Habari za Punde

Mkutano wa SADC Wasekta ya Mazingira Maliasili na Utalii AICC Arusha.

Na.Faki Ali -Maelezo Zanzibar.(Arusha.) 17.10.2019                                        
Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa Sekta za Mazingira, Maliasili na Utalii wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC utakaofanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha AICC kuanzia tarehe 21 hadi tarehe 25 mwezi huu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Kituo cha AICC Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utlii Dkt. Aloyce Mzukwi alisema lengo la mkutano huo ni kuangalia mwenendo wa hali ya mazingira na mabdiliko ya tabianchi na kubainisha mkakati wa SADC wa Uchumi wa bahari na kutathmini maendeleo katika sekta za misitu, wanayamapori na Utalii.

Alisema mkutano wa Mawaziri wa sekta za Mazingira, Maliasili na Utalii utatanguliwa na mikutano ya wataalamu wa sekta ya wanyamapori utakaofanyika tarehe 18 na 19 na kufuatiwa na Mkutano wa Makatibu wakuu tarehe 21 hadi tarehe 24. 
Dkt. Mzukwi alisema mkutano wa Mawaziri wa sekta hizo tatu ni muendelezo wa mikutano ya SADC itakayofanyika nchini katika kipindi cha mwaka mmoja ambacho Tanzania ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo.

Aliongeza kuwa mkutano wa Mawaziri unatarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan siku ya Ijumaa tarehe 25 katika Ukumbi wa AICC Mjini Arusha.

Mapema mwezi Agosti mwaka huu, Serikikali ya Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa 39 wa SADC uliofanyika Mjini Dar es salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alikabidhiwa na kupokea jukumu la uenyekiti wa Jumuiya hiyo.

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ni moja ya Jumuiya za kikanda katika bara la Afrika iliyoanzishwa kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika nyanja za uchumi, ulinzi, siasa na usalama.

Nchi 16 wanachama wa SADC ni Angola, Botswana, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo DRC, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.         

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.