Habari za Punde

“KILA MTANZANIA ANAWEZA KUWEKEZA, TUMIENI FURSA ZILIZOPO” WAZIRI KAIRUKI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akioneshwa namna maziwa yanavyo poozwa katika makonteni maalum baada ya kuchemshwa ili kutengeneza mtindi katika kiwanda cha kuchakata maziwa cha Mather Dairies kilichopo Ikwiriri Wilaya ya Rufiji mkoa wa pwani alipotembela kukagua kiwandani hapo Januari 23, 2020. Anayetoa maelezo hayo ni Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho Mzee Abdallah Nyarando
Na. Mwandishi Wetu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji nchini Mhe. Angellah Kairuki amewaasa wananchi kuthubutu uwekezaji katika maeneo yenye tija kwa kuzitumia fursa za uwekezaji zilizopo ili kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo yao na nchi kwa ujumla.
Ametoa kauli hiyo tarehe 23 Januari, 2020 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kiwanda cha kuchakata maziwa ya mtindi cha Mather Dairies kilichopo Kijiji cha Ikwiriri Wilaya ya Rufiji katika Mkoa wa Pwani alipotembelea kiwandani hapo ikiwa ni eneo la mwisho kutembelea katika ziara yake ya siku 6 Mkoa wa Pwani.
Akiwa katika kiwanda hicho kilichowekeza mtaji wa zaidi ya milioni 300 chenye uwezo wa kuchakata zaidi ya lita 2000 kwa siku ambazo hutengeneza maziwa ya mtindi aina ya Yogurt Full Manyonyo, waziri alitoa hamasa hiyo kwa Watanzania kuzichangamkia fursa na kuwatoa shaka kuwa hakuna Mwananchi asiyeweza kuwekeza kikubwa ni kuwa na nia na uthubutu.
“Ni ukweli kuwa, kila uwekezaji Mtanzania anaweza kuufanya muhimu kuwa na ujuzi, teknolojia pamoja na mtaji pasipo kutia shaka na kujiamini,”alifafanua Waziri Kairuki
Aliongezea kuwa, ikiwa uwezo wa kuwekeza ni mdogo kwa kuzingatia ukosefu wa ujuzi wananchi wanapaswa kutumia fursa za mafunzo ya ukuzaji ujuzi unaotolewa katika vyuo mbalimbali na kutumia watu wenye uzoefu inapofaa kulingana na aina ya uwekezaji unaotaka kuufanya.
Aliwaasa watanzania kuacha tabia ya kukatishana tamaa na kuona namna ya kushikamana kuweza kuwekeza katika sekta mbalimbali.
“Kumekuwa na tabia ya kukatishana tamaa pindi mtu anapothubutu kuona fursa na kuichangamkia, ni rai yangu kwa wananchi kuona watanzania tunawekeza kufanya mambo makubwa katika maeneo yote yenye fursa, na kuzitumia vyema mamlaka zilizopo kwa kupata msaada ya ushauri elekezi na miongozo ya namna bora ya kuwekeza,”alifafanua
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho Mzee Abdallah Nyarando alieleza namna alivyoanza uwekezaji wake mwaka 2010 kwa mtaji wa shilingi milioni 20 na hadi kukamilika kwa kiwanda hicho ametumia jumla ya shilingi Milioni 300, na kuweza lengo ni kuongeza thamani ya maziwa, kuzalisha ajira na kujipatia kipato.
 “Kiwanda hiki kimeweza kusaidia zaidi ya vijana 12 ambao wamekuwa wa msaada katika kuzalisha na kuuza maziwa maeneo mablimbali nchini ikiwemo; Masasi, Kibiti, Rufiji, Mtwara na Dar es Salaam,”alisema Mzee Nyarando.
Alitoa wito kwa wananchi kuondokana na hofu za kuwekeza katika maeneo mbalimbali na kueleza zipo faidi za kuwekeza katika nchi yao na kujipatia kipato ili kujikwamua kiuchumi.
Akiwasilisha taarifa yake kwa Waziri Kairuki Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Mhe. Juma Njwayo alieleza kuwa Tanzania ina fursa nyingi za kusaidia kundi kubwa la vijana katika kujikwamua kiuchumi kwa kuangalia maeneo muhimu ya uwekezaji katika Nyanja mbalimbali.
Aliongezea kuwa, wananchi hawana budi kujiajiri kwa kutumia nguvu kazi walizonazo na kuzichangamkia fursa za Wilaya yake ambazo alizibaini ni pamoja na shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi na biashara na kuwataka kuzitumia kwa kuzingatia uwepo wa miundombinu muhimu ya kuvutia uwekezaji.
“Wilaya yetu ina vivutio vingi ikiwemo ardhi inayokubali mazao mbalimbali kama mahindi, mpunga, korosho, mazao jamii ya mikunde na mbogamboga  na matunda aina ya matikiti hivyo zitumieni kwa tija na kuhakikisha tunaondokana na ukosefu wa ajira,”alieleza Juma
Alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa wawekezaji kuona maeneo yenye rutuba na kuwekeza katika mazao hayo na kubainisha fursa zilizopo katika ufugaji kwa kuzingatia uwepo wa mabwawa ya asili maji katika wilaya hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akiangalia namna maziwa aina ya Yogurt yaliyohifadhiwa katika chupa maalum tayari kwa kuuza alipotembelea kiwanda cha kuchakata maziwa cha Mather dairies kilichopo Ikwiriri Wilaya ya Rufiji Mkaoa wa Pwani 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akipokea taarifa ya kiwanda cha kuchakata maziwa cha Mather Dairies maarufu kwa jina la manyonyo kutoka kwa Meneja wa kiwanda hicho Bw. Hamis Abdallah mara baada ya kuiwasilisha kwake.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akiangalia moja ya pakiti iliyo na bacteria maalum wanaotumika kuchachusha na kugandisha maziwa ili kutengeneza maziwa mtindi katika kiwanda hicho.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akisalimiana na baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha kuchakata maziwa cha Mather Dairies alipowasili kiwandani hapo kukagua shughuli za uzalishaji huo
Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Kuchakata maziwa cha Mather Dairies Mzee Abdallah Nyarando akitoa maelezo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki kuhusu mtambo wa kupooza maziwa akiwa kiwandani hapo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Kuchakata maziwa cha Mather Dairies Mzee Abdallah Nyarando pamoja na mke wake wakati wa ziara yake kiwandani hapo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watendaji wa Ofisi yake, wa Wilaya ya Rufiji pamoja na wafanyakazi wa kiwanda cha kuchakata maziwa cha Mather Dairies mara baada ya kumaliza ziara yake kiwandani hapo.

(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.