Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Afungua Mkutano wa Kwanza wa Kamati ya Mawaziri wa SADC Jijini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa kwanza wa Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya Menejimenti ya Maafa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini Mwa Afrika (SADC) uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Madinat Al Bahr Mbweni Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuwa na mipango na mikakati ya kupambana na maafa hasa yale yanayotokea mara kwa mara.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake wakati akifungua Mkutano wa Kwanza wa Kamati ya Mawaziri wenye Dhamana ya Menejimenti ya Maafa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika katika Hoteli ya Madinat Al Bahr nje kidogo ya Jiji la Zanzibar.

Alieleza kuwa kwa kuzingatia athari za maafa zinazogharimu maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ni lazima jumuiya hiyo ikajipanga vizuri kwa kuandaa mikakati imara ya kuvitambua na kuviwahi viashiria vipya vya maafa kila vinapoanza kujitokeza.

Hivyo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Kamati hiyo ina nafasi ya kutoa maelekezo na mapendekezo juu ya nini kifanyike kwa ngazi ya kitaifa na kikanda ili kuweza kujikinga na maradhi mapya yaliyoingia ya Virusi vya Corona (Covid-19) ambayo tayari yameshaenea katika nchi mbali mbali duniani.

Aidha, alieleza kuwa changamoto ya nzige iliyojitokeza hivi karibuni katika ukanda wa Afrika Mashariki, ambao wanaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya kilimo na usalama wa chakula katika baadhi ya nchi ni suala ambalo linahitaji kuzungumzwa na kupangiwa mikakati ya pamoja.

“Wahenga wanasema tahadhari kabla ya athari, naamini kwamba haya ni miongoni mwa majukumu ya Kamati hii inayoshughulika na masuala ya maafa”,alisisitiza Rais Dk. Shein.

Katika hotuba yake hiyo Rais Dk. Shein alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya SADC kwa kuendelea kuiongoza vyema Jumuiya hiyo hatua ambayo imepelekea kupata mafanikio makubwa sambamba na kuiletea maendeleo endelevu Tanzania.

Rais Dk. Shein alisema kuwa kufanyika kwa Mkutano huo ni hatua muhimu katika kujenga matumaini mapya ya wananchi kuhusiana na maafa, kuzingatia kwamba miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la maafa pamoja na viashiria vyake katika nchi wanachama wa SADC.

Rais Dk. Shein aliongeza kuwa maafa hayo husababisha upotevu wa maisha, mali za watu na uharibifu wa miundombinu na hivyo, yanaathiri sana ajenda za maendeleo zinazopangwa kutekelezwa na nchi wanacha wa SADC.

Kwa maelezo ya Rais Dk. Shein takwimu za utekelezaji wa “Mkakati wa Sendai” zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2015 na 2018, Ukanda wa SADC umepata zaidi ya matukio 160 ya maafa ambayo yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 20,000 na yameathiri wengine milioni 22.

Kadhalika, Rais Dk. Shein aliongeza kuwa maafa hayo yalileta uharibifu mkubwa ambao gharama zake zilikadiriwa kuwa ni Dola za Kimarekani bilioni 3.7 pamoja na madhara makubwa ya kisaikolojia kwa jamii zilizoathirika.

Rais Dk. Shein alieleza kuvutiwa na ajenda kuu ya Mkutano huo iliyo kwenye kaulimbiu isemayo “ Ushiriki wa kisekta kwenye kupunguza madhara ya maafa ni njia bora ya kujenga uhilimi katika ukanda wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)”.

Aidha, alieleza kuwa ilivyokuwa maafa ni matukio yanayoleta hasara kubwa kwa taifa lolote kutokana na majanga yanayoambatana nayo, ajenda na kauli mbiu ya mkutano huo zimesadifu sana katika lengo kuu la mkutano huo.

“Mkutano huu ni muhimu, tukijua kwamba washiriki nyote mna uwezo na ushawishi mkubwa katika nchi zenu wa kuyaingiza masuala ya kukabiliana na maafa katika mipango ya maendeleo, mipango ya kisekta, miradi inayofadhiliwa na wahisani mbali mbali pamoja na mipango mengine ya kiutawala”,alisema Dk. Shein.

Dk. Shein aliieleza mikakati  mbali mbali inayopangwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukabiliana na maafa ikiwa ni pamoja na kuandaa Sera ya Kukabiliana na Maafa ya mwaka 2011, kutungwa Sheria na hatimae kuanzishwa Kamisheni,

Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali imeandaa Mkakati wa Mawasiliano Wakati wa Maafa na Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa katika ngazi ya Kitaifa na Wilaya, kuanzisha kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura kilichopo Maruhubi Unguja, kutoa elimu ya maafa,  pamoja na kuandaa mikakati maalum ya kuimarisha huduma za usafiri baharini.

Mikakati mengine ni ununuzi wa vyombo vya kisasa vya usafirishaji wa abiria, mizigo na mafuta Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali imejenga vituo vya uokozi vinavyosimamiwa na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) katika eneo la Nungwi na Kibweni Unguja na kituo cha Mkoani kwa upande wa Pemba.

Hatua nyengine zilizochukuliwa na Serikali kwa maelezo ya Rais Dk. Shein ni ununuzi wa mitambo mbali mbali na ndege zisizo na rubani (drones) ili kujua hali ya usalama wa meli na vyombo vya habarini, boti za uokozi za kisasa sambamba na kutekeleza Mradi wa Kuendeleza Huduma Mjini (ZUSP).

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliwahamasisha wajumbe wa Mkutano huo wa nchi za SADC kuwaleta walimu wao kuja kujifunza Kiswahili hapa Zanzibar kutokana na Zanzibar kuandaa mpango wa mafunzo kwa ajili ya walimu wa kwenda kusomesha Kiswahili katika mataifa yao katika Chuo chake Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Aliongeza kuwa hatua hiyo imekuja kutokana na lugha ya Kiswahili ilichaguliwa kuwa miongoni mwa lugha za mawasiliano katika mikutano ya Jumuiya ya Nchi za SADC na kusisitiza kuwa Zanzibar iko tayari kuisaidia Jumuiya ya SADC katika kuisomesha lugha hiyo.

Nae Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenista Mhagama alisema matukio mbali mbali ya maafa yaliyotokezea katika nchi za SADC na athari zake kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi wanachama.

Alieleza athari za vimbunga ambavyo vilipewa majina ya “Idai na Kenneth” vilivyotokea mwaka jana 2019 na kusababisha madhara makubwa katika nchi ya Msumbiji, Zimbwabwe, Comoro na Malawi.

Aidha, alieleza uzoefu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala mbali mbali ya maafa pamoja na mikakati iliyopangwa katika kuyakabili maafa ikiwa ni pamoja na kutungwa kwa sheria na kanuni mbali mbali.

Mapema Katibu Mtendaji wa  SADC Dk. Stergomena Lawrence Tax alitoa pongeza kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuandaa mkutano huo, mkutano ambao utaitangaza vyema Zanzibar pamoja na vivutio vyake.

Viongozi mbali mbali walishiriki katika mkutano huo akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Mawaziri wa SADC wanaosimamia masuala ya maafa nchini mwao, Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya SADC, Dk. Stergomena Lawrence Tax pamoja na viongozi wengine wa nchi za Jumuiya hiyo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.