Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akikabidshiwa Cheti Maalum Kwa Kazi Nzuri na Shukari kwa Uongozi wake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi, kilichotolewa na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Zanzibar, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma Zanzibar, iliofanyika katika ukumbi wac Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.
UONGOZI wa Ofisi ya Rais na Utumishi wa Umma na Utawala
Bora kwa kushirikiana na Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) umetakiwa kuandaa
programu maalum ya mafunzo ya muda mfupi kwa ajili ya Viongozi, Watendaji Wakuu
na Watumishi wengine wa Serikali.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi
wa kongamano la maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma Zanzibar yaliyofanyika
katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul wakil, Kikwajuni mjini Zanzibar.
Katika hotuba yake
hiyo, Rais Dk. Shein alisema kuwa programu
hiyo ya mafunzo ya muda mfupi kwa ajili ya viongozi hao yana lengo la kuongeza ufanisi katika Utumishi wa Umma ili
wapate masomo ya kuwakumbusha majukumu yao na kuweza kuwahudumikia vyema
wananchi.
Rais Dk. Shein katika
hotuba yake hiyo alieleza kuwa ubunifu ni muhimu katika utumishi wa Umma na ndio
utakaowafanya watumishi kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Alisisitiza kwamba
bila ya kuwa wabunifu Zanzibar inaweza
kubaki nyuma katika karne hii ya sayansi na teknolojia ambapo kwa bahati mbaya
miongoni mwa watumishi wapo wachache ambao ni wagumu kubadilika katika kutimiza
majukumu yao ya utumishi.
Aliongeza kuwa
watumishi wa aina hiyo ni lazima wabadilike na wahakikishe wanakwenda na kasi
ya kutoa huduma zilizo bora na kutoa nasaha zake za kuhakikisha watumishi
wanakuwa wabunifu wa kutafuta njia bora, rahisi na nzuri ya kuwatumikia
wananchi ambao ndio waajiri.
Rais Dk. Shein alisema
haja ya kuwepo kwa Chuo cha Utumishi wa Umma ambacho kutokana na mahitaji
maalumu ya kitaalamu, maadili, fikra, mawazo na tabia zinazohitajika kwa wafanyakazi
katika sekta ya umma nchi zote duniani zina vyuo maalum vya kutoa mafunzo
maalum kwa watumishi wa umma.
Alieleza kuwa utumishi
wa Umma ulio bora ni chachu muhimu katika kuongeza kasi ya maendeleo hapa
nchini kiuchumi na kuuimarisha ustawi wa jamii hasa kwa kutambua kuwa utumishi
wa Umma ni kigezo muhimu cha misingi ya Utawala Bora.
Alieleza furaha yake
jinsi ya watumishi wa Umma wanavyowahudumia wananchi na kuwapongeza wafanyakazi
wote nchini na kueleza kwamba mwamko umebadilika na watumishi wengi
wanazingatia umuhimu wa kuwatumikia wananchi kwani wao ndio wenye nchi na
wanaoiweka Serikali madarakani.
Rais Dk. Shein alisistiza
haja ya kuendelea kufanya kazi kwa kujiamini na kutofanya kazi kwa gati gati
kwani watumishi wanaujuzi, wanajua na wanaweza kutekeleza vyema kazi zao na
kusisitiza kutofanya kazi kwa mazoea na kuwataka kuwa wabunifu.
Alisisitiza haja ya
kuwepo kwa mabadiliko kwa kila yule anayepewa dhamana kwa lengo la kuimarisha
Utumishi wa Umma.
Akieleza juu ya ujumbe
wa mwaka huu usemao “ Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
Uwajibikaji na Ubunifu ndio chachu ya Maendeleo katika kuimarisha Utumishi wa
Umma”, na kueleza kuwa iwapo ujumbe huo utazingatiwa na kufanyiwa kazi
mabadiliko makubwa yatapatikana na kusisitiza haja ya kuufanyia kazi kwa vitendo
ujumbe huo.
Alieleza haja ya Taasisi
inayoshughulikia Serikali Mtandao kuwaelimisha wananchi pamoja na kuwaelisha
watumishi wa Umma Serikalini na kwenye taasisi nyengine maana ya Serikali
Mtandao na madhumuni yake kwani unarahisiha utendaji wa kazi.
Aliitaka Taasisi hiyo Kuwaeleza
wananchi juu ya huduma gani wanazipata hasa ikizingatiwa kuwa Serikali imetoa
mamilioni ya fedha kwa ajili ya Serikali Mtandao huo.
Rais Dk. Shein
aliwataka viongozi na watumishi wa Umma kufanya kazi kwa mashirikiano ya pamoja
huku akieleza kuwa Serikali inapiga vita suala la rushwa na uhujumu wa uchumi
na ndio maana kuna Sheria maalum juu ya suala hilo na kueleza umuhimu wa
maadili kwa viongozi .”maadili ndio chachu ya kutoa mwelekeo wa kuongoza watu”,
alisisitiza Dk. Shein.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa katika kuendeleza juhudi za kuhakikisha kwamba viongozi wa umma
wanashikamana na maadili ya umma sambamba na kuwajibika kwa uwazi na kwa
kuzingatia misingi ya sheria, kwa lengo
la kutoa huduma bora kwa wananchi.
Alisema kuwa Serikali
iliunda Tume ya Maadili ya viongozi wa Umma Zanzibar ambayo ina jukumu la
kutekeleza na kusimamia Sheria ya Maadili ya viongozi wa Umma, namba 4 ya mwaka
2015 ambapo pia, inawataka viongozi wote wa Umma kujaza na kurejesha Fomu ya Tamko
la Mali na Madeni..
Alieleza kuwa jumla ya
viongozi 16,20 walijaza fomu na kuzirejesha katika mwaka 2016/2017 na viongozi 1,664
walifanya hivyo katika mwaka 2017/2018 na katika mwaka 2018/2019 jumla ya
viongozi 1,727 walitimiza wajibu wao huo wa kisheria.
Nae Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman aliahidi
kuendelea na jitihada za kuimarisha utumishi wa Umma hapa nchini na kutumia
fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa uongozi wake bora na jinsi anavyowajali
watumishi wa Umma.
Alisema kuwa kwa
upande wa Zanzibar tokea mwaka 1964 masuala ya Utumishi wa Umma utekelezaji
wake ulianza lakini mageuzi makubwa yametokea mwaka 2010 katika uongozi wa Rais
Dk. Shein baada ya kafanywa mageuzi na kufanya programu maalum ya matumizi ya
Utumishi wa Umma ikiwa ni pamoja na Sera, Sheria na Kanuni ambayo yote hayo ni
matunda ya Rais Dk. Shein.
Alisema kuwa mageuzi
hayo yametokea na kuundwa kwa Wizara maalum kamili ya Utumishi wa Umma huku
akitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa taasisi kuhakikisha inawapa stahiki
zao wale wote wanaomaliza masomo.
Alieleza kuwa Zanzibar
ina Awamu Saba na kila awamu imefanya mambo yake makubwa lakini katika suala la
Utumishi wa Umma maabadiliko makubwa ya watumishi yamefanyika kuanzia mwaka
2010, ambapo katika hotuba zake Dk. Shein alikuwa akisema kuwa atahakikisha
watumishi wa Umma anawawekea mazingira bora.
Aidha, Rais Dk. Shein
aliwatunuku vyeti Katibu Mkuu wa Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Abdulhamid Yahya Mzee, Haji Omar Kheir;Waziri wa Mwanzo katika Wizara ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora pamoja na Waziri Haroun Ali Suleiman.
Pia, wakati huo huo
Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd alimkabidhi Cheti maalum Rais Dk.
Shein kutokana na kazi nzuri aliyoifanya na shukurani kwa uongozi wake
uliotukuka sambamba na mchango mkubwa wa kuimarisha sekta ya Umma uliopelekea
kuwepo kwa ufanisi.
Nae Naibu Waziri Ofisi
ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dk. Mary Machuche Mwanjelwa alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kufanya maadhimisho hayo kwani yana faida nyingi
kwa utumishi wa Umma.
Alieleza kuwa kwa
upande wa Tanzania Bara katika kuadhimisha wiki hii Ofisi yake ilikukutana na watumishi
wa Umma kwa kuangalia wametoa huduma zao vipi kwa watumishi hao na kufanya
maonyesho ambayo ndio sehemu ya watumishi wa Umma na kukutana kwa pamoja na
kuona mrejesho wake na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea.
Alieleza kuwa maadhimisho
hayo ya Siku ya Utumishi wa Umma Zanzibar pia, ni sehemu ya kuuenzi Muungano
uliopo ambao umeasisiwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na Hayati Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Nae Katibu Mkuu Ofisi
ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Yakuti Hassan Yakuti alieleza kuwa
maadhimisho hayo yana lengo la kukuza ushirikiano na nchi kadhaa za Afrika.
Alisema kuwa nchi za
Afrika kila mwaka huanzimisha siku hii kila ifikapo tarehe 23 Juni ya kila
mwaka kwa kutambua mchango wa watumishi wa umma katika nchi husika.
Alisema kuwa Maadhimisho
hayo kwa upande wa Tanzania yalianza mwaka 2003 baada ya kukubaliwa na Umoja wa
Afrika ambapo Tanzania iliainisha kama ilivyo kwa nchi nyengine ikiwa ni pamoja
na kuandaa makongamano na kuonekana haja ya kuanzishwa hapa Zanzibar mwaka huu.
Katibu Mkuu huyo
alieleza kuwa kuanzia mwakani kuanzia tarehe 17 Juni hadi 23 kwa kushirikiana
na Taasisi zote za Serikali na kuomba kuzikumbusha Wizara na Taasisi zote za
Umma kujiandaa mapema kwa ajili ya shughuli hii ambayo itakwenda sambamba na
maonyesho, makongamano na kutoa tunzo kwa watumishi waliofanya vizuri katika
kazi.
Katika kongamano hilo
mada mbali mbali zilitolewa ikiwa ni pamoja na mada isemayo, Mafanikio
yalipatikana katika Utumishi wa Umma Zanzibar, Mchango wa Chuo cha IPA katika
Utumishi wa Umma Zanzibar, Mchango wa Srikali Mtandao katika Utumishi wa Umma
Zanzibar na Uwajibikaji katika Utumishi wa Umma.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment