Habari za Punde

WAZIRI WA NISHATI SITAKI KUSIKIA MGAO WA UMEME,AAGIZA ABUBAKARI KUCHULIWA HATUA KALI

Waziri wa nishati Dkt Medard Kalemani akizungumza na waandishi wa habari mkoa wa Iringa katika bwawa la Mtera akitoa katazo la kuwepo kwa mgao wa umeme hapa nchini
 Waziri wa nishati Dkt Medard Kalemani akiwa mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela alipofanya ziara katika bwawa la Mtera

NA FREDY MGUNDA,IRINGA.
Waziri wa nishati Dkt Medard Kalemani amepiga marufuku kwa uongozi wa TANESCO kutoa nishati ya umeme kwa mgao wakati hakuna tatizo lolote la uzalishaji katika vituo vyote vitatu.

Akizungumza wakati wa ziara katika kituo cha uzalisha ji wa umeme Mtera mkoani iringa,Dkt Medard Kalemani alisema kuwa “haiwezekani mtu mmoja anaamua kutoa maagizo ya kuwepo mgao wakati hakuna tatizo lolote lile”.

Alitoa agizo hilo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Felchesmi Mramba Kuhakikisha anamchukulia hatua mfanyakazi aitwae Abubakari kwa kosa la kuagiza mkoa wa Mwanza kuwepo kwa mgao wa umeme bila sababu za msingi.

"Usipomchukulia hatua huyu mfanyakazi anaeitwa Abubakari basi Mimi nitajua nani wa kumchukulia hatua kwa kuwa tatizo hilo kwa Abubakari limekuwa likijirudia mara kwa mara" alisema 

Alisema serikali imejenga nyumba za wafanyazi pale ubongo kwa ajili ya uangaliangalizi wa mwenendo wa umeme nchi nzima lakini bado wafanyakazi wanakaidi kukaa hapo jambo linalopelekea ufanisi wa kazi kuwa hafifu.

Aliwaagiza Mameneja wa TANESCO mikoa yote hapa nchini kuhakikisha wanawasimamia vilivyo wafanyakazi wengine ili watimize wajibu wao katika kutimiza ahadi ya kutoa huduma ya nishati kwa wananchi.

Aidha Dkt. Medard Kalemani alitoa tahadhari kwa wananchi waliokaribu na mto Ruaha mkuu kuchukua tahadhari kwa kuwa wameamua kufungulia maji kutoka katika bwawa la Mtera na Kidatu kutokana na kujaa hadi kupitiliza kiwango kinacho hitajika. 

Alisema Wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari na kuongeza kuwa maji hayatakuwa yanasambaa bali yatapita kwenye mkondo wake wa asili ambako wananchi wanafanya shughuli zao za kijamii.

"TANESCO tumeona ni muhimu kutoa tahadhari kwa Wananchi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, kwa kawaida Bwawa la Mtera kulijaza huchukua miezi 3 hadi 4 kwa mvua za masika, lakini kwa kipindi hiki mvua za vuli zimekuwa nyingi ndani ya mwezi mmoja hivyo kina kimeongezeka", alisema 

Alisema tahadhari inatolewa kwa Wananchi kusitisha shughuli zao za kijamii kama uvuvi, kulisha mifugo, kilimo na nyingine kwenye mkondo wa maji au sehemu zenye vidimbwi ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

Aliongeza kuwa, kawaida kina cha maji kujaa ni mita 698.50 juu ya usawa bahari na kuongeza hivi sasa kina cha maji kimefikia 698.03 juu ya usawa wa bahari.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela alisema kuwa wamekuwa wakitoa elimu mara kwa mara kwa wananchi kwa lengo la kuwaokoa wananchi na madhara ambayo wanaweza kuyapata kipindiki cha mafuriko hasa wale wanaofanya shughuli katika bwawa la Mtera na kandokando ya mto Ruaha.

Kasesela alisema kuwa historia inaonyesha kila baada ya miaka kumi mvua hunyesha kwa wingi kama ilivyo hivi sasa na kupelekea bwawa hilo la Mtera kujaza maji kupita kiasi hivyo lazima kuwepo kwa mkakati maalumu wa kila mwaka kutoa elimu kwa wananchi.

“Hii ni historia ambayo nimeikuta na nimeona ikifanya kazi kama hivi ambavyo tunaona bwawa limejaa maji hadi kupita vipimo vinavyotakiwa kwenye bwawa hili” alisema Kasesela
Kasesela alimuomba waziri kusaidia kuharakisha ujenzi wa daraja jipya ambalo michoro yote imekamilika ila fedha bado hazijapatika kwa lengo la kuliokoa daraja la sasa kutokana na magari yanayopita hapo yanauzito mkubwa sana

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.