Habari za Punde

Wazazi watakiwa kuipa kipaumbele elimu ya maandalizi

 Wazazi, walimu wa Skuli za maandalizi, madrasa na vyuo vya Qur,aan, Masheha na Watu Mashuhuri wakiwa katika Ukumbi wa Skuli ya Maandalizi Madungu

 Afisa WEMA Idara ya Maandalizi Msingi na Vyuo vya Qur-an Ukhti Amina Salum Khalifan akizungumza na Wazazi, walimu wa Skuli za maandalizi, madrasa na vyuo vya Qur- an, Masheha na Watu Mashuhur katika Ukumbi wa Skuli ya Maandalizi Madungu.
Mkurugenzi idara ya Maandalizi na Msingi Bi Safia Ali Rijali akizungumza na Wazazi, walimu wa Skuli za maandalizi, madrasa na vyuo vya Qur- an, Masheha na Watu Mashuhuri katika Ukumbi wa Skuli ya Maandalizi Madungu.NA Ali Othman , Pemba

Mkurugenzi idara ya Maandalizi na Msingi Bi Safia Ali Rijali amewataka wazazi kuhakikisha kwamba watoto wanaanza elimu ya maandalizi kwa umri sahihi uliopendekezwa.

Bi Safia ameyasema hayo katika ukumbi wa Skuli ya Maandalizi Madungu, wakati akizungumza na Wazazi, walimu wa Skuli za maandalizi, madrasa na vyuo vya Qur- an, Masheha na Watu Mashuhuri kutoka katika shehia mbali mbali ambazo zimebainika kuandikisha idadi ndogo ya wanafunzi.

Amesema baada ya kutembelea baadhi ya shehia hizo amebaini kwamba, wapo wazazi ambao kutokana na sababu mbali mbali huacha kuwaandikisha watoto wao katika elimu ya maandalizi licha ya watoto hao kufikia umri sahihi wakuandikishwa

Aidha, Bi Safia amewataka wazazi kushirikiana kikamilifu katika malenzi  na kutenga muda wa kukaa na watoto na kuwahimiza kusoma,  akiwaasa baadhi ya mababa kuacha tabia ya kuwaachia wanawake swala la malezi kwa kisingizio cha kutokua na muda.

Akizungumzia swala la afya  Bi Safia amewataka wazazi kujali afya za watoto na kuhakikisha kwamba wanawapatia chakula bora na kuchukua hatua stahiki dhidi ya ukatili wanaotendewa watoto katika jamii.

Wakati huo huo Afisa WEMA Idara ya Maandalizi Msingi na Vyuo vya Qur-an Ukhti Amina Salum Khalifan amewataka Wazazi, walimu wa Skuli za maandalizi, madrasa na vyuo vya Qur- an, Masheha na Watu Mashuhuri kuhakikisha kwamba wanawasimamia vyema watoto ili wawe  raia wema baadae.

Shehia ambazo zimebainika kuandikisha idadi ndogo ya wanafunzi ni Birikau, Furaha, Kwale, Pembeni, Uwandani, Kilindi Wilaya ya Chake Chake na Chokocho, Michenzani, Mkanyageni, Shidi, Mtuhaliwa, na Makoongwe kwa wilaya ya Mkoani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.