Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati wa hafla ya kusherehekea mafanikio ya SUZA toka kuazishwa kwake Zanzibar mwaka 1999 -2019, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein, Tunguu Zanzibar Wilaya ya Kati Unguja.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amesema kuwa kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar
(SUZA) ni matokeo ya kutafsiri kwa vitendo dhamira ya kupanua fursa ya elimu
hapa Zanzibar baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Rais Dk. Shein
aliyasema hayo leo katika hafla ya kusherehekea mafanikio ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA)
iliyofanyika kwenye ukumbi wa Dk. Ali Mohamwd Shein uliopo katika Kampasi ya
Chuo Kikuu hicho, Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Katika maelezo yake
Rais Dk. Shein alisema kuwa Chama cha Afro Shirazi Party (ASP), kilikuwa na
dira na malengo ya muda mrefu ya kuandaa rasilimali watu ya kuitumikia nchi hii
na kusukuma mbele maendeleo yake.
Aliongeza kuwa malengo
hayo ya kizalendo yaliyotangazwa na Rais wa mwanzo wa Zanzibar Marehemu Mzee
Abeid Amani Karume, tarehe 23, kwala 1964 yameweza kufanikiwa hatua kwa hatua
kutokana na dhamira ya dhati ya viongozi waliopo ambao kwa pamoja wamechukua
hatua madhubuti za kuimarisha maendekeo ya elimu nchini.
Alieleza kuwa hali
hiyo imechochea kuwepo kwa hatua za kuimarisha sekta ya elimu kwa kuzifungua
fursa za kuanzisha vyuo vikuu hapa Zanzibar kwani kabla ya mwaka 1998, Zanzibar
haikuwa na Chuo Kikuu hata kimoja na vijana wachache waliobahatika walilazimika
kuifuata fursa ya kusoma vyuo vikuu nje ya Zanzbar.
Alisema kuwa uongozi
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Tano wa Dk. Salmin Amour Juma
ulifanya uamuzi wa kuanzishwa kwa Vyuo Vikuu nchini kwa kuruhusu kuanzishwa kwa
vyuo vikuu viwili vya binafsi mwaka 1998.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa kwa lengo la kutimiza matakwa ya Kisheria na mamlaka aliyonayo, Rais
Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Sita, Dk. Amani Abeid Karume alizindua rasmi
Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar mwaka 2001 na kumpongeza kwa mchango wake mkubwa
alioutoa kiongozi huyo akiwa Mkuu wa mwanzo wa Chuo hicho.
Rais Dk. Shein ambaye
pia, ni Mkuu wa Chuo hicho alieleza kuwa ni dhahiri kwamba mafanikio
yaliopatikana katika kipindi cha miaka 18 ni ya kupigiwa mfano na ni makubwa
ambayo yakwenda sambamba na malengo yaliyowekwa na Serikali wakati kilipoanzishwa
chuo hicho.
Aidha, Rais Dk. Shein
alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba, ilipoingia
madarakani baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 iliendeleza jitihada za kuimarisha
elimu ya juu pamoja na kukiimarisha chuo hicho kwa kuzingatia mipango ya
maendeleo ya Zanzibar ikiwemo Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2010-2015.
Rais Dk. Shein alitoa
pongezi kwa Baraza la Mapinduzi kwa kutoa mwongozo wa Kisera wa kukiimarisha
chuo hicho kwa kukiunganisha na Taasisi zilizokuwa zikitoa elimu ya juu katika
fani mbali mbali hapa Zanzibar.
Miongoni mwa Taasisi
hizo ni Chuo cha Afya na Sayansi za Tiba, Chuo cha Uongozi wa Fedha na Chuo cha
Mandeleo ya Utalii kwa awamu ya kwanza na hivi karibuni tu katika awamu ya pili
kimeunganishwa na SUZA, Chuo cha Kilimo cha Kizimbani.
Alieleza kuwa kati ya
faida za muunganisho huo ni kwamba baada ya Chuo cha Afya na Sayansi za Tiba
kuwa miongoni mwa Skuli za SUZA, Serikali iliamua kuanzisha masomo ya Shahada
ya Udaktari, ili kuweza kumarisha upatikanaji mzuri wa wataalamu wa sekta ya
afya.
“Mtakumbuka kuwa
katika mahafali iliyopita, wahitimu wa mwanzo 25 walimaliza masomo yao ya
Udaktari mwaka 2018, na hivi sasa vijana hao wameshaajiriwa na Wizara ya Adfya
na wapo katika Hospitali ya Mnazimmoja”,alisema Dk. Shein.
Aidha, alieleza kuwa
ni jambo la faraja kwamba kuanzia mwaka huu wa masomo, mafunzo ya Shahada ya
Udaktari wa meno na Shahada ya Uuguzi na Ukunga yataanza kutoewa.
Alieleza kuwa kutokana
na haja ya Zanzibar ya kutoa wataalamu wa ngazi ya juu wa lugha ya Kiswahli,
Serikali iliamua kuanzisha mafunzo ya Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Kiswahili
ambapo tayari wahitimu 11 wameshamaliza Shahada hiyo ya juu ya lugha ya
Kiswahili.
Dk. Shein alieleza
kuwa kazi kubwa iliyo mbele hivi sasa ni kuhakikisha mafanikio yaliopatikana
yanaendelezwa kwa vitendo, yanatangazwa kwa wananchi na wageni ikiwa ni hatua
muhimu ya kutathmini jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alieleza kufarajika
kwake kwa kuona kwamba Chuo hicho kimepata Cheti cha Ithibati (Accreditation)
kilichotolewa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), pamoja na Cheti cha
Utambuzi wa kutoa masomo ya Afya na kuitumia Hospitali ya Mnazimmoja kuwa ni
hospitali ya kufundishia kutoka Bodi ya Afrika Mashariki.
Pia, alipongeza
jitihada za kuzinduliwa rasmi kwa skuli mpya ya Utibabu wa Meno, Skuli ya
Kilimo na Taasisi ya Masomo ya Ubaharia za Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar
ambayo hio ni sifa ya pekee kwa Chuo hicho.
Rais Dk. Shein
aliwapongeza Makamo Wakuu wa Chuo na Manaibu wao wote waliotangulia kwa kazi
nzuri waliyoifanya na kutoa pongezi maalum kwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo
aliyepo hivi sasa Said Bakari Jecha na Wajumbe wote wa Baraza pamoja na
aliyekuwa Mmakamo Mkuu wa Chuo Profesa Idris Rai ambaye amefanya kazi kubwa ya
kuhakikisha SUZA inapiga hatua kufuatana na maelekezo ya Serikali.
Alieleza kuwa wakati
SUZA ikianzishwa kulikuwa na Kampasi moja leo zipo Kamapasi 8, ilianza na Skuli
moja na leo zipo skuli 8, kulikuwa na taasisi moja leo zipo mbili pamoja na
vituo viwili maalum kwa ajili ya utafiti ambavyo mwanzoni havikuwepo.
Pia, kwa upande wa programu, zilianza mbili zilizokuwa na
idadi ya wanafunzi 71 ambapo hivi sasa Chuo kinaendesha programu 62 zenye idadi
ya wanafunzi 4042.
Alieleza mipango ya
kuansihwa kwa Skuli ya Kompyuta, mawasiliano na Habari, Skuli ya Uhandisi wa
Mafuta na Gesi pamoja na Taasisi ya Uvuvi na Masomo ya Bahari ambazo zote
zinakwenda sambamba na mipango ya maendeleo.
Dk. Shein aliuagiza
uongozi wa Chuo hicho kuendelea kuwajengea uwezo wahadhiri na watumishi wake wa
kada mbali mbali iki kukidhi mahitaji ya chuo hicho ili kiweze kutoa wahitimu
weledi wanaokubalika katika ngazi ya Taifa na Kimataifa.
Nae Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma alimpongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi zake
za kuhakikisha kinapata mafanikio makubwa ambayo tayari hivi leo yameshaanza
kupatikana na yanaonekana wazi.
Mapema Makamu Mkuu wa
Chuo hicho Dk. Zakia Mohamed Abubakar alitumia fursa hiyo kueleza historia ya
Chuo hicho na kueleza kuwa Kamati ya watu saba iliundwa na aliyekwua Rais wa
Zaanzibar Dk. Salmin Amor Juma mwaka 1996 kufanyia kazi suala la kuanzishwa kwa
SUZA ikiongozwa na Profesa Saleh Idrissa.
Alieleza kuwa Chuo
hicho ni cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kilichoanzishwa kwa Sheria Namba
8 ya mwaka 1999 na kuzinduliwa mwaka 2001 hatua iliyopelekea kuzinduliwa rasmi na Dk. Amani Abeid Karume
akiwa ni Mkuu wa Chuo wa Mwanzo.
Dk. Zakia alisema kuwa
Chuo kilianza masomo kwa kuanza na Idara ya Sanaa mwaka 2001/2002 mwaka wa
mwanzo wa masomo ikiwa na wanafunzi 71 Shahada 50 na Stashahada 21.
Nae Katibu Mtendaji wa
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Professa Charles Kihampa alitoa pongezi kwa
Serikali kwa kuanzisha Shahada ya Udaktari wa Meno ambacho SUZA kitakuwa cha
pili kwa Tanzania pamoja na kuanziasha programu ya Kilimo ambayo kwa Tanzania
inatolewa na Chuo cha Sokoine kiliopo Morogoro pekee.
Pia, alitumia fursa
hiyo kueleza kuwa TCU itaendelea kuiunga Mkono SUZA katika kuhakikisha inapata
mafanikio zaidi kwani tayari hivi sasa SUZA inatambulika Kitaifa na Kimataifa.
Mapema Rais Dk. Shein
alitembelea mabanda ya maonesho yaliomo
ndani ya ukumbi huo ambayo yaliendeshwa na SUZA na kupata maelezo kutoka kwa wanafunzi
wa chuo hicho juu ya shughuli na elimu inayotolewa na Skuli pamoja na Taasisi
zote zilizomo katika Chuo Kikuu hicho.
Pia, Rais Dk. Shein
akiwa Mkuu wa Chuo hicho cha SUZA, alitoa vyeti vya utambuzi kwa viongozi
waliokitumikia Chuo hicho tokea kuanzishwa kwake pamoja na yeye kukabidhiwa
vyeti vya Utambuzi na Ithibati wa Chuo Kikuu hicho cha Taifa cha Zanzibar
(SUZA).
Viongozi mbali mbali
wa vyama vya siasa na Serikali pamoja na wakuu wa vyuo mbali vya ndani na nje
ya Zanzibar walihudhuria pamoja na Mabalozi, Wawakilishi wa Mashirika ya Umoja
wa Mataifa, Wakufunzi, wanafunzi, wazee na wageni mbali mbali.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment