Habari za Punde

Jukwaa la Pamoja Sekta ya Sheria Zanzibar.


Katibu Mkuu Wizara ya Sheria na Katiba Zanzibar Mhe. Georde Joseph Kazi, akihutubia wakati wa mkutano wa Wadau wa Sekta ya Sheria Zanzibar, wakijadili utafiti wa uwezekano kuazishwa kwa Jukwaa la Wanasheria Zanzibar, uliofanyika katika ukumbi waHoteli ya Zanzibar Beach Resort mazizini Zanzibar.

Na. Raya Hamad - WKS
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Ndg George Joseph  Kazi amesema kuundwa kwa jukwaa la wadau wa sekta ya sheria kutasaidia kuwaunganisha  wadau wa sekta hiyo na kuleta maendeleo endelevu katika  kada  hio muhimu  kwa maslahi yaTaifa.

Ameyasema hayo kwenye mkutano uliowakutanisha viongozi na watendaji kutoka  sekta ya sheria uliojadili taarifa ya utafiti juu ya uwezekano wa kuanzisha jukwaa la pamoja kwa wahusika washeria Zanzibar

Mhe.George Kazi amewataka wajumbe hao kutoa michango na mawazo yao na kufanya upembuzi ili kuona mahitaji  muhimu yatakayosaidia  kufahamu sekta ya sheria,  kwa kutambuwa kuwa sekta ya sheria ndio kiini katika masuala yote ya maendeleo ya nchi .

Mbali ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu , Ofisi ya Mkurugenzi  wa Mashtaka, Tume ya kurekebisha Sheria na Mahakama lakini  kumekuwa na ongezeko kubwa la wanasheria  hata hivyo kinachokosekana ni kutokuwa na jukwaa la pamoja linalowaunganisha wanasheria hao.

Jukwaa ambalo litasimamia na kuangalia maendeleo ya sekta ya sheria hali ilivyo na jinsi gani itakuwa na uratibu  ambao utasaidia  kujuwa mambo mengi ya kuangalia wapi tulipotoka ,tulipo na tunakoelekea,  matatizo gani yanayoikumba  sekta sheria iwe ya Jinai na  Madai kwa ajili ya maendeleo chanya ya sekta ya hiyo.

Katibu George  amesema sekta ya sheria inaendelea kukuwa kwa kasi hivyo wizara imeona ipo haja ya kuwa na chombo ambacho kitasaidia kuzidisha kasi ya uwajibikaji ili kila mmoja atimize wajibu wake “muhimu kujielewa kama wanasheria kufahamu jukumu walilonalo na kazi wanazozifanya ikiwemo kufanya tathmini ya kile wanachokifanya badala ya kufanya kazi kwa mazoea, hii itasaidia  kuleta chachu katika sekta ya sheria kujenga  utamaduni wa kujisomea na kufahamu mambo mapya yanayotokea hivyo jukwaa hili litatusaidia tuweze kujitambua”alisema George

Ameendelea kusema kuwa kupitia Jukwaa upo uwezekano wa kufanya utafiti na kufahamu kiwango cha ongezeko la wanasheria, kuwafahamu mawakili  na mahakimu na kuona sekta ya sheria imekuwa kwa kiwango gani na je  ni kweli wamebobea kuwa wataalamu wanaofikia kiwango na  vigezo vinavyohitajika katika kada ya sheria Kuwepo kwa Jukwaa moja litawezesha pia  kutoa mapendekezo na kuwasilisha taarifa zao  ambazo zitapelekea Wizara kuweza kuzifanyia kazi kwa pamoja .

Nao wawasilishaji  kutoka  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ndg  Mohammed  Khamis na ndugu Mussa Kombo  wamesema  lengo la kuwa na chombo hiki nikusaidiana mawazo na ushauri ilikuona uwajibikaji unaimarika na sio kuingilia majukumu yaVyombo vya kisheria pia kuondosha migongano ya kisheria baina ya taasisi na kutekelezwa kwa vitendo mawazo na ushauri  utakaotolewa .

Nae Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar ndugu Ibrahim Mzee Ibrahim ameanisha  mambo manne ambayo yakitekelezwa ipasavyo yatakuwa nichachu yamaendeleo ikiwemo vyombo vya mashtaka kufahamu majukumu yao yakiutendaji, pia kufuatwa kwa Maadili na taratibu zake,  usimamizi pamoja na suala la uwajibikaji na ushirikiano baina ya vyombo vya Sheria vilivyopo nchini.

Aidha amesema kinachounganisha taasisi hizi zote za sheria ni muongozo wa taasisi na kila chombo kinamamlaka yake na imewekewa sheria  hivyo kuwepo kwa jukwaa hili kutasaidia kuondosha baadhi misuguano na kuwa na sauti ya pamoja katika utekelezaji wa masuala ya utowaji  haki na sheria na mwisho wa yote ni taasisi yenyewe  iliyopewa mamlaka kuona vipi inabadilika kwa kufuata taratibu

Mkurugenzi Mipango  Sera  na Utafiti Bi Daima Mohamed Mkalimoto  amewataka wawasilishaji ya mada kuyapitia majukumu ya Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na bajeti ya Wizara ili kujenga hoja kwa msingi imara  itayosaidia  kuundwa kwa kwa jukwaa la pamoja .

Bi Daima ametoa mapendekezo  kwa  kuona tunaanajifunza pia mazuri yanayotekelezeka kutoka kwa wengine na kusema kuwa uhai wa sekta ya sheria utaonekana kwa kuangalia zaidi na kuona umuhimu wa  kuweka jukumu la kulinda rasilimali za nchi  kuangalia mikataba kiundani kutoa mapendekezo  pia kuweka uwiyano  katika jamii hata katika ngazi za Mikoa na  Wilaya ili na wao waweze kuangalia masuala ya kisheria katika maeneo yao.

Kamishna  wa Kazi Bi Fatma Iddi  Ali amesema kuundwa kwa Jukwaa la pamoja kwa sekta ya sheria hakutakuwa na muingiliano bali ni kuondoa ukakasi lakini utazingatia umuhimu wa taasisi zinazoguswa kwani kila taasisi inayosimamia sheria ina taratibu zake namiongozo yake ya kiutendaji

Aidha amesisitiza  juu ya namna yakumuandaa na kumuuangalia mwanasheria na kazi anazozifanya ili aweze kuwa na maadili mazuri anakoelekea kwa vile mwanasheria ndie anaetegemewa kuwa Jaji, Mrajisi wa mahakama , Hakimu, Wakili ama   kwa namna yeyote kuwa msimamizi katika masuala ya sheria na  utowaji wa  haki, Bi Hamisa Mmanga Makame Mkurugenzi mipango uendeshaji na rasilimaliwatu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ameipongeza serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kutokana na jitihada zilizopo ukilinganisha na miaka yanyuma hivi sasa kila siku kunapiga hatua na maendeleo yanaonekana kupitia sekta ya sheria.

Wakili wa Mahakama kuu Zanzibar Bw  Zaharani Mohamed Yussuf  ametoa msisitizo kushirikishwa kikamilifu kwa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana ambao nao wanasimamia  utatuzi wa migogoro, mali hivyo kuwepo kwachombo hiki kutarahisisha utowaji wa haki kwaupande wao na kwa wanajamii .

Mkutano  huo uliowakutanisha viongozi na watendaji kutoka  sekta ya sheria uliojadili taarifa ya utafiti juu ya uwezekano wa kuanzisha jukwaa la pamoja kwa wahusika wa  sekta ya sheria Zanzibar umeandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Shirika la Mendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP  umefanyika kwenye ukumbi wa mkutano uliopo  Zanzibar Beach Resort  Mazizini.

Muwezeshaji kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar Ndg Mohammed Khamis akitoa mada kuhusu taarifa ya utafiti juu ya uwezekano wa kuanzisha jukwaa la pamoja kwa wahusika sekta ya sheria Zanzibar  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.