Habari za Punde

Uongozi wa Wizara ya Biashara na Viwanda Yawasilisha Taarifa ya Mpango Kazi wa Wizara Yao.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akiongoza mkutano wa Uongozi wa Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi kwa mwezi wa Julai hadi Disemba 2019 /2020, uliofanyika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar, uliofanyika 17-2-2020.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali ya Mapinduzi awamu ya saba itakamilisha ujenzi wa kiwanda cha Mwani kisiwani Pemba kama ilivyowaahdi wananchi wake.

Alieleza kuwa pamoja na bei ya zao la karafuu kupanda na kushuka katiuka soko la Dunia, Serikali itaendelea kusimamia ahadi yake na kuwalipa wakulima kiwango kile kile cha bei (asilimai 80 ya bei ya soko la Dunia) .  

Alisema Wizara ya Viwanda na Biashara inachangia ipasavyo maendeleo ya utalii hapa nchini.

Aidha,  ameutaka uongozi wa Wizara hiyo kupitia vitengo vyake vya elimu kujikita katika suala la utoaji wa elimu  ili kuwaelimisha wafanyabiashara juu ya sheria mbali mbali zilizopo badala ya kusubiri wakosee na kuwachukulia hatua.
    
Dk. Shein ametoa pongezi kwa Uongozi na watendaji wa Wizara hii kwa kuandaa vyema taarifa ya mpango kazi na utekelezaji mzuri wa majukumu yao na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika  uchumi na   maendeleo ya Taifa.   

Nae, Waziri wa Biashara na Viwanda Amina Salum Ali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi kwa Wizara hiyo kwa kipindi cha Julai – Disemba  2019, alisema katika kipindi hicho Wizara ilikadiria kununua jumla ya tani 3,500 za Karafuu , lakini hadi kufikia Disemba 2019 ilifanikiwa kununua jumla ya tani 1,638.5 zenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 20.3, na kuainisha kuwa kiwango kikubwa cha karafuu hizo ziliuzwa katika nchi za India na Singapore.

Alisema shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) limeanzisha maandalizi ya uanzishaji wa Kiwanda cha kuchakata Mwani katika eneo la Viwanda Chamanangwe, huku taaluma ya kilimo  hicho ikitolewa kwa baadhi ya wakulima wa maeneo ya Makangale, Tumbe na Chokocho kwa upande wa Pemba, wakati kwa upande wa kisiwa cha Unguja ni Bweleo, Pwani mchangani na Muungoni.

Aidha, alisema Wizara imefanya utafiti mdogo wa kuangalia soko la Uyoga hapa nchini, ambapo matokeo ya utafiti huo yakionyesha zaidi ya asilimia 90 (hoteli zipatazo 65) zinatumia Uyoga kama chakula cha wageni wao.

Alisema kwa asilimia 70 Hoteli hizo hutumia Uyoga huo kutoka nje ya nchi (canned), wakati baadhi ya Hoteli huagiza kutoka Mikoa ya Iringa na Arusha.
                           
Vile vile alisema Wizara imefanikiwa kuwalipa fidia  wananchi 106 wanaotoka vijiji vya Kiuyu na Mchangamdogo waliokuwa wakimiliki mashamba madogo na makubwa katika eneo la Viwanda Chamanangwe, wakati wale waliobaki wakitakiwa kusubiri uhakiki wa majina yao.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.