Habari za Punde

Jeshi la Mageresza Mkoani Simiyu Mbioni Kuanza Kilimo cha Pamba.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Simiyu, alipowasili leo kwa ziara ya kikazi inayohusu Jeshi la Magereza mkoani humo kuanza kilimo cha pamba kwa kutumia ardhi na nguvukazi ya wafungwa walionao.Wapili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Na Mwandishi Wetu, Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amelitaka Jeshi la Magereza kutumia jumla ya Ekali Elfu Tatu na Sabini na Moja  zilizopo mkoani hapo kwa kilimo cha pamba ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt.John Magufuli la kutaka jeshi hilo kubadilika na kuingia kwenye mfumo wa uzalishaji ili liweze kuondokana na mfumo wa kutegemea bajeti kuu ya Serikali kulisha wafungwa nchini.
Ameyasema hayo  wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni mkoani hapo lengo ikiwa ukaguzi wa shughuli za taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo na kuangalia fursa zinazopatikana katika mikoa mbalimbali nchini ili kuweza kulibadilisha jeshi la magereza.
“Mheshimiwa naibu waziri sisi kama mkoa tuko tayari kushikana na jeshi la magereza kwani kuna ardhi ya kutosha na naomba nikuhakikishie hawa wakilima pamba japo ekali mia moja tu na zikauzwa wataweza kufanya mambo mengi ya maendeleo ikiwemo kujenga nyumba za kuishi askari ambazo zitakua ni za kiwango cha juu,” alisema Mtaka.
Akizungumza katika ziara hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni alisema Serikali imelipokea jambo hilo kwani ndio lengo hasa la serikali kuona jeshi la magereza linajitegemea katika uendeshaji wake pasipo kutegemea bajeti kuu ya serikali.
“Mheshimiwa Rais alishatuagiza tulibadilishe jeshi hili la magereza na tayari tushaanza na tumetenga magereza kumi ya kimkakati nchini ambayo yameteuliwa kuleta mapinduzi katika jeshi, ziara hii ni kuona fursa zilizopo katika mikoa mingine kupitia magereza,nakuahidi jambo hilo tumelichukua kama wizara na muda si mrefu litapatiwa ufumbuzi,” alisema Masauni.
Naibu Waziri Masauni pia alipata nafasi ya kutembelea Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Busega na kuzungumza na mahabusu waliopo kituoni hapo ambapo akuridhishwa na hali ya uchafu katika chumba cha mahabusu kituoni hapo na kuuagiza uongozi kufanya utaratibu wa kusafishwa kwani waliopo ndani ni binadamu na wana haki zao ikiwepo kukaa sehemu safi ili kulinda afya zao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.