Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Azungumza na Ujumbe wa Kampuni ya Millicom Group leo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Bwana Julian wa Kampuni Millicom  walipofika Ofisini kwake kubadilishana Mawazo.
Wa kwanza kutoka Kushoto ni Makamu wa Rais wa Mahusiano wa Kampuni ya Kimataifa ya Millicom Group kutoka Miami Nchini Marekani Bibi Rachel Samren na wa kwanza Kulia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Zantel Bwana Brian Kalocola.
 Makamu wa Rais wa Mahusiano wa Kampuni ya Kimataifa ya Millicom Group kutoka Miami Nchini Marekani Bibi Rachel Samren Kushoto akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif Kulia na Bibi Rachel Samren wakifanya mzaha mara baada ya kukamilika kwa mazungumzo yao hapo Ofisini kwa Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Rais wa Mahusiano wa Kampuni ya Kimataifa ya Millicom Group kutoka Miami Nchini Marekani Bibi Rachel Samren alisema Taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuona huduma za mawasiliano zinawafikia Wananchi bila ya Matatizo.
Amesema Taasisi hiyo inayosimamia huduma za Mawasiliano ya Kampuni za Mitandao ya Simu za Mkononi za Zantel na Tigo imejipanga kitaalamu kuhakikisha kwamba kila Mwanajamii aliyejikubalisha kutumia Mawasiliano ya Kampuni hizo anaridhika na huduma zinazotolewa.
Bibi Rachel Samren akiuongoza Ujumbe wa Viongozi wa Kampuni za Tigo na Zantel alisema hayo wakati akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema Millicom Group kwa sasa imefikia hatua nzuri ya kuungwa mkono kwake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ushirikiano ambao hivi sasa umeshafikia asilimia 99.5%.
Bibi Rachel Samren alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba kinachosubiriwa kwa sasa ni kukamilika kwa asilimia 5% iliyobakia inayohusiana na masuala ya Kisheria.
Makamu wa Rais huyo wa Mahusiano wa Kampuni ya Kimataifa ya Millicom Group kutoka Miami Nchini Marekani Bibi Rachel Samren aliishukuru na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Watendaji wake waandamizi wa Serikali kwa hatua kubwa iliyofikiwa na mafanikio.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliuhakikishia Uongozi huo wa Kampuni ya Kimataifa ya Miricom Group kwamba Serikai ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa kila aina ya msaada katika kuona azma hiyo inafanikiwa vyema.
Balozi Seif alisema Serikali Kuu tayari imeshaazimia kukaribisha Taasisi na Makampuni ya Ndani na Nje ya Nchini katika kusaidiana na Serikali kwenye Sekta za Uwekezaji kwa lengo la kuimarisha Uchumi na kuongeza pato la taifa wakati maisha ya Jamii yataendelea kustawi zaidi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.