Habari za Punde

Maadhimisho ya Miaka 35 ya Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar.

Na.Takdir Suweid. Maelezo Zanzibar.
Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar Saleh Juma Kinana amewaomba Wafadhili na Watu wenye uwezo kujitokeza kuisaidia Serikali katika kutatua matatizo yanayowakabili Watu wenye Ulemavu katika maeneo yao.
Ameyasema hayo huko Viwanja vya Mnazimmoja Mjini Zanzibar wakati alipokuwa akizungumza katika Sherehe za kutimiza miaka thelathini na tano ya kuzaliwa kwa Umoja wa Watu Wenye ulemavu Zanzibar (UWZ).
Amesema Serikali kupitia Idara ya Watu wenye ulemavu imeboresha miondombinu ya Barabara, Usafiri, Elimu na Mawasiliano ili kuondoshea usumbufu wanaoupata Watu hao.
Aidha Kinana ameahidi kukaa na Viongozi wenzake wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,Wilaya na Manispaa zilizomo katika Mkoa  wa Mjini Magharibi ili kuweza kutafuta njia muafaka ya kuwaondoshea Usumbufu wanaoupata Watu wenye ulemavu wakati wanapokuwa Barabarani.
Hata hivyo amewaomba Wafadhili hao kuunga Mkono miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayoanzishwa na Watu wenye Ulemavu katika maeneo yao ili iweze kuwasaidia kupata kipato na kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Afisa Mfuatiliaji wa Masuala ya Watoto wenye ulemavu kutoka U.W.Z Bi Njuma Ali Juma amewataka Wazazi na Walezi kuacha kuwafungia majumbani watoto wao wenye ulemavu na badala yake wawasherikishe katika masuala mbalimbali yanayowahusu ikiwemo kupata elimu na Michezo.
Mbali na hayo ameiomba Serikali kupitia Idara ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar kutekeleza kwa vitendo Sheria ya Watu wenye ulemavu ili kuweza kuwatia hatiani Wazazi na Walezi  watakaowatelekeza Watoto wao wenye ulemavu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.