Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akikata utepe kuashiria kuizindua Boti Mpya ya Kisasa ya Kampuni ya Uvuvi Zanzibar (ZAFICO) Sehewa 2, kushoto kwa Rais Naibu Waziri wa Kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi Zanzibar.Dkt. Makame Ali Ussi, hafla hiyo ya uzindizi imefanyika katika eneo la Hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar leo, 2-12-2019.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba kwa
kuzingatia kuwa bado eneo la bahari la Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania halijatumika ipasavyo katika sekta ya uvuvi imeanza jitihada na
mikakati ya kuhakikisha sekta hiyo inaimarika.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo zilizofanyika
huko katika eneo la Hoteli ya Verde Mtoni, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar katika
uzinduzi wa boti mpya ya Uvuvi “Sehewa 02” inayomilikiwa na Kampuni ya Uvuvi
Zanzibar (ZAFICO) hafla iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa boti 3 za doria
zinazomilikiwa na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, katika Idara ya
Maendeleo ya Uvuvi.
Katika maelezo yake,
Rais Dk. Shein alisema kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina eneo la
Ukanda Maalum wa Bahari wa Kiuchumi (EEZ) lenye ukubwa wa kilomita za mraba
zipatazo 223,000 eneo ambalo litatoa fursa ya kuwekeza katika uvuvi wa Bahari
Kuu ambapo samaki wakubwa wa aina ya jodari na jamii yake na wengine wa aina
mbali mbali wanapatikana kwa wingi.
Rais Dk. Shein
alieleza kuwa bado kunalazimika kuziruhusu meli za kigeni kuendesha shughuli za
uvuvi, kwa makubaliano maalumu ikiwa ni njia moja ya kunufaika na rasilimamali
za baharini.
Alieleza kuwa uvuvi
katika eneo la Bahari Kuu kwa sasa unafanyika kupitia meli kubwa za kigeni
ambazo huwa zimepatiwa leseni za uvuvi kutoka Mamlaka ya Bahari Kuu ambapo hadi
sasa wastani wa meli 100 za kigeni zinavua katika ukanda huo kwa mwaka.
Alisema kuwa jumla ya
tani 12,276.2 za samaki wa aina ya Jodari na jamii zake zimevuliwa na meli
kutoka nchi za Taiwan,Oman, Seychelles, Korea, Thailand, China, France, Spain
na Mauritius ambazo zimepewa leseni ya uvuvi wa bahari kuu na Mamlaka ya Uvuvi
wa Bahari Kuu.
Hivyo, alieleza haja
ya kuongeza bidii katika kuzitumia wenyewe rasilimali za bahari ili kuweza
kufaidika moja kwa moja na matunda yake badala ya kusubiri kupokea faida kutoka
mkono wa pili. “Hali hii inakwenda sambamba na methali isemayo “Kivuli cha
mvumo, huwafunika walio mbali” alisisitiza Rais Dk. Shein.
Rais Dk. Shein
aliongeza kuwa Serikali imeunda upya Kampuni ya Uvuvi ya Zanzibar, “Zanzibar
Fisheries Company-ZAFICO” na imetafutiwa vifaa na nyenzo za kisasa za
kuendeleza sekta ya uvuvi, ili kuweza kufanya matumizi bora ya bahari na
hatimae kuleta tija.
Alieleza kwamba
Shirika hilo lilikuwepo hapo kabla lililoanzishwa mwaka 1974 likijulikana kwa
jina la “ZAFICO- Zanzibar Fisheries Coporation” ambalo ofisi zake zilikuwa eneo
la Malindi ambalo lengo lake kuu la kuanzishwa kwake ilikuwa ni kukuza sekta ya
uvuvi na kuongeza upatikanaji wa samaki kwa wananchi wa Zanzibar.
Hivyo, Rais Dk. Shein
alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba, iliamua kuunda
Kampuni ya Uvuvi Zanzibar (ZAFICO) kupitia Sheria Namb.15 mwaka 2013, ya
usajili wa Makampuni Zanzibar kama ni hatua muhimu ya utekelezaji wa mipango na
mikakati ya kuimarisha sekta ya uvuvi.
Alisisitiza kuwa hayo
yote ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020
ambayo inasisitiza juu ya uimarishaji wa sekta ya uvuvi.
Aidha, Rais Dk. Shein
alisema kwamba historia inaeleza kwamba wavuvi ndio wakaazi wa mwanzo
waliohamia Zanzibar kutoka sehemu za Bara ambao waliishi katika eneo la
Shangani, hivyo kuna kila sabahu ya kuiendeleza kazi hiyo ya uvuvi kwa kadri
teknolojia inavyoimarika.
“Uvuvi kwetu ni kazi
ya jadi, Wahenga walisema “Mkataa asili si mjasiri” kwa hivyo, na sisi ni
lazima tuwe wajasiri katika kuziendeleza kazi za asili tulizozirithi kwa wazee
wetu, ambazo ni za halali na zenye tija kwetu”,alisema Dk. Shein.
Alieleza kuwa kwa muda
mrefu wavuvi wamekuwa wakivua katika maeneo ya bahari yaliyo karibu ambayo
tayari yameashiria upungufu wa upatikanaji wa samaki ambapo shughuli za uvuvi za kila siku katika maeneo hayo zinapelekea
kuwa tishio kubwa kwa mazingira ya bahari.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alisema kuwa mipango ya kuimarisha uchumi wa bahari inaendelea vizuri
hapa nchini ikiwa ni pamoja na jitihada za kununua vyombo vipya vya baharini
vilivyo na ubora pamoja na kuwashajiisha wawekezaji kuewekeza katika eneo hilo.
Alieleza kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuunda Idara itakayokuwa katika Wizara ya
Fedha na Mipango (Tume ya Mipango), ili iweze kusimamia uchumi wa bahari huku
akieleza kwamba tayari wameshajitokeza Washirika wa Maendeleo kuunga mkono eneo
hilo.
Alieleza kuwa Serikali
imepata ufadhili wa Dola za Kimarekani milioni 8.8 kutoka Mfuko wa Kimataifa wa
Maendeleo ya Kilimo (IFAD), ambazo zitatumika katika kuimarisha sekta ya
kilimo, mifugo na uvuvi ambapo pia, fedha hizo zitatumika kwa kujengea viwanda
vidogo vidogo vya kusarifu samaki na mazao mengine ya baharini Unguja na Pemba.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa ili boti hizo zifanye kazi zake vizuri lazima kuhakikishwe kwamba wapo
wataalamu wazuri wa kuziendesha na kuzishughulikia huku akitaka kutumiwa vizuri
boti za doria kwa ajili ya kulinda maeneo ya bahari, fukwe na rasilimali za
bahari ambazo baadhi yao ni muhimu kwa sekta ya utalii ambayo ni muhimu mkuu wa
uchumi.
Alieleza kuwa ili
sekta ya uvuvi pamoja na Kampuni ya (ZAFICO) iweze kupiga hatua na kupata
maendeleo ya haraka, inahitaji ishirikiane na Taasisi mbali mbali za umma na
binafsi huku akiwataka viongozi wa (ZAFICO) kuwa wabunifu na wajenga ari ya
kujifunza zaidi.
Alisisitiza haja ya
kujitathmini utendaji wa kazi zao kwa kufanya rejea za yale mambo ambayo
yalipelekea (ZAFICO) ya mwanzo kuanguka. Pia alipongeza ujumbe wa sherehe hizo
usemao “Tuimarishe uchumi wa bahari”.
Nae Waziri wa Wizara
ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mmanga Mjengo Mjawiri alisema kwamba
Serikali imegharimu fedha nyingi katika ununuzi wa boti hizo hatua ambayo ni
miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.
Aliongeza kuwa
mafanikio ya ununuzi wa boti hizo sambamba na kuifufua upya Kampuni ya ZAFICO
yote hayo yanatokana na usimamizi imara wa Rais Dk. Shein katika kuhakikisha sekta
ya utalii inaimarika.
Mapema Katibu Mkuu wa
Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mariam Juma Saadallah alisema kuwa Boti ya ZAFICO
imetengenezwa nchini SriLanka na Kampuni ya Hairu Naval Craft Engineering Ltd
ikiwa na urefu wa mita 18.5m na upana mita 5.1m kwa thamani ya TZS Bilioni
1,130.000.
Aidha, alisema kuwa
katika kuimarisha ulizni wa bahari na kupambana na uvuvi haramu, Idara ya
Maendeleo ya Uvuvi kupitia Mradi wa SWIOFish umenunua boti 3 za doria kutoka
kampuni ya ‘TOM CAT BOAT BUILDINGS’ iliopo Afrika ya Kusini kupitia Kampuni ya
Kizalendo ya hapa Zanzibar iitwayo Visiwani Traders ambapo boti hizo zilizogharimu
jumla ya TZS 583,165,440.
Mapema Rais Dk. Shein
aliizindua Boti hiyo na kupata maelezo kutoka kwa wafanyakazi pamoja na
viongozi wa ZAFICO akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Zahor Kassin
Mohammed ambapo pia, alipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya
Maendeleo ya Uvuvi Mussa Aboud Jumbe kuhusiana na Boti hizo 3 za doria.
Pia, Rais Dk. Shein
alipata fursa ya kutembelea banda la Wajasiriamali walikuwa wakiuza bidhaa
mbali mbali zikiwemo zile zinazotokana na rasilimali za bahari ambapo pia,
wakati huo huo alikabidhi vifaa vya uvuvi zikiwemo mashine, nyavu na vihori kwa
vikundi vya uvuvi kutoka Wilaya mbali mbali hapa nchini.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment