Habari za Punde

KAMATI YA UVUVI YA FUMBA YAPEWA MAFUNZO YA KUJIKINGA NA MAAFA BAHARINI

Afisa Elimu Msaidizi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Aziza Ali Rajabu akitoa mafunzo kwa Wajumbe wa  Kamati ya Uvuvi  Fumba kuhusu maafa huko  katika Ofisi ya Sheha wa Fumba Wilaya Magharibi B 
Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar 12/02/2020.                                                                        
Afisa Elimu kutoka Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Haji Ame Haji amewataka wavuvi kuzingatia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa ili kujiepusha na maafa 
Hayo aliyasema katika Ofisi ya Sheha wa Fumba  wakati akitoa mafunzo kwa Wajumbe wa  Kamati za Uvuvi huko katika kijiji cha Fumba Wilaya Magharibi B.
Afisa elimu huyo alisema mafunzo ya Wajumbe wa Kamati  ya Uvuvi yatasaidia kupata taaluma ya kujikinga na maafa na kuzingatia taarifa  zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa pamoja na kutumia uzoefu wa asili katika kujiandaa kukabiliana na maafa .
Aidha alisema elimu hiyo itawajengea uwezo  na mbinu za kujikinga na majanga pamoja na kupunguza adhari za maafa yanapotokea ambayo baadhi ya wakati hutokea bila kuonyesha ishara kabla .
Alieleza kuwa maafa yanaweza kutokezea kwa viwango tofauti ikiwemo ya mtu mmoja mmoja ya jamii na hata taifa kwa ujumla .
Nae Afisa Elimu Msaidizi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa  Zanzibar Aziza Ali Rajabu alisema elimu kwa kamati za uvuvi inasaidia katika kujiandaa kabla maafa kutokea.
Alifahamisha kuwa wavuvi wanatakiwa kuwa makini pindipo watapata matatizo ya bahari ili kuweza kuitumia mbinu ya kujiokoa maisha yao bila ya kujali hasara watakayoipata .
“Unatakiwa ujiokoe wewe na utoe msaada kwa wengine wakiwemo Watoto wadogo, Walemavu pamoja na watu Wazima ambao hali zao ni dhaifu na wanaohitaji msaada.”alisema Afisa huyo .
Aliitaka kamati hiyo kuimarisha mawasiliano na wavuvi pamoja uwokozi ili kuwepo na msaada wa haraka na tahadhari za mapema juu ya usalama wao pindipo wakiwa katika kazi zao .
Aliwashauri wavuvi kuhakikisha kuwa wanachukuwa zana za kujiokoa wakati wa matatizo ya bahari ikiwemo makoti ya kujiokoa        (life jacket ), mipira  ya gari na madumu matupu ya mafuta .
Aliwataka wavuvi kuhakikisha kuwa wanakuwa na  akiba ya chakula na maji wakati wanapokwenda baharini ili waweze kujisaidia inapotokezea tatizo la ajali  ama kupotea wakiwa kazini.
Alifahamisha kwamba kamisheni haiwezi kuzuiya maafa moja kwa moja yasitokee bali ni kupunguza athari za maafa endapo yakitokea.
Katibu wa Kamati ya Uvuvi ya kijiji cha Fumba Juma Mohamed Bakari alisema kuwa wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mengi katika shughuli zao za uvuvi jambo ambalo linavunja moyo utendaji wa kazi zao.
Alieleza kufurahiishwa na uamuzi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa kuamua kutoa taaluma kwa Kamati ya Uvuvi ya kijiji chao na ameahidi kuwa wataifikisha elimu hiyo kwa wavuvi wenzao.
Mafunzo kama hayo kwa Kamati za uvuvi yameshatolewa katika vijiji mbali mbali vinavyozungukwa na bahari ikiwemo Bwejuu, Bweleo, Kizimkazi, Matemwe, Mangapwani, Jambiani Kibigija na Chwaka .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.