Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein,
akizungumza na mgeni wake Balozi wa
Angola Nchini Tanzania .Mhe.Sandro Agostinho De Oliveira , alipofika Ikulu
Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha, leo Ikulu. 6-2-2020.(Picha na
Ikulu)
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameupongeza uwamuzi
wa busara na wenye tija wa Angola wa kutaka kushirikiana na Zanzibar kwenye
sekta ya utalii hatua ambayo itaimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo, Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa Angola katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Sandro Agostinho de Oliveira aliyefika
Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais.
Rais Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kuusifu na kuupongeza uwamuzi huo wa Angola wa kutaka
kushirikiana na Zanzibar katika sekta ya utalii na kusisitiza kuwa hatua hiyo
ni chachu ya maendeleo kwa pande mbili hizo.
Katika mazungumzo
hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi Oliveira kuwa Zanzibar na Angola zina mambo mengi ya kushirikiana kwa pamoja
ambayo yanaweza kuleta mafanikio makubwa kwa pande zote mbili yakiwemo
mashirikiano katika sekta ya utalii.
Dk. Shein alieleza
kuwa uhusiano na ushirikiano wa
kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Angola ni njia moja wapo kubwa
itakayopelekea kuimarika zaidi kwa sekta ya utalii ambapo Zanzibar imepiga hatua kubwa..
Aidha, Dk. Shein
alimueleza Balozi Oliveira kuwa Zanzibar na Angola zote kwa pamoja zina mambo mengi
ya kujifunza kwa kila upande ikiwa ni pamoja na namna ya kuendeleza na
kuimarisha sekta ya utalii.
Alisema kuwa kwa
upande wa Zanzibar sekta ya utalii ni
nguzo kubwa ya uchumi ambayo imekuwa ikichangia kiasi cha asilimia 20 ya Pato
la Taifa na asilimia 80 ya fedha za kigeni.
Rais Dk. Shein
alisisitiza kuwa mashirikiano katika sekta ya utalii yatazidisha na kuimarisha
uhusiano wa kihistoria ulioanzishwa na waasisi wa pande mbili hizo kupitia
vyama vyao vya (CCM) na MPLA.
Dk. Shein aliongeza
kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina mashirikiano makubwa na nchi za Kusini
mwa Bara la Afrika kwani iliweza kushirikiana nazo bega kwa bega katika
kupigania uhuru ikiwemo Angola, Msumbuji na Afrika Kusini kupitia vyama vyao
vya ukombozi vya siasa.
Aliongeza kuwa, kutokana
na Angola kupata mafanikio makubwa katika sekta ya mafuta na gesi asilia ipo
haja kwa Zanzibar na nchi hiyo kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha Zanzibar
inapanua wigo kwa nchi hiyo ambayo ni ya pili kwa uzalishaji wa mafuta na gesi
asilia barani Afrika ikitanguliwa na Nigeria.
Akieleza kuhusu
mashirikiano katika sekta ya elimu, Rais Dk. Shein alieleza kuwa ipo haja kwa pande
mbili hizo kushirikiana katika sekta ya elimu hasa kupitia vyuo vya nchi hizo
kikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) katika Kada ya lugha hasa lugha
Kireno.
Aidha, Dk. Shein aliongeza
kuwa mashirikiano yanaweza kuimarishwa katika sekta hiyo ya elimu, ikiwa ni
pamoja na kubadilishana utaalamu na wataalamu hasa katika lugha ya Kireno
ambayo itasaidia sana Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii.
Rais Dk. Shein pia,
alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Angola Joao Lourenco kwa kazi nzuri
anayofanya ya kuiongoza nchi hiyo kwa mafanikio makubwa ambapo hivi sasa uchumi
wake unakuwa kwa asilimia 8.4 na kueleza kuwa hayo ni miongoni mwa mambo
yaliopelekea ushindi wa kishindo wa kiongozi huyo pamoja na chama chake cha
(The People's
Movement for the Liberation of Angola) MPLA.
Nae Balozi wa Angola
nchini Tanzania Sandro Agostinho de Oliveira alimueleza Dk. Shein kuwa Angola iko
tayari kushirikiana na Zanzibar katika sekta ya utalii hasa ikizingatiwa kwamba Zanzibar imeanza
kupata mafanikio na kutajika duniani kote katika sekta hiyo.
Balozi Oliveira alimueleza
Rais Dk. Shein kuwa Angola ina mambo mengi ya kujifunza kutoka Zanzibar katika
sekta ya utalii, hivyo iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha
sekta hiyo muhimu ya kukuza uchumi.
Katika maelezo yake
Balozi Oliveira alimueleza Dk. Shein, kuwa Angola pia, iko tayari kutoa nafasi
za masomo kwa Zanzibar katika Chuo chake kinachotoa mafunzo ya mafuta na gesi
asilia ikiwa ni njia moja wapo ya kuendeleza ushirikiano wa kihistoria uliopo.
Alieleza kuwa kutokana
na mafanikio makubwa yalioipata nchi yake katika sekta ya mafuta na gesi
asilia, Angola iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika sekta hiyo.
Sambamba na hayo, Balozi
huyo alimueleza Rais Dk. Shein juhudi zinazochukuliwa na nchi yake katika
kupambana na rushwa huku akisisitiza kuwa nchi yake itaharakisha mchakato wa mashirikiano na Zanzibar katika kuendeleza
sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya utalii, elimu, mafuta na gesi
asilia pamoja na kuendeleza utamaduni.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment