Habari za Punde

SHULE YA MSINGI MWISENGE KUWA NA MAJENGO YA KISASA - MAJALIWA



SERIKALI imeamua kuifanyia ukarabati mkubwa shule ya msingi Mwisenge ambayo alisoma Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere ili iwe sehemu ya historia ya Tanzania.

Akizungumza mara baada ya kutembelea shule hiyo jana (Jumamosi, Desemba 7, 2019), Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeamua kuifanya shule hiyo iliyopo kwenye manispaa ya Musoma iwe sehemu ya historia ya Mwalimu Nyerere pamoja na historia ya Tanzania kwa ujumla.

“Shule hiyo haiwezi kubeba historia ya Mwalimu Nyerere, endapo majengo na miundombinu ya shule hiyo haitakarabatiwa na kujengwa upya,” amesema na kuongeza kuwa: “Mipango ya kuifanya shule hiyo iwe sehemu ya historia ya Tanzania inaendelea serikalini; na kwamba historia ya Baba wa Taifa itapatikana shuleni hapo.” 

Amesema baada ya mchakato huo kukamilika, shule ya msingi Mwisenge itaubeba mkoa wa Mara na nchi ya Tanzania kwa ujumla.

Amesema kuwa uamuzi wa kufanya shule hiyo kuwa shule yenye historia ya Tanzania unatokana na viongozi mbalimbali wa Tanzania kusomea shuleni hapo ambapo amewataja Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Jaji Joseph Warioba na Mzee Joseph Butiku kuwa ni miongoni mwa viongozi wa kitaifa waliosoma kwenye shule hiyo.

Amewapongeza viongozi wa mkoa wa Mara kwa kusimamia matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya shule hiyo na akawataka viongozi wengine wa umma waige mfano huo.

Mapema, akitoa taarifa ya ukarabati wa shule hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma, Bi. Fidelica Myovela amesema kuwa manispaa yake inahitaji zaidi ya sh. milioni 161 ili kukamilisha ukarabati wa shule hiyo ambao tayari umeanza.

Amesema kuwa hadi sasa wamepokea zaidi ya sh. milioni 772.6 kutoka TAMISEMI kwa ajili ya ukarabati huo ambapo hadi sasa wamekwishafanya ukarabati kwa asilimia 85 ya kazi yote.

Amesema kuwa kati ya fedha hizo, jumla ya sh. milioni 20 zilitolewa na Rais Magufuli Septemba, mwaka jana ambaye pia aliagiza tathmini ya gharama za ujenzi na ukarabati wa miundombinu shuleni hapo ianze mara moja.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, DESEMBA 8, 2019.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.