Habari za Punde

Hutuba ya Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar SUZA Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein,


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar(SUZA) Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akisoma ya Cheti cha Ithibati kilichotolewa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), wakati wa hafla hiyo ya kusherehekea mafanikio ya SUZA toka kuazishwa kwake Zanzibar mwaka 1999 -2019, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein Tunguu SUZA


HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN AMBAE PIA NI MKUU WA CHUO KIKUU CHA TAIFA CHA ZANZIBAR (SUZA) KATIKA HAFLA YA KUSHEREHEKEA MAFANIKIO YA CHUO KIKUU CHA TAIFA CHA ZANZIBAR TANGU KUANZISHWA KWAKE
 TAREHE: 14 SEPTEMBA, 2019.

Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali,

Mheshimiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi,

Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri Mliopo,

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja,

Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya

Mheshimiwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Taifa
Cha Zanzibar,

Makamo Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar,

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar,

Waheshimiwa Mabalozi

Ndugu Viongozi na Watendaji mbali mbali wa Serikali mliohudhuria,

Ndugu Wahadhiri na Wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar,

Ndugu Wanachuo,

WageniWaalikwa,

Mabibi na Mabwana.
  
Assalam Aleikum

Kwa hakika, sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu Mtukufu Subhanahu Wataala aliyeumba mbingu na ardhi na vyote  vilivyomo. Tunamshukuru Mola wetu kwa kutujaalia neema ya uhai na afya njema tukaweza kujumuika kwenye mkusanyiko huu, kwa lengo la kusherehekea mafanikio mbali mbali yaliyopatikana katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001. Miongoni mwa mafanikio mengi yaliyopatikana ni pamoja na Chuo chetu kuweza kuthibitishwa na kutambuliwa katika kusomesha masomo ya Udaktari kwa Shahada ya Kwanza na Shahada ya Pili.

Ni jambo kufurahisha sana kuwa sherehe hizi, zimesadifu kufanyika katika mwezi  huu wa Septemba, ambapo Jemadari wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, alitangaza elimu bure kwa watoto wote wa Zanzibar takriban miaka 55 iliyopita. Sherehe hizi tunazifanya siku ya sita tu baada ya sherehe nyengine muhimu tulizozifanya Ikulu Jumatatu ya tarehe 9 Septemba 2019.  Sherehe hizo tulizifanya kwa ajili ya kuwapongeza vijana wetu waliopata daraja la kwanza katika mitihani ya taifa iliyopita ya kidato cha nne na cha sita, ambapo jumla ya wanafunzi 375 walipata daraja hilo. Mara hii tumepata vijana wengi zaidi wa daraja la kwanza kwa vidato hivyo, kuliko mara zote zilizotangulia ikiwa ni ishara njema ya mafanikio yetu katika sekta ya elimu.Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kupata mafanikio hayo na kwa mara nyengine tena, natoa pongezi kwa vijana wetu wote hao.

Wananchi wa Zanzibar, miaka 18 iliyopita katika mwezi kama huu wa Septemba, walifungua ukurasa mpya wa maendeleo hasa ya elimu kwa kukizindua rasmi kwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) katika mwaka 2001. Ukurasa huu mpya wa maendeleo nchini ulitokana na kuanza kuwepo kwa fursa nyingi zaidi kwa wananchi wa Zanzibar kuweza kupata elimu ya Chuo Kikuu hapa hapa Zanzibar. Kwani itakumbukwa kuwa katika mwaka 1998, dhamira ya kuwa na vyuo vikuu hapa Zanzibar ilianza kutekelezwa kwa kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Zanzibar kilichopo Tunguu na Chuo Kikuu Kishirikishi cha Elimu cha Chukwani ambacho sasa kinaitwa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Al-Sumait.

Ndugu Wananchi,
Leo tumekusanyika hapa kufurahia mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu hiki cha SUZA na kushuhudia mafanikio hayo kwa njia ya maonesho na taarifa za Taasisi na skuli mbali mbali  zilizotolewa.  Nachukua fursa hii kutoa shukurani na pongezi zangu za dhati kwa viongozi wote wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar waliopo na waliopita, kwa mafanikio makubwa ambayo chuo hiki kimeyapata tangu kilipoanzishwa miaka 18 iliyopita. Kadhalika, natoa shukurani kwa jumuiya ya Chuo kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kunialika niwe Mgeni Rasmi wa sherehe hizi zilizofana sana. Nasema ahsante sana kwa kunipa heshima hii.

Nikiwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, napenda niungane na uongozi, wahadhiri, wafanyakazi na wana chuo wote wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, katika kuyasherehekea mafanikio ambayo chuo chetu kimeyapata, kwa kipindi chote tangu  kilipoanzishwa. Kadhalika, kwa niaba ya jumuiya ya Chuo Kikuu cha SUZA, nakukaribisheni wageni wetu nyote mliokuja kuungana nasi katika kuzifanikisha sherehe hizi. Kwa hakika, kufika kwenu kunatupa faraja, kwani ni ishara ya kuziunga mkono jitihada za Chuo chetu katika kuyatekeleza majukumu yake.  Lengo la chuo chetu ni kuwa Taasisi bora ya kutoa nguvu kazi ya wataalamu mahiri wenye maarifa, uzalendo na maadili watakaokuwa chachu ya kuongeza kasi ya maendeleo ya Zanzibar katika nyanja zote za maendeleo ya kiuchumi na huduma za jamii. Ni jambo la kutia moyo kuona kuwa lengo hilo linazidi kufanikiwa kila mwaka kwa kutoa wahitimu bora na wengi kwa fani mbali mbali.

Ndugu Wananchi,
Kuanzishwa kwa Chuo hiki ni matokeo ya kutafsiri kwa vitendo dhamira ya kupanua fursa ya elimu hapa nchini baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964. Waasisi wa Mapinduzi walipoamua kutoa elimu bure kwa watoto wote wa wakulima na wafanyakazi wa Zanzibar, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa Manifesto ya Chama cha Afro-Shirazi ya Uchaguzi Mkuu wa 1963.  Chama cha A.S.P kilikuwa na dira na malengo ya muda mrefu ya kuandaa rasilimali watu ya kuitumikia nchi hii na kusukuma mbele maendeleo yake.

Malengo hayo ya kizalendo yaliyotangazwa na Rais wa mwanzo wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, tarehe 23 Septemba, mwaka 1964,  yameweza kufanikiwa hatua kwa hatua, kutokana na dhamira ya dhati ya viongozi wetu waliotangulia na waliopo ambao kwa pamoja wameweza kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha maendeleo ya elimu nchini. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuongeza idadi ya skuli  za ngazi mbali mbali mijini na mashamba. Hali hio pamoja na kuimarisha upatikanaji wa walimu bora, vitabu vya kufundishia pamoja na vifaa mbali mbali na nyenzo za kujifunzia katika skuli zote za Zanzibar, ikawa ndio sababu ya kupata vijana wengi katika skuli zetu za Unguja na Pemba wenye sifa za kujiunga na elimu ya juu. Hali hio, ikachochea kuwepo kwa haja zaidi ya kuimarisha sekta ya elimu kwa kuzifungua fursa za kuanzisha vyuo vikuu hapa Zanzibar, kwani kabla ya 1998, Zanzibar haikuwa na Chuo Kikuu hata kimoja na vijana wetu wachache waliobahatika, walilazimika kuifuata fursa ya kusoma vyuo vikuu nje ya Zanzibar.

Ndugu Wananchi,  
Kwa kuzingatia haja ya kupanua fursa ya elimu ya juu hapa Zanzibar, ili kuongeza idadi ya wataalamu wetu na vile vile kuimarisha maendeleo ya sekta ya elimu na sekta nyengine, uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Tano wa Dk. Salmin Amour, ulifanya uamuzi wa kuanzishwa kwa Vyuo vikuu nchini kwa kuruhusu kuanzishwa kwa vyuo vikuu vya  viwili  vya binafsi mwaka 1998 kama nilivyovitaja hapo awali.

Kadhalika, kutokana na umuhimu wa Serikali nayo kuwa na Chuo Kikuu chake cha Umma, Serikali ilitunga sheria Namba 8 ya mwaka 1999 ambayo ndio sheria mama iliyopelekea kuanzishwa rasmi kwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar mwaka 2001. Kwa lengo la kutimiza matakwa ya kisheria na mamlaka aliyo nayo, Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu wa Sita, Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume alikizindua rasmi Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar mwaka 2001.
Katika hotuba yake ya uzinduzi wa Chuo hiki, Dk. Amani akiwa  Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar wa mwanzo alieleza miongoni mwa sababu za msingi za kuanzishwa kwa SUZA kwa kusema. Namnukuu. 

“The State University has been demanded by the circumstances confronting the development of Zanzibar. The aim shall be to produce professionals and well-read persons who will serve the needs of the country. Its curricular must therefore be dynamic demand driven, community oriented and adaptable to the changing economic, scientific and technical trends of the world”. Mwisho wa kumnukuu.

Dk. Amani akimaanisha kuwa haja ya kuanzishwa kwa Chuo kikuu cha SUZA, imetokana na mahitaji yetu ya maendeleo. Lengo la kuanzishwa kwake ni kufundisha wasomi na wataalamu tunaowahitaji kwa maendeleo ya nchi yetu. Kwa hivyo, mitaala yake lazima ilenge katika utoaji wa mafunzo ya mambo ya maendeleo tunayoyahitaji katika jamii yetu na yende sambamba na mabadiliko ya dunia katika uchumi, sayansi na ufundi. Naamini mtazamo huu wa Dk. Amani Abeid Karume, ndio dira ya utendaji wa chuo hiki na ndio sababu ya mafanikio tunayoyaona leo.

Ndugu Wananchi,  
Nafahamu kuwa mchakato wenyewe kwa kuanzisha Chuo hiki, ulikuwa mrefu na haikuwa kazi rahisi, lakini kutokana na dhamira ya dhati ya viongozi wetu waanzilishi, lengo la kuanzishwa kwa Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar liliwezekana na leo tunaadhimisha miaka 18 ya Chuo hiki tukiwa tumepata mafanikio makubwa sana ya kupigiwa mfano.

Nimefurahi kuwa miongoni mwa waanzilishi na viongozi wa chuo waliotangulia, wapo hapa pamoja nasi na tumewakabidhi vyeti maalum vya kuutambua na kuuthamini mchango wao kwa maendeleo ya SUZA ya sasa na baadae. Kwa wale ambao wameshatangulia mbele ya haki, tunamuomba Mwenyezi Mungu awape malazi mema peponi Amin.  Nampongeza sana Dk. Amani Abeid Karume, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUZA wa mwanzo aliyetoa mchango muhimu katika maendeleo ya chuo hiki.  Natoa pongezi kwa wenyeviti wa Baraza la Chuo na wajumbe wote waliokitumika chuo hiki kwa vipindi tofauti.  Natoa pongezi kwa Mawaziri wote wa Elimu waliokisimamia chuo hiki na kukiwezesha kupiga hatua za maendeleo tunayoyashuhudia. 

Kadhalika, natoa pongezi kwa Makamo Wakuu wa Chuo na Manaibu wao wote waliotangulia kwa kazi nzuri waliyoifanya.  Pongezi maalum nazitoa kwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo aliyepo hivi sasa Bwana Said Bakari Jecha na Wajumbe wote wa Baraza pamoja na aliyekuwa Makamo Mkuu wa Chuo Prof. Idris Rai ambae amefanya kazi kubwa ya kuhakikisha SUZA inapiga hatua kufuatana na maelekezo ya Serikali.  Yeye pamoja na viongozi  wote hao nawapa pongezi kwa kazi kubwa ya kizalendo ya kushirikiana na Jumuiya ya Chuo katika kuhakikisha kuwa chuo chetu kinatekeleza maagizo yanayotolewa na Serikali kwa mujibu wa sheria na matarajio ya wananchi wa Zanzibar.  Hongereni sana. Katika historia ya SUZA, Makamo Mkuu wa Chuo aliyemaliza muda wake Prof. Idris Rai atakumbukwa kwa  mchango wake alioutoa kwa maendeleo ya chuo hiki ambao utaendelea kuthaminiwa.

Ndugu Wananchi,
Ni dhahiri kwamba mafanikio tuliyoyapata katika kipindi kifupi cha miaka 18 ni ya kupigiwa mfano.  Vyuo vikuu mbali mbali ambavyo vinasifika dunia hivi sasa, ni vile ambavyo vimeanzishwa miaka au karne nyingi zilizopita vikiwemo Vyuo vya zamani sana katika historia ya Vyuo vikuu duniani. Historia inaonesha kwamba  baadhi ya vyuo vikuu  ambavyo vinasifika na kutajikana duniani hivi sasa, vimeanzishwa takriban miaka elfu moja iliyopita. Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Bologna kilichoko nchini Italy kilianzishwa mwaka 1088. Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza kilianzishwa baina ya mwaka 1096 na 1167. Kile Chuo Kikuu maarufu cha “Cambridge” kilianzishwa mwaka 1209. Wahispania nao walianzisha chuo chao Kikuu cha “Salamanca” mwaka 1134. Wafaransa walianzisha chuo kikuu cha Paris baina ya mwaka 1160  na 1250. Chuo  Kikuu cha “Al Azhar” nchini Misri nacho ni miongoni mwa Taasisi Kongwe za elimu duniani, ambacho  kilianzishwa mwaka  970 AD, ingawa haikupewa jina la  chuo Kikuu wakati  wa kuanzishwa kwake.  Vyuo hivi nilivyovitaja ni miongoni mwa vyuo vikuu  10  vikongwe duniani na vinaendelea kutoa taaluma katika fani mbali mbali hadi leo. 

Historia hii  inaonesha kwamba Chuo  chetu cha SUZA bado ni kichanga. Licha ya uchanga wake, bado chuo chetu ni kidogo kwa idadi ya wanafunzi pale tunapojilinganisha na vyuo vikuu vya nchi mbali mbali. Kwa mfano Chuo Kikuu  Huria cha  Taifa cha Indira Gandi (Indira Gandhi National Open University) kina wanafunzi waliosajiliwa na wanaoendelea na masomo wapatao  4,000,000   hivi sasa.  Hiki ni Chuo Kikuu kikubwa duniani kwa idadi ya wanafunzi kikifuatiwa na Chuo kikuu cha Taifa cha Bangladesh ambacho kina idadi ya wanafunzi wapatao 2,097,182 waliosajiliwa na wanaoendelea na masomo.

Kwa hivyo, mafanikio tuliyoyapata kwa kipindi cha miaka 18 na tukizingatia ukubwa wa chuo chetu, bila ya shaka  ni makubwa  na yanakwenda sambamba  na malengo yaliyowekwa na Serikali wakati tulipokianzisha. Maendeleo tunayoendelea kuyaona yanaonesha wazi kwamba tutaendelea kupiga hatua kwa haraka na Chuo hiki kitaendelea  kuongeza idadi ya wanafunzi  kwa kadri kinavyoendelea kupevuka.

Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba, ilipoingia madarakani baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, iliendeleza jitihada za kuimarisha elimu ya juu pamoja na kukiimarisha Chuo Kikuu cha Taifa SUZA kwa kuzingatia mipango mikuu ya maendeleo ya Zanzibar ikiwemo Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2010 – 2015, ambayo katika ibara ya 150(f) (i) ilieleza, nanukuu:
“Kukamilisha ujenzi wa majengo mapya ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) huko Tunguu”
Mwisho wa kunukuu.

Katika kukiimarisha Chuo kikuu cha SUZA, kwa kuongeza idadi ya majengo, samani na vifaa vyengine vya kufanyiakazi, Serikali ilianzisha masomo na fani mpya mbali mbali kwa madhumuni ya kwenda sambamba na mahitaji ya wataalamu tulio nao kwa sekta mbali mbali za maendeleo hapa Zanzibar. Baadhi ya programu hizo ziliandaliwa upya ndani ya mfumo uliokuwa ukiendelea wa chuo. Hata hivyo, programu nyengine kadhaa ziliendelezwa kutokana na hatua muhimu ambayo Serikali ilichukua ya kuziunganisha baadhi ya Taasisi zilizokuwa zikitoa elimu ya juu katika fani mbali mbali. Miongoni mwa Taasisi hizo ni Chuo cha Afya na Sayansi za Tiba, Chuo cha Uongozi wa Fedha na Chuo cha Maendeleo ya Utalii kwa awamu ya kwanza; na hivi karibuni tu katika awamu ya pili tumekiunganisha na SUZA, Chuo cha Kilimo cha Kizimbani.
Kazi ya kuunganishwa vyuo hivi na SUZA haikuwa rahisi kwani ilipitia katika taratibu kadhaa zilizo ndefu. Kwa mfano, kabla ya kuunganishwa na SUZA, kila kimoja miongoni mwa vyuo hivyo, ikiwemo SUZA yenyewe, kilikuwa na Sheria yake iliyokianzisha pamoja na kanuni zilizoambatana na sheria hizo.Kwa mantiki hii, ililazimu sheria hizo zibadilishwe, ili ipatikane sheria moja mpya ya SUZA. Katika hatua hii, ni dhahiri kwamba kulikuwa na changamoto, lakini mafanikio na faida zake ni nyingi zaidi. Wanasema watu ‘ukitaka vizuri, ukubali kudhurika’. Hii ni tafsiri ya usemi wa Kiingereza kwamba: ‘No pain, no gain’. Na sisi tumezikabili changamoto hizo, na leo tumefikia hatua nzuri ya mafanikio ambayo tunayaeleza hapa.Tujipongeze sana kwa kufanya uamuzi huu wa busara.

Kati ya faida hizo ni kwamba, baada ya Chuo cha Afya na Sayansi za Tiba kuwa miongoni mwa Skuli za SUZA, Serikali iliamua kuanzisha masomo ya Shahada ya Udaktari, ili kuweza kuimarisha upatikanaji mzuri wa wataalamu wa sekta ya afya na kuendeleza utoaji wa huduma za kiwango bora katika Hospitali na vituo vyetu vya afya.

Ndugu Wananchi,
Mtakumbuka kuwa katika mahafali iliyopita, wahitimu wa mwanzo 25 walimaliza masomo yao ya udaktari mwaka 2018, na hivi sasa vijana hao wameshaajiriwa na Wizara ya Afya na wapo katika Hospitali ya Mnazimmoja. Kupatikana kwa madaktari hawa pamoja na vijana wetu wengine waliomaliza masomo yao ya udaktari nje ya Zanzibar na kuajiriwa, kumetuwezesha kuwa na ongezeko la madaktari wetu. Ongezeko hilo limeleta uwiano mzuri zaidi wa madaktari kwa wagonjwa wanaowahudumia. Hadi kufikia mwezi wa Disemba 2018, uwiano wa daktari mmoja ni kuwahudumia watu 6,435 (1:6435) ikilinganishwa na mwaka 2017 ambapo ilikuwa daktari mmoja anahudumia watu 8,392 (1:8392). Tuna matumaini makubwa kuwa hali hii itazidi kuimarika kwa kadiri vijana wetu wanavyomaliza mafunzo yao.

Kadhalika, kwa kuzingatia mahitaji ya wataalamu wa afya katika huduma za meno na kuimarisha taaluma za wauguzi na ukunga,  tumeamua  kuanzisha  mafunzo ya fani hizo. Ni jambo la faraja kwamba kuanzia mwaka huu wa masomo, mafunzo ya Shahada ya udaktari wa meno na shahada ya uuguzi na ukunga yataanza kutolewa. Hii ni hatua nyengine muhimu ya maendeleo nchini katika kuimarisha huduma za afya. Kupatikana kwa wataalamu wa fani hii kutatusaidia sana katika kukabiliana na matatizo ya meno yanayowasumbua wananchi. Vile vile, wataalamu wa fani ya uuguzi na ukunga watakuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa malengo ya serikali ya kukabiliana na vifo vya mama wajawazito na watoto wakati wa kujifungua.

Ndugu Wananchi,
Dhamira ya Serikali ya kuziunganisha na SUZA Taasisi zetu za elimu ya juu, imesaidia sana kukua kwa Chuo hicho, sambamba na kuzijengea uwezo zaidi Taasisi na Vyuo vilivyounganishwa pamoja na kuinua daraja, ubora na hadhi ya elimu inayotolewa vikiwa katika mamlaka ya SUZA.  Hivi sasa, vyeti vinavyotolewa katika fani zilizokuwa zikisomeshwa na Taasisi zetu hizo vina thamani kubwa zaidi kwa kuwa vinatolewa na Chuo Kikuu.  Hatua hio, inawapa wahitimu wetu fursa kubwa ya kukubalika katika soko la ajira na utaalamu wao kutambuliwa katika medani ya kitaifa na kimataifa.

Vile vile, uamuzi wetu huo, umetuwezesha kuzipatia Taasisi na Vyuo hivyo, bajeti kubwa zaidi kwa kuzingatia mahitaji halisi ya Programu zinazosomeshwa.  Kadhalika, hatua hio imerahisisha utekelezaji wa mipango yetu ya kuwajengea uwezo wahadhiri pamoja na ujenzi wa miundo mbinu ya kisasa inayohitajika. Juhudi zetu za kupanua Chuo zinakwenda sambamba na kuimarisha uhusiano baina ya Chuo chetu na Taasisi pamoja na Vyuo vikuu mbali mbali ulimwenguni. Idadi ya Hati za Maelewano (MoU) zimeongezeka kutoka 3 mwaka 2011 hadi 70 hivi sasa. Kadhalika, idadi ya programu imeongezeka kutoka 6 wakati kilipozinduliwa chuo hadi sasa ambapo zipo programu 62.  Kadhalika, bajeti ya chuo imeongezeka kutoka TZS bilioni 4.5 hadi TZS bilioni 23 na chuo kinaweza kujiendesha chenyewe kwa kiasi kikubwa. Haya ni mafanikio makubwa ya kupigiwa mfano ambayo kila mmoja wetu anapaswa kutembea kifua mbele na kujivunia.


Ndugu Wananchi,
Kwa malengo ya kupata wataalamu wa kada mahsusi,Chuo hulazimika kuanzisha programu maalum, pamoja na kuanzisha skuli mpya za masomo na shahada mbali mbali. Kutokana na haja ya Zanzibar ya kutoa wataalamu wa ngazi ya juu wa lugha ya Kiswahili, Serikali iliamua kuanzisha mafunzo ya Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Kiswahili. Matunda ya uamuzi huu yameanza kujitokeza ambapo wahitimu11  wameshamaliza shahada hio ya juu ya lugha ya Kiswahili.

Ni dhahiri kwamba kuwa na wahitimu wenye elimu ya juu ya lugha ya Kiswahili kunachangia kutupa heshima kuwa, Zanzibar yenye asili ya Kiswahili ndio wataalamu wa lugha hio. Vile vile, kunatupa nafasi ya kunufaika na fursa za kufundisha Kiswahili kwa wageni wanaokuja nchini na walioko nchi za nje wenye mahitaji ya kujifunza lugha hii adhimu. Nakutieni shime kuichangamkia fursa ya kufundisha Kiswahili katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kuwa tayari Jumuiya hio imeshaidhinisha matumizi ya lugha ya Kiswahili katika Jumuiya hio.

Ndugu Wananchi,
Wakati nikitembelea mabanda ya maonesho ya Skuli na vitengo mbali mbali vilivyo katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar, niliweza kujionea na kuelezwa mambo mbali mbali ya mafanikio yaliyofikiwa na Taasisi yetu hii tangu ilipozinduliwa rasmi miaka 18 iliyopita.

Nimevutiwa sana na kazi mbali mbali nilizoziona katika mabanda ya Skuli zote za Chuo na Taasisi zake. Kwa mfano nimevutiwa sana na banda la Skuli ya Elimu kwa kuona matunda ya kuanzishwa kwa Skuli ya Sekondari ya SUZA. Katika maonesho haya, nimefurahishwa na kazi waliyoiandaa kwa ajili ya elimu mjumuisho kwa kuonesha mashine ya nukta nundu na namnazinavyoweza kuwasaidia watoto wenye ulemavu wa macho. Hongereni sana kwa kazi hio nzuri na vile vile, nakupongezeni kwa kuendelea kutoa wanafunzi wa daraja la kwanza katika mitihani ya kidato cha sita ambao ni kati ya wanafunzi bora waliofika Ikulu kupongezwa.

Kadhalika, nimefurahishwa na niliyoyaona katika Skuli ya Afya, Skuli ya Kiswahili pamoja na Skuli ya Biashara na kupata taarifa za utafiti za kituo cha TROCEN na Kurugenzi ya Elimu ya Juu na Tafiti kwa kushirikiana na Skuli ya Sayansi ya Asili na Sayansi Jamii. Nimevutiwa sana na jinsi Chuo kinavyoendeleza shughuli za utafiti. Hata hivyo, nawaagiza wakufunzi wote wa chuo katika fani tafauti muongeze kasi katika kufanya tafiti mbali mbali, kwani utafiti ndio dhima moja kubwa ya Vyuo Vikuu. Tafiti ndio kiini na chimbuko la maendeleo ya kitaaluma na njia ya kupata ufumbuzi wa matatizo mbali mbali ya kisayansi na kijamii.

Kadhalika, nimevutiwa sana na maonesho ya miradi mbalimbali ambayo Chuo chetu kinashiriki na matokeo yake. Kwa hakika, maendeleo yaliyopatikana ni makubwa sana kwa kipindi hiki kifupi cha miaka 18, ikilinganishwa na vyuo vingi vilivyoanzishwa hapa Tanzania na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ndugu Wananchi,
Ni wazi kuwa pamoja na mipango mizuri iliyopo, mafanikio ya Chuo hiki yametokana na kuwa na viongozi wazuri wa kuyasimamia maendeleo ya Taasisi hii muhimu ya kutoa elimu ya juu, mazingira mazuri ya kutolea taaluma ya fani mbali mbali pamoja na wahadhiri na wafanyakazi wanaojituma na kutambua wajibu wao. Zaidi ya yote ni umoja na ushirikiano wa wanajumuiya yote ya Chuo, hali ambayo huchangia sana taasisi hii kutoa wahitimu bora kitaaluma, kinidhamu, kimaadili na kiuzalendo. Hongereni sana.

Kazi kubwa iliyo mbele yetu sasa, ni kuhakikisha kwamba tunayaendeleza mafanikio haya kwa vitendo,  tunayatangaza kwa wananchi na wageni ikiwa ni hatua muhimu ya kuthamini jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo kwa faida na maslahi ya wananchi wote.

Nimefarajika kuona kwamba Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kimepata Cheti cha Ithibati (Accreditation) kilichotolewa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), ambapo mafunzo yanayotolewa na Chuo hiki pamoja na vyeti na Shahada zake zinazidi kutambulikana duniani kote.  Kadhalika, SUZA imepata Cheti cha Utambuzi wa kutoa masomo ya Afya na kuitumia Hospitali kuu ya Mnazimmoja kuwa ni hospitali ya kufundishia.  Utambuzi huo umefanywa na Bodi ya Afya ya Afrika Mashariki.  Hii ni hatua nyengine kubwa katika historia ya SUZA na nchi yetu kwa jumla.  Vile vile, natoa pongezi kwa Wawakilishi wa Taasisi nyengine wote waliokuja kushirikiana nasi katika hafla hii ya kujipongeza.  Nasema ahsanteni sana.

Ndugu Wananchi,
Leo kama ilivyoelezwa, tutashuhudia uzinduzi rasmi wa skuli mpya ya Utibabu wa Meno, Skuli ya Kilimo na Taasisi ya Masomo ya Ubaharia za Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar. Ni dhahiri kuwa hatua ya kuongeza Taasisi hizo, itazidi kuipaisha SUZA na kuiongezea sifa ya kuwa miongoni mwa Vyuo Vikuu vichache vyenye kufundisha fani nyingi kwa pamoja ikiwemo Ualimu, Kilimo, Udaktari, Lugha, Uongozi wa Fedha na Utawala, utalii pamoja na Ubaharia.  Hii ni sifa ya kipekee ya Chuo kikuu cha SUZA.

Mafanikio tuliyoyapata katika kipindi hiki kifupi tangu tulipoanzisha chuo hiki ni makubwa na tuna haki ya kuyasherehekea mafanikio tuliyopata  na kujipongeza. Wakati tunaanzisha Chuo hiki mwaka 2001, tulikuwa na Kampasi moja, leo tunazo kampasi 8, tulianza na skuli moja leo zipo  8. Tulikuwa na taasisi moja leo zipo mbili pamoja na vituo viwili maalum kwa ajili ya utafiti ambavyo mwanzoni havikuwepo.

Kwa upande wa programu, tulianza na programu 2 tu zilizokuwa na idadi ya wanafunzi 71, ambapo hivi chuo kinaendesha programu 62 zenye idadi ya wanafunzi 4042.

Mipango yetu ya baadae ni kuongeza skuli mpya kwa kuzingatia mahitaji yetu halisi  ya maendeleo. Tumedhamiria kuanzisha Skuli ya Kompyuta, Mawasiliano na Habari, Skuli ya Uhandisi wa Mafuta na Gesi pamoja na Taasisi ya Uvuvi na Masomo ya Bahari. Programu hizi zinakwenda sambamba na mipango yetu ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na  kuendeleza sekta ya mafuta na gesi na kuimarisha uchumi wa bahari (blue economy).

Hali hii inatoa uwanja mpana kwa vijana wetu watakaotaka kusoma katika Chuo hiki kuweza kuchagua fani ya masomo wanayoitaka. Kadhalika, hatua hii ni muhimu katika kuhakikisha kwamba tunawaandaa na kuwafundisha wenyewe wataalamu wetu wa fani mbali mbali kwa kuzingatia mahitaji na mipango yetu ya maendeleo. Nakipongeza sana Chuo cha SUZA kwa kulizingatia jambo hili katika utekelezaji wa majukumu yake. Hongereni sana. Nna matarajio makubwa kwamba mtazidi kubuni masomo ya fani nyengine mpya kulingana na mahitaji ya maendeleo ya nchi yetu.

Ndugu Wananchi,
Chuo chetu hivi sasa kina sifa ya pekee ya kuwa na Makamu Mkuu wa Chuo mwanamke, Dk.Zakia Mohamed Abubakar. Pamoja na historia kwa chuo hiki, huenda akawa mwanamke pekee mwenye wadhifa huu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunampongeza kwa kupata fursa hio. Ni dhahiri kwamba elimu, uzoefu na ushirikiano alio nao kwa wenzake, utamuwezesha kuyatekeleza vyema maagizo ya Serikali na kukiletea maendeleo Chuo hiki. Natoa shukurani kwa washirika wetu wa maendeleo wanaoshirikiana na chuo katika kuyafikia malengo yake.

Ndugu Wananchi,
Namalizia hotuba yangu kwa kuuagiza Uongozi wa Chuo hiki uendelee kuwajengea uwezo wahadhiri na watumishi wake wa kada mbali mbali, ili kukidhi mahitaji ya chuo. Tumuombe Mwenyezi Mungu atupe uwezo zaidi wa kuitekeleza mipango yetu ya kukiimarisha chuo chetu, ili iwe Taasisi bora yenye kutoa wahitimu weledi wanaokubalika katika ngazi ya Taifa na Kimataifa.

Kwa mara nyengine, natoa shukurani kwa uongozi wa Chuo kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kuandaa sherehe hizi zilizofana sana na  kunialika kuwa Mgeni Rasmi. Namuomba Mwenyezi Mungu atuzidishie amani, umoja na mshikamano, ili tupate kupiga hatua za maendeleo na kuimarisha ustawi wa jamii.  Nakutakieni nyote kila la kheri na Mwenyezi Mungu aturudishe sote nyumbani kwa salama.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.