Habari za Punde


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, wakati ikiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi kwa Ofisi yao kwa mwezi wa Julai hadi Disemba 2019 /2020, uliofanyika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein alipokea taarifa ya utekelezaji ya mpango kazi wa Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2019/2020 na kuutaka uongozi wa Ofisi hiyo kuharakisha zoezi la kuhamia Dodoma.

Alisema baada ya Serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT) kuipatia eneo la kutosha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi zake, kuna umuhimu kwa Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais kuchukuwa hatua  za kujenga Ofisi za muda kama ilivyofanyika kwa Wizara za SMT , huku Serikali ikiweka mikakati madhubuti ya kujenga ofisi za kudumu.


Nae, Waziri wa Nchi  Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed alisema katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Disemba 2019, Ofisi hiyo ilipata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake kupitia programu mbali mbali.

Aliyataja baadhi ya mafanikio hayo ni pamoja na Ofisi ya Baraza la Wawakilishi kuendelea na shughuli zake za kuratibu mikutano ya Baraza hilo pamoja na kazi za Kamati za kudumu, ambapo jumla ya miswada tisa ya sheria ilijadiliwa na kupitishwa, huku maswali 212 ya msingi pamoja na 290 ya nyongeza yakiulizwa.

Alisema Ofisi pia ilifanikiwa kutoa elimu ya kukabiliana na maafa kwa makundi mbali mbali ya kijamii,ikiwemo taasisi za serikali na zisizo za kiserikali, viongozi wa dini, kamati za uvuvi pamoja na wanafunzi katika skuli zenye Dakhalia Unguja na Pemba.

Aidha, Ofisi iliendelea na maandalizi ya Uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa 2020 kwa kutoa mafunzo kwa wahusika juu ya upigaji kura, kuimarisha ofisi za uchaguzi na ulinzi pamoja na kuanza mikutano ya maandalizi ya wahusika kwa ajili ya uchaguzi huo.

AbdiShamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.