Habari za Punde

SERIKALI YATOA AGIZO KWA WANAOSOMA CHINA


Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewataka wazazi na walezi wenye watoto wanaosoma China ambao wapo nchini kwa likizo wasiwaruhusu warudi hadi hapo Serikali itakapotangaza.

Hatua hiyo inatokana na China kukumbwa na mlipuko wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona. “Tunawasihi watoto wasirudi hadi hapo tutakapopata taarifa za kidiplomasia kuhusiana na maendeleo ya ugonjwa huo.”

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Januari 30, 2020) wakati akijibu swali la Mbunge wa Mafinga Mjini, Mheshimiwa Cosato Chumi katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma. Mbunge huyo alitaka kujua namna 
Serikali ilivyojipanga kukabiliana na homa hiyo pamoja na baa la nzige.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema ni kweli China kuna mlipuko wa homa hiyo ya mapafu ambayo hadi sasa imepoteza maisha ya watu wengi na tayari baadhi ya nchi jirani nazo wananchi wake wameanza kupata maambukizi. “Watoto wasirudi hali ikikaa vizuri warudi China kuendelea na masomo na ikiwa vinginevyo Serikali itatafuta utaratibu mwingine.”

Amesema tayari Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameshatoa taarifa kwa umma kuhusu ugonjwa huo na aliwahakikishia Watanzania kuwa homa hiyo haijaingia nchini.

Waziri Mkuu amesema: “Katika kukabiliana na homa hiyo, Serikali imejipanga kwa kuimarisha mawasiliano na ubalozi wetu huko China ili kujua hali inaendeleaje, na Balozi wa Tanzania nchini China, Balozi Mbelwa Kairuki anafanya kazi hiyo ya kutoa mrejesho wa kila siku wa hali ilivyo huko.”

Amesema licha ya kutuma mrejesho, pia Balozi huyo anafanya kazi nzuri ya kutoa elimu kwa Watanzania kwa kutafuta madaktari wa Kitanzania ambao wamejifunza ugonjwa huo na kuwaelimisha Watanzania waliopo nchini China namna ya kujikinga na homa hiyo.

Akizungumzia baa la nzige lililoikumba nchi jirani ya Kenya, Waziri Mkuu amesema kuwa tayari Serikali imeshachukua tahadhari ambapo Wizara ya Kilimo ya Tanzania inashirikiana na ya Kenya kumaliza tatizo hilo. Pia amewataka wananchi wanaoishi kwenye mikoa, wilaya na vijiji vilivyo mipakani, watoe taarifa mara watakapowaona wadudu hao.

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI, JANUARI 30, 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.