RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleza haja kwa uongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati kuendeleza uzalendo na uadilifu katika ufanyaji wa kazi zao.
Hayo aliyasema leo, Ikulu Jijini Zanzibar
alipokutana na uongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati wakati ilipowasilisha
utekelezaji wa Mpango Kazi kwa kipindi
cha Julai hadi Disemba 2019/2020.
Rais Dk. Shein aliwanasihi viongozi hao pamoja na
wafanyakazi wote wa Wizara hiyo kuendelea kushirikiana sambamba na kuendeleza
kasi ya kuwa wazalendo kwa kupenda vyao na kuithamini nchi yao sambamba na kuwa
waadilifu katika kazi zao na maisha yao.
Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwashukuru na
kuwapongeza wafanyakazi wote wa Wizara hiyo na kueleza kuwa yeye binafsi pamoja
na Serikali wameridhika na utendaji wao wa kazi na kusisitiza haja ya kuendelea
kumsaidia Waziri wao kutokana na uongozi wake madhubuti.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya
kufuata taratibu na sheria katika
kufanya maamuzi yao ili kuepuka sintofahamu kwa wananchi na kuwataka
kutumia busara kubwa sana katika utendaji wao wa kazi hasa pale wanapoitukia jamii.
Alisisitiza umuhimu wa taarifa kwa viongozi wa
mamlaka ya juu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku huku akiwataka viongozi hao pamoja na
watendaji wa Wizara hiyo kuongeza kasi ya utendaji wa kazi zao ili kufikia
malengo waliyokusudia.
Aidha, Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa Mamlaka
ya Hifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe kuongeza kasi katika utoaji wa elimu kwa
wananchi juu ya uingiaji wa vyombo vya
moto kwa kushirikiana na taasisi
nyenginezo ili zoezi hilo liende vyema.
Rais Dk. Shein pia, ameitaka Mamlaka ya Maji
Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja inaweka huduma ya umeme unaotumia
nguvu za jua katika kisima kimoja wapo kwenye visima vinavyosimamiwa na Mamlaka
hiyo.
Katika maelezo yake katika uwasilishaji wa Mpango
Kazi wa Wizara hiyo Rais Dk. Shein aliwataka viongozi na watendaji kuendelea kupendana
na kushirikiana ili waweze kufanikisha shughuli zao ikiwa ni pamoja na
kuwatumikia vyema wananchi.
Rais Dk. Shein aliipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa
Huduma za Maji na Nishati (ZURA) kwa kuja na hoja Serikalini ya kujenga jengo jipya
la Ofisi lililopo Maisara hatua itakayozidisha ufanisi na kuinua ari kwa
wafanyakazi kufanya kazi ipasavyo.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza kazi nzuri ya uwasilishaji
iliyofanywa na Wizara hiyo huku akisisitiza haja ya kuwepo kwa usimamazi mzuri kwa
watendaji wa Wizara hiyo kutokana na sekta zake kuwagusa wananchi moja kwa
moja.
Mapema Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati
Salama Aboud Talib akisoma utangulizi wa Utekekezaji wa Wizara hiyo alisema
kuwa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati inatekeleza Malengo na Mikakati
ya Serikali ya kuhakikisha kwamba Wananchi wa Visiwa vya Zanzibar kwa ujumla
wao wanapata huduma stahiki.
Akizitaja huduma hizo alieleza kuwa ni pamoja na
maji, nishati ya uhakika iliyo salama na endelevu, makaazi bora na matumizi
mazuri ya ardhi yenye kukidhi mahitaji ya wananchi na shughuli nyengine za
kiuchumi na kijamii.
Waziri huyo alieleza kuwa Wizara yake kupitia
Mamlaka ya Maji (ZAWA) imeendelea kusimamia miradi na program za uhuishaji na
upanuzi wa shughuli za maji Mijini na usambazaji wa maji Vijijini.
Alisema kuwa katika utekelezaji wa program hiyo,
Mamlaka ya Maji kupitia mradi wa maji wa Mkoa wa Mjini Magharibi (ADF12)
imekamilisha kazi ya utekelezaji wa mradi kwa uchimbaji wa visima vipya sita
vyenye uwezo wa wastani wa lita 150,000 kwa saa kwa kila kisima.
Utekelezaji mwengine ni ukarabati wa visima vikongwe
23, ujenzi wa matangi 2 yenye ujazo wa lita milioni mbili Saateni na milioni
moja la Mnara wa Mbao pamoja na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita
75.7.
Aliongeza kuwa Wizara hiyo kupitia Shirika la
Umeme katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 imefanikiwa kutekeleza azma
ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme katika maeneo yao
kwa kufikisha umeme katika vijiji 26 (Unguja 16 na Pemba 10) ambapo jumla ya
TZS Bilioni 1.96 zimetumika.
Alisema kuwa Wizara kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa
Huduma za Maji na Nishati (ZURA) inaendelea kutekeleza shughuli za ujenzi wa
jengo la Ofisi hapo Maisara.
Alieleza kuwa ujenzi huo umefikia asilimia 96 na
jengo litakamilika na kukabidhiwa mwezi wa Machi 2020. Aidha, matayarisho ya
ujenzi wa Bandari mpya ya mafuta Mangapwani yanaendelea na hatua iliyofikiwa ni
kukamilika ulipaji wa fidia kwa vipando na mali za wananchi wa eneo hilo.
Sambamba na hayo, Wizara kupitia Mamlaka ya
Hifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe imekamilisha utayarishaji wa Mpango wa
Uingiaji wa Vyombo vya Moto kwa kushirikiana na taasisi nyenginezo ikiwemo
Baraza la Manispaa, Usalama Barabarani,
Shirika la Bandari pamoja na wadau wengine.
Pia, alieleza kuwa Serikali inaendelea na azma
yake ya kuhakikisha Zanzibar inazalisha umeme kwa kutumia nishati mbadala ya
jua baada ya Serikali kuridhia uzalishaji wa nishati hiyo kwa kutumia mfumo wa
Mzalishaji wa Kujitegemea ambapo bado Serikali inahusika kwa njia moja au
nyengine katika aina ya uwezekezaji huo.
Kwa maelezzo yake hadi hivi sasa jumla ya
wawekezaji wasiopungua 47 wameonesha nia ya kuekeza katika miradi ya Nishati ya
jua ambapo miongoni mwa wawekezaji hao ni Mirambo ya Tanzania na Green Energy
ya Kenya.
Nao viongozi wa Wizara hiyo walimpongeza Rais Dk.
Shein kwa maelekezo yake anayoyatoa kwao hatua ambayo inawarahisishia kutenda
kazi zao kwa ufanisi huku wakimuhakikishia kuwa wanaendelea kutekeleza vyema
kazi zao ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi wote wa Zanzibar.
No comments:
Post a Comment