Habari za Punde

Serikali Kushirikiana na Wadau wa Maendeleo

Madungu Mohamed Shamte wa Skuli ya Sekondari ya Madungu akiendelea kupokea zawadi ya Laptop kwa ajili ya Skuli yake iliyotoa Wahitimu wa Daraja la Kwanza katika Mitihani ya Taifa ya Mwaka 2018 Kidato cha Sita.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Taifa linahitaji kuwa na Wataalamu wake lenyewe na hii itawezekana iwapo Wanafunzi wataelekeza nguvu zao katika Taaluma hasa ile fani ya Sayansi inayobeba kundi kubwa la Wataalamu hao.
Alisema Serikali Kuu kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo tayari imeshajipanga  kuendelea kuimarisha  Miundombinu ya Elimu ili Mtoto wa Taifa hili anafaidika na Matunda ya zao hilo lililotangazwa Bila ya Malipo na Muasisi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar  ya Mwaka 1964 Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati wa hafla maalum ya kuwazawadia Wanafunzi wa Chuo cha Kiislamu Micheweni zilizotolewa na Mfanyabishara Maarufu Nchini Said Nassir Nassor Bopar  kutekeleza ahadi aliyowapa wanafunzi hao miezi michache iliyopita.
Alisema wakati umefika hivi sasa kwa Wanafunzi wote Nchini kuacha mzaha na kujikita zaidi katika kuisaka  Elimu mahali popote pale kwa vile fursa za kufanya hivyo zipo za kutosha ambazo Serikali kupitia Wizara inayosimamia masuala ya Elimu imeshajenga mazingira rafiki kwao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa ushirikiano baina ya Wanafunzi wa jinsia zote, Walimu na Wazee ili kazi ya upatikanaji wa Eilimu kwa Wanafunzi wote iwe rahisi na kufikia mafanikio yaliyokusudiwa.
“ Jukumu letu kama Serikali limeshakamilika la kukutandikieni jamvi la kupata Taaluma kwa njia muwafaka. Sasa kazi ni kwenu kuchangamkia fursa hizo”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Wanafunzi hao na wengine Nchini kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado ina nia ya kumuona Mtoto wa Visiwa vya Zanzibar  mwenye kipaji anakamilisha kiu yake ya kujipatia Elimu kwa mujibu wa matakwa yake.
Alisema Rais wa Zanzibar katika kutilia mkazo suala hilo kila Mwaka amekuwa akiongeza ufadhili kwa Wanafunzi wanaofaulu vyema wa Daraja la kwanza kuendelea na masomo yao ya juu iwe ndani au nje ya Nchi akianzia na nafasi Tano na Mwaka huu ameshafikisha Nafasi 60.
Balozi Seif Ali Iddi alimpongeza na Kumshukuru Mfanyabiashara Maarufu Nchini Said Nassir Nassor  {Bopar} kwa moyo wake wa Kizalendo unaomsukuma kila mara kuunga mkono jitihada za Maendeleo zinazowazunguuka Wananchi katika maeneo mbali mbali Nchini.
Alisema mchango mkubwa unaotolewa na Mzalendo huyo utaendelea kuthaminiwa na Serikali kwa vile hulenga moja kwa moja kwa Jamii katika kupunguza changamoto zinazowakwaza katika maisha yao ya kila siku hasa katika Sekta ya Elimu na Afya.
Mapema akitoa ufafanuzi wa kukamilisha Ahadi alizotoa kwa Wanafunzi hao wa Chuo cha Kiislamu Micheweni Mfanyabiashara Said Nassir Nassor {Bopar} aliwaasa Wanafunzi hao kwa kuwatahadharisha kwamba bila ya Elimu Mwanaadamu kamwe hawezi kujifanyia chochote cha uhakika katika maisha yake.
Hata hivyo Bopar  alisema Elimu hiyo iwapo haitazingatia hekma na busara Mwanafunzi hasa Mtoto wa Kike inaweza kumletea mashaka hasa kipindi hichi kilichokumbwa na mfumko wa matendo maovu ya udhalilishaji wa Kijinsia unaowapotezea muelekeo wa Elimu wakati mwengine.
Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma alisema Wizara hiyo itaendelea kushirikiana na Wadau wa Sekta ya Elimu katika kuona Vijana wa Zanzibar wanajikomboa Kielimu.
Waziri Riziki alimshukuru Mfanyabiashara Said Nassir Nassor  Bopar kwa kufanya uungwana wa kutekeleza ahadi anazotoa katika Sekta ya Elimu ambazo zinaendelea kuleta faraja kubwa kwa Wanafunzi, Walimu pamoja na Wazazi kwa ujumla.
Alisema wapo Wafanyabiashara wengi wenye uwezo mkubwa zaidi ya Bwana Bopar lakini bado wanaendelea kuwa wazito wa kufunua mikono yao katika kuisaidia Jamii hapa Nchini.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikabidhi Chakula kwa Uongozi wa Hospitali ya Vitongoji pamoja na kugawa Miwani kwa Wanafunzi 119 vyote vimetolewa na Mfanyabiashara Maarufu Nchini Said Nassir Nassor {Bopar} kukamilisha ahadi aliyotowa Miezi Miwili iliyopita.
Hafla hiyo fupi  iliyohudhuriwa pia na Viongozi wa Serikali, Kisiasa na Wazazi imefanyika katika Ukumbi wa Kiwanda cha Mafuta ya Makonyo kiliyopo Wawi Chake Chake Kisiwani Pemba.
Akizungumza na Wananchi hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitahadharisha Vifaa na Misaada inayotolewa na Wahisani lazima ilengwe na kuwafikia wale walinaousudiwa.
Balozi Seif alisema wapo baadhi ya watendaji na matukio yameshawahi kuripotiwa wakiwa na tabia ya udokozi inayoondoa uaminifu na wakati mwengine tabia hiyo huwavunja moyo wale wanaoamua kujitolea kutoa misaada.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwanasihi Wanafunzi waliobahatika kupata msaada wa Miwani kuendelea kuzitunza ili zidumu mwa muda mrefu kwa vile zimetengenezwa kwa gharama kubwa nje ya Nchi.
Mapema Afisa Mdhamini Wizara ya Afya Pemba Bibi Shadya Shaaban Seif alisema Wanafunzi kati ya 18,000 na 16,000 wa Skuli 146 Kisiwani Pemba wamefanyiwa uchunguzi wa maradhi ya macho ndani ya Mwaka huu wa 2019.
Bibi Shadya alisema kati ya hao Wanafunzi 88 wa Kike na 31 wa Kiume wamebainika kuwa na uoni mdogo wa Macho jambo ambalo lilipelekea kupatiwa msaada wa Miwani ili waweze kudumu vyema masomo yao.
Hata hivyo Afisa Mdhamini huyo wa Wizara ya Afya Pemba  alisema licha ya huduma za macho kuendelea kutolewa bure lakini bado njia sahihi ya kuepukana na tatizo hilo ni kwa Jamii kuendeleza Utamaduni wa kupenda kula Matunda na Mboga mboga mara kwa mara ili kujihakikishia Afya bora.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.