Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Azungumza na Uongozi wa Wizara ya Kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi Zanzibar.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein, akiongoza mkutano na Uongozi wa Wizara ya Kilimo Maliasili Uvuvi na Mifugo Zanzibar, wakati wa kuwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi kwa mwezi wa Julai hadi Disemba 2019/2020, uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar. 

RAIS wa Zanzibar naMwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameutaka uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kukutana moja kwa moja na wakulima ili kufanikisha dhamira ya kuwepo matumizi ya mbegu bora za kilimo.

Dk. Shein amesema hayo Ikulu Jijini Zanzibar, wakati akipokea taarifa ya Utekelezaji wa mpango kazi ya Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2019/2020.

Alisema pamoja na matumzi ya vyombo vya Habari vya Redio na Televisheni kuwa na mchango mkubwa katika uhamasishaji wa matumizi bora ya mbegu za kilimo, ni vyema wataalamu na watendaji wa Wizara hiyo wakakutana moja kwa moja na wakulima kwa kuzingatia uzito wa jambo hilo.

Alisema uhamasishaji wa matumizi ya mbegu bora ni jambo zito na linalohitaji kupewa umuhimu na kuwa endelevu ili kuleta matokeo chanya katika kilimo, hususa nmpunga.  

Aidha, ameitaka wizara hiyo kuwa na mipango mizuri ya mafunzo kwa watendaji wake ili kuondokana na changamoto mbalimbali ,sambamba na kuwa na mipango mbadala katika kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazojitokeza.

Ameeleza ni vyema kukawa na utaratibu maalumu tekaotekelezwa kwa awamu tofauti kuambatana na ukubwa wa kiwango fedha zitakazopatikana katika bajeti.

Dk. Shein ameipongeza Wizara hiyo kwa juhudi za kuwaendeleza kielimu watendaji wake kwa lengo la kukuza uwezo wao, ambapo pia alitumia fursa hiyo kumpongeza mhitimu wa shahada ya Udaktari (PHD Pathology)kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Ali Mohamed aliehitimu hivi karibuni, hatua aliyosema itaongeza idadi ya watafiti Wizarani humo.

Rais Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kuendeleza utamaduni wa kukaa pamoja na uongozi wa Wizara za Fedha na Mipango pamoja na ile ya Biashara ili kufahamu kwa kina mwenendo wa kibiashara katika masoko mbalimbali yaliopo nchini ili hatimae kuelewa mahitaji halisi ya aina tofauti za vyakula.

Vile vile aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kukaa pamoja na watendaji wa Halmashauri za Wilaya na kuangalia namna ya kuwepo usimamizi mzuri katika uendelezaji wa masoko yaliopo kwa kuwa na mipango borakatikaupangajiwabidhaazao.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein ameutaka uongozi wa Wizara hiyo kutuma waraka Serikalini na kuelezea ukubwa wa changamoto zinazojitokeza katika ushughulikiaji wa kilimo cha mpunga kinachotegemea mvua, wakati huu ambapo Serikali imekuwa ikisaidia upatikanaji wa ruzuku na pembejeo mbalimbali kwa lengo la kuendeleza kilimo hicho.

Alisema kuwepo kwa taarifa za kuchelewa kuanza kazi za kilimo hicho, kwa madai ya wakulima kuchelewa kutuma fedha za kuchangia gharama za ukulimaji/kuburuga kwa mategemeo ya fedha hizo kulipwa na Wabunge au Wawakilishi, hakuendani na azma na dhamira ya Serikali katika uimarishaji wa kilimo cha mpunga.

Aidha, Dk. Shein aliwataka watendaji wa Wizara hiyo kuwa wabunifu, waadilifu na kuendelea kufanyakazi kwa misingi ya uzalendo, sambamba na kujenga mashirikiano ya pamoja kili kupata mafanikio zaidi.

Nae, Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulahmid Yahya Mzee aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kuhakikisha kila mara unatowa msukumo na misaada kwa wakulima, wafugaji na wavuvi nchini kote,ili waweze kupata mafanikio zaidi katika shughuli zao.

Alisema katika siku za hivi karibuni kumeanzakujitokeza mizozo kati ya wakulima na wafugaji katika baadhi ya maeneo, hivyo akasisitiza umuhimu wa kuliangalia suala hilo kwa makini ili kuepusha athari hapo baadae.

Ameupongeza uongozi wa Wizara hiyo kwa maandalizi na mpangilio bora wa mpango wa Utekelezaji uliowasilishwa, pamoja na utekelezaji mzuri wa majukumu yao.

Mapema, Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi,Mmanga Mjengo Mjawiri alisema katika kipindi hicho Wizara hiyo imefanikiwa kupata mafaniko makubwa katika utekelezaji wa mpango kazi.

Alisema mafanikio hayo yamekuja kutokanana upatikanaji wa fedha, ambapo jumla ya shilingi Bilioni 12.56 zilipatikana kwa ajili ya kuendeleza shughuli mbalimbali,ikiwemo za maendeleo.

Aliyataja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuanza kwa ujenzi wa Miundombinu ya umwagiliaji maji kwa njia yak kutumia mabomba katika mabonde saba kupitia mradi ERPP, yakiwemo ya Ole (ekari 9.2), Dobi (ekari 25), Michigini(ekari 28), Kibondemzungu (ekari 25), Koani (ekari 22), Mchangani (ekari 22) pamoja an Bandamajiekari 15.

Alisema pia ujenzi wa Soko la samaki na diko la Malindi ulianza pamoja na kufanikiwa kukamilisha ujenzi wa jengo la hifadhi za TUMCA liliopo Mkokotoni, hifadhi ya CHABAMCA iliopo Mazizini, sambamba na kukamilika kituo cha ulinzi wa bahari kiliopo kisiwani Pungume.

Alisema ununuzi wa Boti tatu za Doria zenye thamani ya Dola za Kimarekani 250,000 kutoka Afrika Kusini pamoja na ununuzi wa boti moja ya uvuvi kutoka nchini Srilanka ulikamilika na hatimae kuwasili Zanzibar.

Aidha, alisema katika kipindi hicho jumla ya Wataalii  39,951  (wandani 3,996 na nje 35,955) walitembelea Hifadhi za Jozani, Masingini, Kiwengwa Pongwe na Ngezi Vumawimbi, huku Hifadhi za Jozani na Ghubaya Chwaka ikipata tuzo ya Tourism Award kwa kupokea watalii wengi katika mwaka huo wa 2019.

Vile vile alisema Wizara ilifanikiwa kuendesha mafunzo ya uchimbaji wa mabwawa na ujengaji wa vizimba vya kufugia majongoo kwa vijiji vya Uzi, Unguja Ukuu, Fundo pamoja na Pangani, ambapo wafugaji 95 wa majongoo na samaki walinufaika.

Alieleza kuwa ugawaji wa vifaranga vya samaki 20,000 ulifanyika katika Shehia za Bumbwini makoba ,Mafufuni, Jozani, Jadida pamoja na Vifaranga vya majongoo 9,000 kwa shehiya za Uzi, Uzi Ng’ambwa na Kukuu.

Waziri Mjawiri alisema katika utekelezaji wa mpango huo pia kulijitokeza baadhi ya changamoto, ikiwemo ya ongezeko la mvua zaidi ya wastani (milimita 900) jambo lililosababisha mabonde ya mpunga kujaa maji na kuchelewesha kilimo cha mpunga.

Aidha, alisema wakulima kumi wa Sehiya ya Chaani walikataa kuchukua fidia za nyumba zao kwa ajili ya kupisha ujenzi wa miundo mbinu ya umwagiliaji maji (bwawa) kupitia mradi wa kuendeleza miundombinu ya uwagiliaji maji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.