Habari za Punde

Waziri wa Kazi Uwezeshaji Wazee Wanawake na Watoto Mhe.Maudline Castico Afungua Kongamano la Kilele Cha Maadhimisho ya Siku 16 za Wanaharakati Kupinga Vitendo Vya Uzalilishaji na Ukatili.

Na Mwashungi  Tahir    Maelezo.
Waziri wa Kazi Uwezeshaji Wazee Wanawake na Watoto.Mhe.Maudline Cyrus Castico amesema elimu bado inahitajika kutolewa kwa upana zaidi katika jamii ili kudhibiti vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ambavyo vimeshamiri nchini.
Hayo ameyasema Waziri wa Vijana,Utamaduni, Sanaa na Michezo  Ali Abeid Karume kwa niaba ya Waziri wa Kazi Uwezeshaji Wazee Wanawake na Watoto Moudline Cyrus Castico katika Kongamano la  kilele cha Maadhimisho ya siku 16 za Wanaharakati wa Kupinga Vitendo vya Ukatili wa Kijinsia huko katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil ulioko Kikwajuni.
Amesema Serikali imeandaa mpango kazi wa Kitaifa kwa kushirikiana na masheha katika utoaji wa elimu ili vitendo hivi viweze kupungua au kumalizika kabisa iwapo jamii itaelimika kupitia kwenye shehia zao.
Aidha amesema Wizara inafanya kazi kwa karibu na Masheha, Waratibu wa Wanawake na watoto kupitia kwenye kamati zao ambao ni kiungo muhimu kati ya Wizara na Jamii katika kushughulikia matukio yanayotokea na kupokea taarifa pamoja na kufuatilia mwenendo wa kesi katika maeneo yao.
Pia amesema anawapongeza wadau wote nchini kwa juhudi kubwa za kupambana na vitendo vya ukatili na  udhalilishaji wa kijinsia.
Hivyo amsema matunda ya juhudi hizi yanaonekana wazi kwa kuona kasi ya kutoa taarifa ya vitendo hivi inaongezeka na kuondoa suala la kuvifumbia macho vitendo hivyo hatua kwa hatua.
Akitoa wito kwa wadau mbali mbali kwa kuunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuondoa tatizo hilo na  imewataka wazazi na walezi na jamii kwa ujumla  kuongeza juhudi ya kuzuia vitendo hivyo katika maeneo mbali mbali kwani Kinga ni Bora kuliko kutibu.
Hata hivyo aliitaka jamii kuondosha muhali linapotokea vitendo hivyo isisite kuripoti mnamohusika  na kuhakikisha muhanga anapata huduma za kimatibabu na kuchukuliwa hatua za kisheria ili kuepuka athari isiendelee zaidi.
Nae Mwanaharakati wa Chama cha Wanasheria wanawake Zanzibar Zafela             Jamila Mahmoud  amesema ili kupungua au kuondosha vitendo vya udhalilishaji lazima watoto waache kuangalia masuala ya ngono katika mitandao.
Pia vijana wa kiume kuacha kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume kwani hili linachangia kubaka na pia elimu inahitajika zaidi katika kupinga suala la udhalilishaji wa kijinsia.
Mada zilizowasilishwa katika Kongamano hilo la siku moja. ni Vijana na watoto katika Mapambano ya vitendo Ukatili na Udhalilishaji, Wajibu wa Ushiriki wa vyombo vya Habari  katika kupambana na Vitendo vya ukatili na Udhalilishaji , Sheria  dhidi ya Vitendo vya ukatili na udhalilishaji na utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kupambana na Vitendo vya Ukatili na Udhalilishwaji wa Wanawake na Watoto (2017-2022).
Kauli mbiu wa Kongamano hilo ni Imarisha Usawa Pambana na Udhalilishaji pinga Ukatili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.