Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene akiwasilisha
azimio la Itifaki ya ziada ya Nagoya - Kuala Lumpur juu ya
uwajibikaji wa kisheria na fidia kwa madhara yanayoweza kutokea kutokana na
matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa mbele ya Bunge hii leo
mjini Dodoma. Ni itifaki
itakayosaidia juhudi za kuhifadhi
mazingira na matumizi endelevu ya bioanuai kwa kutambua madhara yanayoweza
kutokea katika afya ya binadamu, mazao au bidhaa zilizofanyiwa mabadiliko ya
kijenetiki kwa njia ya bioteknolojia ya kisasa.
Na. lulu mussa
Bunge la Tanzania hii leo limeridhia Itifaki ya ziada ya Nagoya - Kuala
Lumpur juu ya uwajibikaji wa kisheria na fidia kwa madhara yanayoweza kutokea
kutokana na matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa.
Akiwasilisha azimio Bungeni Dodoma,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) George
Simbachawene amesema kuridhiwa kwa Itifaki hiyo, Tanzania itaimarisha ushirikiano na Nchi
Wanachama katika kusimamia na kutekeleza masuala yanayohusu bidhaa au mazao
ambayo yanatoka nje ya Nchi.
Aidha, imebainika kuwa Itifaki ya Nagoya – Kuala Lumpar
itasaidia juhudi za kuhifadhi mazingira
na matumizi endelevu ya bioanuai kwa kutambua madhara yanayoweza kutokea katika
afya ya binadamu, mazao au bidhaa zilizofanyiwa mabadiliko ya kijenetiki kwa njia
ya bioteknolojia ya kisasa.
Simbachawene
amesema kuwa Itifaki hii itaongeza upatikanaji wa fursa za kujenga uwezo wa
wataalam nchini katika kusimamia
matumizi salama ya bioteknolojia ya kisasa na kusimamiwa na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira
ya mwaka 2004 na Kanuni za Usimamizi wa Matumizi Salama ya Bioteknolojia ya
Kisasa ya Mwaka 2009.
“Itifaki
ya Nagoya – Kuala Lumpar itasaidia kuimarisha uhifadhi wa mazingira, kulinda
afya ya binadamu na wanyama dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi ya
bioteknolojia ya kisasa” alisisitiza Simbachawene.
Akiwasilisha
maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Makamu
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Kanali (Mst) Masoud Ali Khamis ameishauri Serikali kuzipitia
Sheria za nchi ambazo zitaenda sambamba na malengo ya Itifaki kwa kuhakikisha
nchi inanufaika.
Itifaki ya Ziada ya Nagoya - Kuala
Lumpur kuhusu uwajibikaji kisheria na fidia kwa madhara yanayoweza kutokea
kutokana na matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa ilianzishwa ili kuwezesha utekelezaji
wa Itifaki ya Cartagena inayohusu Matumizi Salama ya
Bioteknolojia ya Kisasa ilipitishwa na Nchi Wanachama wa Mkataba wa Hifadhi ya
Bioanuai Mwaka 2000 ambapo Tanzania iliridhia Itifaki hii mwaka 2003.
No comments:
Post a Comment