Waziri wa Kilimo,Maliasili,Mifugo na Uvuvi (kushoto) akichangia katika mkutano wa Wizara hiyo wa utekelezaji wa malengo ya mpango kazi kwa kipindi cha Julai 2018-Juni 2019 na mpango kazi wa mwaka 2019-2020 uliofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati)
[Picha na Ikulu.] 26/08/2019.
RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza
haja kwa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuongeza kasi katika
kufanya utafiti kwani sekta zote za Wizara hiyo zinagusa chakula ambacho ndio
maisha ya mwanaadamu.
Hayo aliyasema leo, Ikulu mjini Zanzibar
alipokutana na uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wakati
ilipowasilisha Mpango Kazi wa Julai 2018
hadi Juni 2019 sambamba na Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa mwaka 2019/2020.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa suala zima la utafiti lina umuhimu mkubwa kwani tayari hivi sasa Serikali ina taasisi tatu za utafiti ikiwemo, Taasisi ya Utafiti wa Afya, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo.
Alieleza haja ya kuendelea kuzitumia taasisi za
kilimo kwani zina umuhimu mkubwa na ndio maana akafanya jitihada za kuzianzisha
na kusisitiza haja ya kuendeleza tafiti kwani ndio nguzo na nyenzo kubwa ya
Wizara hiyo.
Alieleza kuwa Chuo cha Kilimo cha Kizimbani
(KATI), hivi sasa kimeiunganishwa na SUZA, hivyo ni vyema wakakiimarisha na
kutokiwacha mkono kwani bado kinahitaji mchango kutoka kwa uongozi wa Wizara
hiyo.
Alisisitiza kuwa bado kilimo kina nafasi katika
Uchumi wa Bahari (Blue Economy) na kueleza kuwa Serikali ya Mpinduzi ya
Zanzibar imo katika mpango wa kuandaa Idara itakayoratibu Uchumi wa Bahari hapa
Zanzibar.
Alisema kuwa kwa mara ya kwanza Wizara hiyo
imepata fedha nyingi katika Bajeti yake ambapo hizo zote ni jitiha za Serikali
pamoja na jitihada za Wizara hiyo
akisisitiza Wizara hiyo ieleze mafanikio makubwa iliyoyapata yakiwemo
mafunzo.
Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd ambaye
alishirikia kikamilifu mkutano huo kwa upande wake alitoa pongezi zake kwa na
kusisitiza suala zima la uzalishaji wa vifaranga vya samaki ili wananchi wengi
walioamua kufanya kazi hiyo wafaidike.
Pia, alieleza haja ya kuwepo kwa mradi wa
kuzalisha vifaranga vya kuku kwani hivi sasa vifaranga vya kuku vingi vinaagizwa
kutoa nje ya nchi huku akisisitiza haja ya kuzalisha viungo vya chakula kwa vingi
kwani masoko yapo sambamba na suala la ajira kwa vijana.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza kazi nzuri ya uwasilishaji
iliyofanywa na Wizara hiyo huku akisisitiza haja kwa uongozi kuendeleza mafunzo
kwa wafanyakazi pamoja na kuendeleza uadilifu.
Nae Mshauri wa Rais wa Zanzibar Pemba, Dk. Maua
Abeid Daftari alipongeza azma ya Wizara hiyo kuliimarisha zao la halizeti
ambalo alisema lina mapato mazuri na kusisitiza haja ya kuendelezwa utafiti
katika maeneo ya Matangatuwani na Weni kisiwani Pemba.
Mapema Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uuvi Mmanga Mjengo Mjawiri akisoma
muhtasari wa Wizara hiyo alisema kuwa
Wizara imelenga kuendeleza mageuzi katika sekta ya kilimo kwa kukifanya kilimo
kiwe cha kisasa, jumuishi na chenye ushindani.
Ambapo kwa maelezo ya
Waziri Mjawiri sekta ya kilimo inachangia katika sekta ya viwanda na utalii ili
kuleta tija na maisha bora ya wananchi wa Zanzibar na maendeleo ya uchumi kwa
ujumla.
Alisema kuwa kilimo
ikijumuisha mazao, mifugo, uvuvi, misitu na rasilimali zisizorejesheka bado ni
mhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar ambao
asilimia 40 ya wananchi wamejiajiri kwenye sekta hii na inakadiriwa zaidi ya asilimia
70 ya wananchi wanategemea kilimo ambapo mwaka 2018 kimechangia pato la taifa la
asilimia 21.3.
Waziri Mjawiri alieleza
malengo na mikakati elekezi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2018/2019 ikiwa ni pamoja
na kukamilisha utaratibu wa Chuo cha Kilimo Kizimbani (KATI) Zanzibar kujiunga
na Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) pamoja na
ununuzi wa meli mbili.
Aidha, alieleza
mafanikio yaliopatikana mwaka 2018/2019
ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa mpunga, kuongeza uzalishaji wa miche
ya mikarafuu, kuzindua kampeni ya kuendeleza zao la nazi, kuzalisha vifaranga
240,000 vya majongoo bahari pamoja na kuanza kwa mradi wa ujenzi wa miundombinu
ya umwagiliaji maji.
Sambamba na hayo, Waziri
Mjawiri alieleza kuwa kufuatia ziara ya Rais Dk. Shein nchini Indonesia aliyoifanya
Agosti, mwaka 2018 uongozi ulipata kuona aina mpya ya mwani wenye thamani ambao
Zanzibar unapatikana pamoja na kutayarishwa kwa Makubaliano mawili ya Masharikiriano
katika sekta ya kilimo na uvuvi.
Nao viongozi hao
walieleza jinsi walivyonufaika baada ya kuona ufugaji unaofanywa na Kampuni ya ufugaji
ya Al Rawabi ya Dubai ambako walikwenda kujifunza uwekezaji katika uzalishaji
wa maziwa ambapo pia, Rais Dk. Shein aliwahi kuitembelea Kampuni hiyo katika
ziara yake ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) aliyoifanya Januri 2018.
Akisoma taarifa ya
utekelezaji wa Mpango Kazi wa Wizara hiyo, Katibu Mkuu wake Mariam Juma Abdalla
Saadalla alieleza mikakati ya kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi
sambamba na kuhifadhi rasilimali zisizorejesheka.
Katibu Maariam alieleza
kuwa upatikanaji wa fedha nyingi ambazo zimetokana na msukumo wa Rais na
muongozo wake umepeelekea uwezo na kuongeza ufanisi katika Wizara hiyo pamoja
na kuwepo kwa miradi kadhaa ambayo wataweza kuitakeleza ikiwemo kujenga
maghala, kununua meli inayosarifu samaki, kujenga Viwanda vya samaki Unguja na
Pemba pamoja na kujengwa mabwawa ya kufugia samaki.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment