Habari za Punde


HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR ALIYOITOA
WAKATI AKIFUNGA MKUTANO WA 18 WA BARAZA LA TISA LA WAWAKILISHI TAREHE 17 APRIL, 2020
 Mheshimiwa Spika,
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu mwingi wa Rehma kwa kutujaalia uhai, akatupa na afya njema akatuwezesha kufanikisha Mkutano huu wa Kumi na nane wa Baraza la Tisa ulioanza tarehe 01 April, 2020 hadi leo tarehe 17 April, 2020 tunapouakhirisha, baada ya shughuli zote zilizopangwa kukamilika. 

Mheshimiwa Spika,
Katika Mkutano huu, Baraza lako Tukufu limepokea na limejadili Miswada 8 pamoja na Ripoti zipatazo 16 kutoka Wizara zetu.  Miswada iliyowasilishwa ni kama ifuatavyo:-

1.   Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya mambo ya Rais Namba 5 ya mwaka 1993 na kutunga Sheria ya mambo ya kuweka masharti bora zaidi kuhusiana na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

2.   Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Sheria ya masuala ya Diaspora na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

3.   Mswada wa Sheria ya kufuta na kuandikwa upya Sheria ya vileo na kuweka Masharti ya kuzuia, kudhibiti na kusimamia Uagizaji, kuhifadhi kwenye maghala, uuzaji, usambazaji na unywaji, vileo na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

4.   Mswada wa Sheria wa vipimo Nam. 4 ya mwaka 1983 na kuanzisha Sheria ya Wakala wa viwango na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

5.   Mswada wa Sheria ya kuanzisha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Zanzibar na mambo Mengine yanayohusiana na hayo.

6.   Mswada wa Sheria ya kufuta Sheria ya Taasisi ya utafiti wa Kilimo Nam. 8 ya 2012 na kutunga Sheria ya Taasisi ya utafiti wa Kilimo Zanzibar na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

7.   Mswada wa Sheria wa Usajili na Usimamizi wa Wataalamu wa maabara za Tiba na mambo mengine yanayohusiana na hayo, na

8.   Mswada wa Sheria ya kuanzisha Taasisi ya utafiti wa Afya Zanzibar na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Mheshimiwa Spika,
Baraza lako Tukufu lilipata muda wa kutosha kuijadili Miswada yote hii minanekwa kina na kuipitisha.  Nawapongeza Wajumbe wote waliopata nafasi ya kutoa michango yao ambayo bila shaka ilihitajika ili kuiimarisha Miswada hiyo.  Naamini michango iliyotolewa na Wajumbe wa Baraza lako Tukufu imejitosheleza na hakuna haja kwa upande wangu kuitolea maelezo mengine.

Mheshimiwa Spika,
Baraza lako Tukufu pia limepokea, limejadili na limepitisha Ripoti za Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, juu ya Utekelezaji wa maagizo ya Kamati za Kudumu za Baraza kwa mwaka 2019/2020.  Sina budi kuzipongeza Kamati zote kwa utekelezaji makini wa majukumu yao.  Napenda kuwashukuru Mawaziri wote kwa uwasilishaji wa taarifa hizo; na pia Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kwa michango yao ambayo itaendelea kuisadia Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake.

Mheshimiwa Spika,
Kama tunavyojua Dunia hivi sasa imekumbwa na janga kubwa la maradhi ya Corona yanayosababishwa na kirusi kiitwacho COVID-19. Maradhi haya tayari yamesababisha na yanaendelea kusababisha vifo vya watu wengi duniani kote.  Kwa hivi sasa Bara la Uropa, Asia na Marekani yameshapoteza watu wengi.  Duniani kote zaidi ya watu milioni moja tayari wameshaambukizwa na Corona na zaidi ya watu 100,000 wameshapoteza maisha yao.  Kwa mujibu wa Gazeti la East Afrika la tarehe 5 mwezi huu, wanasayansi kutoka London School of Hygiene and Tropical Medicine wanakadiria kuwa kwa kila nchi ya Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania watu wapatao 10,000 watakuwa wameambukizwa na ugonjwa wa Corona ifikapo mwezi wa Mei.  Idadi hii itashuka endapo nchi zenyewe zitakuwa zimechukua tahadhari kubwa ikiwemo watu kutokusanyika na kutokuchanganyika ovyo na kufuata masharti ya wataalamu wa Afya.  Ugonjwa huu hadi sasa hauna dawa wala chanjo.  Aidha, uwezekano wa kupata chanjo ya kujikinga na maradhi haya hivi karibuni haupo.  Wataalamu wa afya wanasema kuwa inaweza kuchukuwa zaidi ya miezi 6 kupatikana kwa chanjo ya Corona.

Mheshimiwa Spika,
Maradhi ya Corona hayana dawa lakini ikiwa tutafuata miongozo na maelekezo ya Viongozi na Wataalamu wa Afya ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), tunaweza kabisa kuutokomeza ugonjwa huu nje ya visiwa vyetu na nje ya Tanzania kwa jumla.  Kwa mujibu wa miongozo ya viongozi wetu na wataalamu wa Afya, ugonjwa wa Corona dawa yake kubwa ni kujikinga nao usikupate kwa kufuata mambo yafuatayo:-

-        Kuosha mikono kwa sabuni na maji ya kutiririka angalau sekunde 20;
-        Kuacha tabia ya kujigusa macho, pua na mdomo kwa mikono ambayo haijaoshwa;
-        Kuvaa barkoa na kuweka Sanitizer;
-        Kuepuka mikusanyiko;
-        Kuepuka kuchanganyika na mgonjwa; kujitenga na watu wengine hasa pale Corona ikiwa imeshaingia nchini kama hivi sasa hapa kwetu.  Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na wataalamu wetu wa afya maradhi haya siyo tena yanatoka nje ila tunaambukizana wenyewe kwa wenyewe.
-        Kaa nyumbani (Stay at Home) kama huna sababu maalum ya kutoka nje.

Mheshimiwa Spika,
Napenda kuwajulisha wananchi wenzangu kuwa hivi sasa tuko katika vita dhidi ya Corona; tunapambana na adui ambaye haonekani, hachagui rangi, umri, jinsia, Taifa wala hadhi ya mtu.  Adui huyu anachojua ni kushambulia tu mtu yeyote bila ya huruma. Ukipambana na adui wa aina hii ambaye haonekani; anayeshambulia kila mtu, unatakiwa kuwa makini na kuchukua tahadhari kubwa vyenginevyo utajishtukia umeshakuwa mateka.  Nchi ikishawekwa mateka na adui huyu shuhudia vifo vya watu wengi.  Zipo nchi hivi sasa zinapoteza watu wapatao 800 hadi 1,000 kwa muda wa masaa 24.  Nchi hizi zina vifaa vya kisasa, wataalamu wa tiba waliobobea lakini zimezidiwa.  Naomba tutafakari hali hii ili tupate kuelewa ukubwa wa adui tunayepambana nae.

Mheshimiwa Spika,
Hapa kwetu Serikali zetu zote mbili zimechukuwa hatua za tahadhari mara tu ugonjwa huu ulipoanza kuripotiwa nchini China mwezi wa Disemba, 2019 ili kuwakinga wananchi wake wasiambukizwe.  Viongozi wetu Wakuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, wamechukuwa hatua mbali mbali za kupambana na ugonjwa wa Corona ikiwemo kuzuia ndege kutua nchini kutoka nchi ambazo zimekumbwa na ugonjwa huu; kuanzisha utaratibu wa kuweka watu kwenye karantini; kufunga Maskuli, Madrasa na Vyuo mbali mbali, kuzuwia mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.  Vile vile, Serikali yetu ilizuia kufanyika kwa Ijitimai ya Kimataifa, Mkutano wa Kimataifa wa Wawekezaji na Kongamano kubwa la Kilimo.  Hatua zote hizi zilikuwa na lengo moja tu nalo ni kuwakinga wananchi wetu na maambukizi ya maradhi ya Corona.

Aidha, Rais wetu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ametoa maagizo kujengwa maabara ya kisasa ndani ya miezi mitatu katika eneo la Binguni ili kuchunguza na kutafiti maradhi mbali mbali ikiwemo Corona.

Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza kwa dhati Viongozi wetu hawa kwa juhudi zao za dhati walizozichukua za kujikinga nchi yetu na janga la mripuko wa maradhi ya Corona.  Hatuna budi kuthamini juhudi zao kwa kufuata malekezo yao na yale yanayotolewa mara kwa mara na wataalamu wetu wa afya.

Mheshimiwa Spika,
Tahadhari mbali mbali za kujikinga na ugonjwa wa Corona zilizotangazwa kwa wananchi na Serikali yetu zitafanikiwa tu ikiwa sote kwa umoja wetu bila kujali cheo, kabila wala wasifu wa mtu tutazizingatia na kuzifuata bila ya muhali.  Tahadhari hizi ni kwa wananchi wote kutoka ngazi zote na wala hatutoruhusu majadiliano.  Kwa Lugha nyengine, ‘hakuna mbora ambaye atakuwa juu ya tahadhari hii tulizojiwekea za kujikinga na maradhi haya thakili’.  Mtu yeyote atakayethubutu kuzivunja tahadhari za kujikinga na maradi ya Corona atachukuliwa hatua kali bila ya kumuangalia usoni.  Napenda kuwashukuru Mawaziri wetu wa Afya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Ummy Mwalimu na Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Hamadi Rashid kwa kutupa taarifa za kila siku za hali ya ugonjwa inavyoendelea.

Mheshimiwa Spika,
Nyote ni mashahidi kuwa mara tu baada ya kutoka safarini nchini Cuba nilikuwa kwenye karantini na ujumbe wangu wote kwa mujibu wa sheria zetu tulizoziweka.  Nimetumikia kipindi cha zaidi ya siku 14 kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu wa afya.  Nikaongeza na siku nyengine saba ili kujiridhisha kuwa tuko salama.  Nawashukuru Wataalamu wa Afya waliokuwa wakija kututembelea kila mara ili kujua tunavyoendelea.  Hakuna anayependa kukaa karantini lakini ni sheria na hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria.  Kama nilivyowahi kusema kukaa karantini si adhabu bali ni kitendo cha kiungwana cha kujihakikishia usalama wako na waliokuzunguka, hasa kwa vile maradhi haya ya Corona tayari yameshaingia nchini mwetu.

Nachukuwa nafasi hii kuwataka Viongozi wa ngazi zote tushirikiane na wananchi katika kuzisimamia taratibu tulizoziweka za kupambana na maradhi ya Corona.  Afya yetu ndio rasilimali yetu, Kinga ni Bora kuliko Tiba. Tuache ukaidi na dharau wa kufuata maelekezo ya Viongozi wetu na wataalamu wetu wa afya.  Sisi Wazanzibar tunasemwa sana kwa ukaidi na dharau, lakini Wahenga wamesema mkaidi hafaidi mpaka siku ya Iddi, si hivyo tutadhurika sisi wenyewe na familia zetu na jamii inayotuzunguka kwa ukaidi na dharau zetu.  Mheshimiwa Rais wetu Dk. Ali Mohamed Shein ameteua viongozi mbali mbali kuanzia ngazi ya Shehia mpaka Serikali Kuu kwa nia ya kumsaidia kazi, hivyo ni wajibu wetu kila mmoja wetu katika eneo lake atimize wajibu wake kulisimamia suala la Corona.

Mheshimiwa Spika,
Katika hotuba yangu ya kuakhirisha Mkutano wa Kumi na Tano wa Baraza la Tisa nilieleza maamuzi ya Serikali zetu mbili kuendeleza Mradi wa Kunusuru Kaya Maskini TASAF ambao bila shaka ni mkombozi wa wanyonge.

Kwa furaha kubwa, nachukua nafasi hii kuwaeleza Waheshimiwa Wajumbe na wananchi wote kwamba kama mlivyoona na kusikia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii tarehe 17 Februari, 2020 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amezindua rasmi Awamu ya Pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF III-II) unaotegemewa kutekelezwa kwa miaka minne.

Kufuatia uzinduzi huo Serikali zetu zote mbili zimeanza hatua mbali mbali za matayarisho ya kitaalamu ya utekelezaji wa awamu hiyo.  Utekelezaji huo unategemea kuvifikia vijiji vyote kwa Tanzania Bara na Shehia zote kwa Tanzania Zanzibar.  Aidha, kwa upande wa Zanzibar jumla ya Shilingi Bilioni 21.5 zitatumika kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika,
Nachukua nafasi hii kwa mara nyengine tena kuwataka viongozi na wananchi kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa awamu hii ya pili.  Hatuna budi kushiriki kikamilifu katika hatua zote za mradi kuanzia ukusanyaji wa taarifa za walengwa katika ngazi za Shehia ili kuweza kupata takwimu sahihi ambazo ndio kiini cha upatikanaji wa mlengwa aliyetimiza vigezo na masharti ya mpango.

Nawaomba watendaji na wahusika wote kufanya kazi kwa uadilifu, juhudi na uaminifu ili kuendeleza sifa nzuri ambayo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla imejipatia katika utekelezaji wa Mradi huu wa TASAF iliyopelekea watu kutoka Mataifa mbali mbali kuja kujifunza namna tunavyotekeleza Miradi ya TASAF Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,
Tupo katika kipindi cha Masika na tayari mvua zimeshaanza nchini kote. Nawakumbusha wananchi umuhimu wa kuzitumia vizuri mvua hizi kwa shughuli za kimaendeleo zikiwemo kilimo cha mazao ya chakula na miti ya kudumu.  Ni wakati mzuri wa kupanda miche ya mikarafuu na minazi ambayo inatolewa bure na Serikali.  Aidha, nawataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kujiepusha na maafa kwa kuhama katika maeneo hatarishi, kufuatilia mienendo ya watoto wetu hasa kwa vile shule zimefungwa kutokana na tatizo la Corona, kufuatana maelekezo ya wataalamu wa Mazingira, wataalamu wa Afya na kuendelea kufuatilia taarifa za kitaalamu na elimu zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa kanda ya Zanzibar.


Mheshimiwa Spika,
Napenda kuwaasa wananchi wote kuchukua tahadhari za kudumisha usafi ili kujikinga na maradhi ya mripuko kama kipindupindu na maradhi ya matumbo.  Mbali na juhudi za Serikali za kuondosha maradhi hayo, wananchi kwa upande wao wana nafasi ya kujilinda kwa kudumisha usafi hasa kipindi hiki cha mvua za masika.

Mheshimiwa Spika,
Juhudi za Serikali za uondoshaji wa maji ya mvua katika mitaa yetu zinaonekana na tayari misingi ya Chumbuni, Jang’ombe, Mwanakwerekwe – Sebleni - Mikunguni hadi Mpiga Duri imekamilika.  Ujenzi wa misingi hii umeigharimu Serikali yetu fedha nyingi.  Natoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali katika kuitunza ili iendelee kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa kwa muda mrefu.  Serikali haitamvumilia mwananchi ye yote atakaye unganisha misingi hii na bomba lake la maji machafu kutoka nyumbani kwake.  Hili ni kosa na lazima lichukuliwe hatua za kisheria.  Tuache tabia ya kuijaza taka misingi hii ili isifanye kazi iliyokusudiwa ya kupitisha maji.



Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya Corona hatutakiwi kukaa pamoja kwa kipindi kirefu.  Kwa hivyo, napenda kumalizia hotuba yangu kwa kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu wako na Wenyeviti wote wa Baraza kwa kuviendesha vyema vikao vyetu kwa hekima na busara.  Nawashukuru pia Waheshimiwa Wawakilishi kwa kutumia nafasi yao ya Kidemokrasia ya kuisimamia, kuishauri na kuihoji Serikali, jambo ambalo limeonesha nia thabiti mliyokuwa nayo ya kuitaka Serikali kuwajibika ipasavyo kwa wananchi wake.  Kadhalika, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri kwa kujibu maswali walioulizwa kwa ufasaha.  Namshukuru pia Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ufafanuzi wake alioutoa katika mambo mbali mbali yaliyohitaji ufafanuzi wa kisheria, na hasa wakati wa kujadili na kupitisha Miswaada mbali mbali.  Pia namshukuru Katibu wa Baraza na Watendaji wenzake wakiwemo wakalimali wa lugha ya alama, waandishi wa habari kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mwisho, nawaomba Wawakilishi wenzangu waendelee kuwaelimisha wananchi wetu kuhusu suala hili la Ugonjwa wa Corona, sisi tunatakiwa tuwe mfano wa kuigwa ukiachia madaktari wetu, sisi ndio tuwe askari wa mstari wa mbele katika kupambana na vita vya maradhi ya Corona.

Kabla sijamaliza hotuba yangu, napenda kuwapongeza watumishi wote wa Wizara ya Afya wa Unguja, Pemba na Tanzania Bara ambao wanajitolea kupambana kwa hali na mali ili kuokoa maisha ya wananchi wote.  Watumishi wa Afya ndio askari wetu, lazima tuwasaidie vita hivi kwa kufuata maelekezo yao ya kujikinga na maradhi haya hatari ya Corona.  Tukifuata maelekezo yao idadi ya wagonjwa nchini itakuwa ndogo.  Serikali kwa upande wake itahakikisha inawapatia vifaa vinavyotakiwa vya kujikinga na maradhi ya Corona ili wafanye kazi zao bila ya kuambukizwa.  Nawashukuru wote kwa uzalendo wao wanaouonyesha, Mwenyezi Mungu atawalipa kwa kujitolea muhanga kuokoa maisha ya Watanzania.

Aidha, napenda kuwashukuru kwa dhati wale wananchi wote  waliojitokeza kutoa misaada yao ya vifaa mbali mbali vya kinga kuisaidia Serikali yetu katika mapambano haya dhidi ya ugonjwa huu hatari.  Mwenyezi Mungu atawajazia maradufu pale walipotoa.

Mwisho kabisa, nawashukuru wananchi wote wa Zanzibar kwa kuitikia wito wa Serikali wa kupambana na maradhi ya Corona kwa njia ya kufuata tahadhari zilizowekwa.  Nawaomba tuzidi kushirikiana ili tushinde vita hivi.  Ni wakati huu ambapo sisi Wazanzibari na Watanzania kwa jumla tunahitaji kuwa wamoja na kushikamana kuliko wakati wote ule.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya maelezo hayo sasa, kwa heshima na taadhima naomba kutoa hoja kwamba Baraza lako Tukufu liahirishwe hadi siku ya Jumatano tarehe 6 Mei, 2020 saa 3.00 barabara za asubuhi panapo majaaliwa.
Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa Hoja.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.