Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Oktoba 20, 2019 ameondoka chini kwenda Urusi ambako atamwakilisha Rais Dkt.John Pombe Magufuli katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika na Urusi. Pichani, Waziri Mkuu akisalimiana na Spika wa Bunge Job Ndugai kwenye Uwanja Ndege wa Julius Nyerere kabla ya kuondoka. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Mhe.Kassim Majaliwa ameondoka nchini juzi (Jumapili, Oktoba 20, 2019) kwenda Urusi kuhudhuria mkutano baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi (Russia-Africa Summit), utakaofanyika jijini Sochi, Urusi, Oktoba 23 – 24, 2019.
Waziri Mkuu anahudhuria mkutano huo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli.
Mkutano huo utakaoendeshwa chini ya uenyekiti wa pamoja (Co-chaired) wa Rais wa Shirikisho la Urusi, Vladimir Putin, na Rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sisi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), unalenga kurejesha na kuimarisha uhusiano baina ya mataifa ya Afrika na Urusi ambao uliyumba baada ya kusambaratika kwa “Union of Soviet Socialist Republic” (USSR) mwaka 1991.
Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali utafanyika katika sehemu mbili, ambazo ni Kongamano la Biashara (Russia Business Forum) linalotarajiwa kufanyika Oktoba 23, na Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi za Urusi na Afrika uliopangwa kufanyika Oktoba 24, 2019.
Waziri Mkuu atashiriki kwenye mikutano yote miwili.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, OKTOBA 20, 2019
No comments:
Post a Comment