Habari za Punde

Naibu Waziri Mhe.Kanyasu Aiagiza TFS Idhibiti Wachimbaji Wadogo wa Madini Kupitia Maeneo ya Uchimbaji Katika Shamba la Miti la Biharamulo - Chato.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akizungumza na wachimbaji wadogo katika eneo la Mataba ndani ya Shamba la miti la Biharamulo- Chato linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania( TFS) kuhusu umuhimu wa kufuata sheria na taratibu za kuchimba madini ndani ya Hifadhi hiyo katika mkoa Geita. 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ameiagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS)  kupitia  Menejimenti ya  Shamba la Miti la Biharamulo- Chato mkoani Geita idhibiti  upanuzi wa  Uchimbaji madini unaofanywa na Wachimbaji wadogo  nje ya yale maeneo ambayo yanatambulika  kwa shughuli hiyo katika Shamba hilo.

 Aidha, Mhe.Kanyasu ameiagiza TFS idhibiti uanzishwaji wa  makazi mapya pamoja na ukataji ovyo wa miti unaoendelea  hadi pale Kamati ya Mawaziri nane itakapotoa ripoti iliyokuwa imeundwa na Rais John Pombe Magufuli kufuatia maombi yaliyokuwa yamewasilishwa na  wilaya ya Chato kupitia Mbunge wao, Dkt. Medard Kalemani ya kuomba ardhi yenye ukubwa wa hekta 25 nje ya hifadhi hiyo  ili  kuwawezesha Wachimbaji hao kuanzisha makazi yao ya kudumu.

Hatua hiyo inakuja kufuatia  uwepo wa leseni saba zilizotolewa na Wizara ya madini na kati ya hizo saba ni leseni moja tu ndo ambayo  imeshalipiwa kibali cha kufanya shughuli hiyo ndani ya Shamba hilo

Agizo hilo amelitoa leo wakati akizungumza na wachimbaji  wadogo wapatao 2000  katika eneo la Matabe ndani ya Shamba hilo, na kuwataka  Wachimbaji hao wafuate sheria na taratibu zinazotakiwa za kuchimba madini ndani ya shamba hilo.

Katika shamba hilo  Wachimbaji wadogo wamekutwa wakiendelea kuchimba dhahabu  katika eneo la Matabe, Ilyamchele na Nyantimba  ambapo wengi wao wakiwa hawana leseni wala kibali cha kuchimba kutoka TFS.

Amewataka Wachimbaji hao wajiunge katika vikundi visivyopungua watu watano ili waweze kukidhi vigezo vya kupewa leseni na badaye 
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) itoe kibali cha kuwawezesha  kufanya tathmini katika maeneo ya leseni hiyo.

Amesema kitendo cha Wachimbaji hao kukosa vibali vya kuchimba madini ndani yua Shamba hilo  kunaikosesha serikali mapato kwa vile hawatambuliki.

Aidha, Mhe.Kanyasu amewaonya wachimbaji hao kuacha tabia ya kukata miti ovyo  kwa ajili ya shughuli za machimbo pasipo kuomba kibali kutoka TFS

"Tutakapokubaini unakata  miti kwa ajili ya machimbo tutachukua sheria kali dhidi yako kwa kulipa faini au jela miaka miwili" alilisitiza Kanyasu.

Kwa upande wake Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Madini, Dkt.Medard Kalemani amewaeleza Wachimbaji hao kuwa nia ya serikali sio kutaka kuwafukuza ila inawataka wafuate sheria na taratibu ili waweze kutambulika na serikali

"Serikali inataka ninyi Wachimbaji wadogo mnufaike wakati huo huo Serikali nayo inufaike hivyo lazima mjiunge kwenye vikundi ili mtambulike kisheria.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Chato, Mhandisi.Mtemi  Msafiri amewaonya Iponya Nybihabi wanaodai kuwa wao ndo wamiliki wa leseni  waache kuwasumbua Wachimbaji wadogo kwani ofisi yake haiwatambui

Kufuatia malalamiko mengi kutoka Wachimbaji wadogo kuwalalamikia Wachimbaji hao  Wakubwa,   Mkuu wa  wilaya hiyo alilazimika kumuamuru Mkuu wa Polisi kuwakamata Wachimbaji hao wakubwa na kisha kuondoka nao.

Naye ,Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo, Emanuel Juang amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa licha ya kusumbuliwa mara kwa mara na Wachimbaji Wakubwa katika eneo la Mataba lakini wapo tayari kufuata sheria na taratibu zinazotakiwa ikiwemo suala kununua miti kwa TFS kwa ajili ya uchimbaji madini.


Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini ambao wanaendesha shughuli zao za  uchimbaji madini katika Shamba la miti la Biharamulo-Chato wakinyoosha mikono juu ikiwa ni ishara  kukubali maagizo aliyayatoa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu kuwa wanapaswa kufuata taratibu na sheria za uhifadhi wakati wanapochimba madini ndani ya hifadhi hiyo ya Misitu mkoani Geita.
Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa madini Dkt.Medard Kalemani  akizungumza na wachimbaji wadogo katika eneo la Mataba ndani ya Shamba la miti la Biharamulo- Chato linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania( TFS) kuhusu umuhimu wa kufuata sheria na taratibu kabala ya kumkaribisha Naibu Waziri Mhe, Kanyasu kuzungumza nao.
Baadhi ya Wachimbaji wadogo wa madini ambao wanaendesha shughuli zao za  uchimbaji madini katika Shamba la miti la Biharamulo-Chato  wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu kuhusu umuhimu wa kuunda vikundi vya wachimbaji madini ili serikali iweze kuwatambua na  wawe na leseni na kisha waombe kibali kutoka TFS.
Mkuu wa wilaya ya Chato. Eng. Mtemi Msafiri akizungumza na wachimbaji wadogo katika eneo la Mataba ndani ya Shamba la miti la Biharamulo- Chato linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania( TFS)  kuwa hakuna Wawekezaji watakaowasumbua wakati wa kuchimba madini yao kwa sasa hadi pale trakapowapa taarifa rasmi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe, Constantine Kanyasu akizUngumza na baadhi ya watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wa kanda ya Ziwa wanaosimamia Shamba la Miti la Biharamulo- Chato kabla ya kutembelea eneo la Mataba ambako Wachimbaji wa madini wamezuiwa kuanzisha makazi mapya pamoja na kuongeza maeneo ya uchimbaji mbali na yale waliyopo kwa sasa katika mkoa wa Geita.
 ( Picha na Wizara ya Maliasili na Utalii)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.