Na Himid Choko, BLW
KAMATI
ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi imeishauri Serikali kutengeneza mpango
madhubuti wa kukabiliana na athari za
kiuchumi zinazosababishwa na kuenea kwa virusi vya CORONA.
Akichangia Ripoti
ya Utekelezaji wa Maagizo ya Kamati ya
Bajeti ya Baraza la Wawakilishi ya Mwaka 2019/2020 kwa Wizara ya Fedha na Mipango, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt.
Mohammed Said Dimwa amesema janga
la maradhi ya COVID 19 lililoikumba Dunia hivi sasa ikiwemo Zanzibar linaleta tishio kubwa la kiuchumi.
Amesema uchumi wa dunia upo katika hatari ya
kuporomoka kutokana na Serikali za nchi mbali mbali kupiga marufuku
mikusanyiko, kuzuia wageni kuingia, na hata wananchi wake kutoka majumbani mwao ili
kujaribu kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya virusi vya CORONA.
Hivyo amesema Kamati yake inashauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ishirikiane na SMT kupitia Kamati ya Kitaifa
ya Mawaziri ili kuweka mikakati ya kitaifa ya pamoja ya kukabilina na janga
hili la ugonjwa katika kuenea kwa maambukizi na pia kunusuru uchumi wa taifa.
Aidha Kamati hiyo ya Bajeti wameiomba SMZ ishirikiane na SMT kutafuta
usaidizi wa kiuchumi kwa taasisi za kimataifa kama vile Benki ya Dunia (WB) na
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwani taasisi hizi huweka bajeti kwa ajili ya kukabiliana na
changamoto za kiuchumi kwa nchi wanachama.
Kamati hiyo pia, imeishauri Serikali kuomba
kupewa tahfifu ya madeni yake (debt relief) kwa kuondolewa au kupunguzwa riba
katika kipindi hichi ambacho nchi yetu inapambana na kuenea kwa maambukizi ya
virusi hivi hatari.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mheshimiwa
Mohammed Raza Dharamsy ameishauri Wizara
ya Fedha na Mipango kuhakikisha bidhaa
na mahitaji muhimu ya mwanadamu hasa chakula vinapatikana kwa wingi kipindi
hiki pamoja na kudhibiti njia zisizorasmi za kuingiza bidhaa na mfumko wa bei.
Akitoa ufafanuzi wa Hoja za Wajumbe waliochangia
hoja hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Balozi Mohammed Ramia amesema Serikali
ya SMZ na SMT kwa sasa wanalishughulikia Suala la CORONA kitaifa na kwa pamoja na wanaendelea
kushirikiana vizuri.
Amesema kwa sasa Serikali imeelekeza kuliangalia
suala la ugonjwa huu kiafya zaidi na baadae watakaa kwa pamoja kulitafakari
suala hili na athari zake kiuchumi.
“Haina maana hivi sasa hatujui kama kuna huu
ugonjwa, tunajua vizuri lakini tukifanya hivi sasa matokeo yatakuwa madogo
zaidi halafu tutakuja pata tabu ya kurekebisha wakati huo…………… Sasa wakati
tunakwenda hivi sijui tutafanya tathmini gani yakua leo sita, kesho nane na
kesho kutwa Kumi. Mheshimiwa Mungu atusaidie.”
Alisema Waziri wa Fedha na Mipango.
Mwisho
Himid
Choko, BLW
Alhamis,
April 16, 2020
No comments:
Post a Comment