Habari za Punde

Rais Dk Shein Afungua Mkutano Mkuu wa Nne wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC)

                            
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia Mkutano Mkuu wa Nne wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Zanzibar, uliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar. 


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali inatambuwa kuwa kuwepo kwa vyama vya wafanyakazi nchini, kunaendana na sheria na Katiba ya Zanzibar ya 1984 pamoja na mikataba ya kimataifa.

Dk. Shein amesema hayo katika ufunguzi wa Mkutano mkuu wa nne wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), uliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Mjini hapa.

Pamoja na mambo mengine mkutano huo wa siku mbili umepanga kufanya Uchaguzi mkuu wa kuwapata Viongozi wapya wataohudumu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Dk. Shein alisema Serikali inatambua kuwa wafanyakazi na vyama vya wafanyakazi ni kundi muhimu  Ulimwenguni  na ili mafanikio yaweze kupatika kazini, ni lazima pawepo wafanyakazi walio tayari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, nidhamu, uadilifu na uzalendo katika mazingira bora.

Alisema kutokana na hali hiyo Serikali imekuwa ikiridhia mikataba mbali mbali ya Kimataifa pamoja na kutunga sheria na kanuni zinazohusiana na masuala ya wafanyakazi.

“Yote hayo yanafanywa kwa madhumuni ya kufikia malengo na kuhakikisha wafanyakazi wanatimiza majukumu yao katika mazingira yalio bora zaidi pamoja na kulinda maslahi yao ”, alisema.

Alisema Serikali imekuwa na mazingatio maalum juu ya wafanyakazi kwa kutambuwa kuwa wanahusiana moja kwa moja na ukuaji wa uchumi, ukiwa ndio msingi wa ustawi wa maisha ya wananchi.

Dk. Shein alisema Serikali inazingatia umuhimu wa  kuimarisha ushirikiano uliopo na Vyama vya wafanyakazi kupitia ZATUC, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020, Ibara ya 139.

Aidha, Dk. Shein aliipongeza Jumuiya ya Waajiri Zanzibar (ZANEMA) kwa kuwa na ushirikiano mkubwa na Serikali, hivyo kurahisisha ushughulikiaji wa changamoto mbali mbali  zinazowakabili wafanyakazi.

“Nikupongezeni viongozi nyote wa Shirikisho mnaomaliza muda wenu wa uongozi, hakika sote tunathamini kazi yenu kubwa na nzuri mliyoifanya katika kulitumikia Shirikisho hili muhimu katika kipindi chote”, alisema.

Akigusia Historia ya Vyama vya Wafanyakazi nchini, Dk. Shein alisema kuwa ilipitia katika hatua mbali mbali, ambapo vyama hivyo vilitowa mchango mkubwa kwa wananchi katika harakati za kupigania uhuru, kupinga ubaguzi na unyonyaji dhidi ya wanyonge.

Akitowa mfano, alisema kuundwa kwa chama cha ‘Zanzibar and Pemba Federation of Labour’ kulichangia sana kuwaunganisha wafanyakazi, kuhamasisha kazi za ujenzi wa taifa na kupigania ustawi bora wa maisha ya wananchi, baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964.

Alisema mnamo mwaka 1952 hadi 1957 Hayati Mzee Abeid Amani Karume alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mabaharia Zanzibar (Zanzibar Seamen Union), ambapo alishirikiana an viongozi wa vyama vyengine katika kudai haki na kuondoa madhila.

Akizungumzia kuhusiana na uchaguzi wa viongozi wakuu wa Shirikisho hilo, Dk. Shein alisema ni haki kwa wajumbe wenye sifa kushiriki kwa uwazi pamoja na kuwachaguwa wagombea waliojitokeza baada ya kujiridhisha kuwa wana sifa na uwezo wa kuwatumikia wafanyakazi.

“Napenda nisema kuwa si kila mtu anaweza kuwa kiongozi, kiongozi anatakiwa awe na sifa maalum, hususan za uadilifu na aliye tayari kuwatumikia wengine, hivyo ni vyema mkachaguwa viongozi bora na wenye uwezo”, alisema.

Aidha, alisistiza kwa kuwataka wajumbe kutokufanya makosa ya kuwachaguwa vongozi walioweka mbele maslahi yao binafsi au wenye kutafuta uongozi kwa njia za hadaa, kwani hatua hiyo inaweza kuwagharimu wafanyakazi.

Aliwataka kuchaguwa viongozi watakaokuwa kioo cha shirikisho , akibainisha kuwa viongozi hao  ni wale wanaojitambuwa na kuwa mfano bora wa utendaji wa majukumu, kauli zao na waliojipamba kwa maadili mema.

“Wanaohitaji kuongoza ni lazima watambuwe kuwa wanabeba dhamana ya kuwatumikia wafanyakazi na wajibu wa kuongoza ni kuonyesha njia na kuyafikia malengo,  lakini pia ni vyema wakaelewa jukumu walilonalo la kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wafanyakazi”, alisema  .

Akinasibisha na kauli yake, Dk. Shein alisema ZATUC inahitaji kuwa an viongozi wenye ushawishi katika kuwaongoza wafanyakazi kuelekea kwenye mafanikio pamoja na kuzingatia maslahi yao.

Aidha,  aliwataka wajumbe watakaochaguliwa kushika nyadhifa mbali mbali kutumia hazina kubwa ya uzoefu kutoka kwa viongozi waliotangulia pamoja na kupata ujuzi na ushauri kutoka kwao.

Alisema kuna umuhimu kwa wajumbe  kuendeleza umoja na mshikamano uliopo kabla ya uchaguzi na baada ya uchaguzi, akitahadharisha kuwa sio jambo jema kuibuka makundi kati ya wagombea walioshinda na wale  walioshindwa.

Aliwahakikishia wajumbe hao kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wapya watakaochaguliwa ili kuendeleza mafanikio yaliofikiwa na kufikia malengo ya kuanzishwa kwa Shirikisho hilo.

Nae, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Moudline Castico, alisema serikali itaendelea kuwashughulikia kisheria Waajiri wasiofuata sheria na miongozo ya Serikali katika kuwapatia stahiki za wafayakazi wao.

Aliwataka wajumbe wanawake kujitokeza na kugombea nafasi mbali mbali za Uongozi wa shirikisho hilo ili kuendeleza mafanikio yaliofikiwa.

Mapema, Katibu Mkuu wa ZATUC Khamis Mwinyi Mohamed aliipongeza Serikali kwa kukubali uanzishaji wa sheria mbali mbali zinazohusiana na wafanyakazi nchini.

Aliipongeza Serikali kwa kuviwezesha vyama vya wafanyakazi kufanya shughuli zake bila bughudha sambamba na hatua yake ya kuto nyongeza za mishahara kila baada ya kipindi, sambamba na mishahara hiyo kupatikana kwa wakati.

Alisema katika kipindi hicho (miaka mitano iliyopita), ZATUC kwa kushirikiana an Serikali imekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji na ustawi wa uchumi wa Zanzibar.
Aidha, aliipongeza Serikali kwa kuridhia mikataba mbali mbali ya Kimatifa pamoja na mikakati mbali mbali ya vipaumbele na kiufundi vya Shirika la Kazi Duniani (ILO).

Katika hatua nyengine, akitowa salam kutoka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Dk. Yahya Msigwa aliipongeza ZATUC kwa kuendeleza uhusiana na ushirikiano na TUCTA hivyo kupanuwa wigo wa mafanikio ya wafanyaakzi nchini.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.