Habari za Punde

WAZIRI MKUU, KASSIM MAJALIWA, AKUTANA NA WAFANYABIASHARA WA KOROSHO WA MKOA WA LINDI NA MTWARA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Naibu Waziri Wizara ya Kilimo, Wakuu wa Wilaya wa Mkoa wa Lindi na Mtwara, Mkatibu Tawala wa Mikoa hiyo, Wakurugenzi  wa Benki ya TADB na CPB, katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi, kabla ya kikao na Wafanyabiashara wa korosho wa Mikoa hiyo,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Wafanyabiashara wa korosho wa Mkoa wa Mtwara na Lindi, katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Januari 3, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo ihakikishe asilimia tatu ya wakulima wa zao la korosho waliosalia wanahakikiwa na kulipwa.

Hadi sasa zaidi ya asilimia 96 ya wakulima wa korosho waliouza korosho zao katika msimu wa 2018/2019 wameshahakikiwa na kulipwa.

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Januari 3, 2020) wakati alipokutana na baadhi ya wakulima wa korosho kutoka wilaya za Ruangwa, Masasi na Tandahimba.

Baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima hao, Waziri Mkuu amewataka waendelee kuwa na subira na kwamba haki yao itapatikana.

 “Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ipo makini, hivyo hakuna Mtanzania yeyote atakayepoteza haki yake.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wanachama wa vyama vya ushirika pale watakapoona ushirika wao hauendi vizuri wasisite kutoa taarifa Serikalini.

Amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya wawachukulie hatua viongozi wote wa vyama vya ushirika watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Kwa upande wao, wakulima wameishukuru Serikali kwa kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi na kwamba wanaimani ya kulipwa madai yao.

Mmoja wa wakulima hao Bi. Mariamu Mganda amesema anamshukuru Waziri Mkuu kwa kukubali kuwasikiliza kwani wamepata tumaini la kulipwa fedha zao.

Mkulima Mwingine Bw. Abdulkareem Said amesema ameridhishwa na utendaji kazi wa Serikali hususan baada ya Waziri Mkuu kukubali kusikiliza kero zao.

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU

IJUMAA, JANUARI 3, 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.