedha shilingi 500,000 taslim na vitu mbali mbali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.