Habari za Punde

Hivi ndivyo COVID 19, inavyoangamiza ujasiriamali wa mwanawake Pemba Wasema ikiendelea kunawiri watakuwa na COVID ya kiuchumi


WAJASIRIAMALI kutoka maeneo mbali mbali kisiwani Pemba, wakiwa kwenye mafunzo maalum ya utengenezaji wa mikoba ya ukindu inayotumia vitambaa na kisha kushonwa kwa cherehani, mafunzo hayo yaliyofayika mwaka 2017 Kiuyu wilaya ya Wete na kuendeshwa na TAMWA, (Picha na Haji Nassor).
Na. HAJI NASSOR, PEMBA                                                                                                         
TOKEA mwezi Disemba mwaka jana, nchini China kulitangaazwa kuibuka kwa ugonjwa wa COVID 19, unaosababishwa na virusi vya Corona.

Awali waliyowengi, walidhani ugonjwa huo ni kama yale magonjwa mengine ya mafua ya ndege, pengine na hata ebola ambayo huwa na kawaida ya kubakia katika nchi chache.

Ugonjwa huu, ulianza kuingia barani Afrika kwenye nchi ya Misri mwezi Machi, na kisha kusambaa kwa kasi kwenye nchi za Afrika Mashariki Tanzania, Uganda na Kenye zikihusika.

Wataalamu wanasema, ugonjwa huo ni wa aina ya pekee, katika kusambaa kwake, maana kwa mfano UKIMWI ulihitaji nji kubwa mfano kubadilishana damu, tendo la kuingiliana na mengine ndipo usambae.

Kwenye COVID 19, inasambaa kwa njia nyepesi mno, mfano mwenye ugonjwa hata chafya yake, mafua, machozi, mate achia mbali damu au kulala nae.

Ndio maana kila mmoja, hata baada ya kuingia kwa ugonjwa huo nchini Tanzania na hadi kufikia Mei 7, kuwa na wagonjwa 509, kati ya hao Zanzibar ikiripoti 134, alikuwa mwoga mara mbili.

Hapo tena matamko ya viongozi wakishirikiana na watalamu wa afya, yalianza kuwataka wafanyabiashara na wajasiriamali kama sio kufunga biashara zao kabisa, basi wachukue kila aina ya tahadhari.

ATHARI YA CORONA KWA WAJASIRIAMALI WANAWAKE
Kisiwa cha Pemba kama kilivyo cha Unguja, kila penye wajasiriamali 10, basi nane kati yao wamewezeshwa au kuoneshwa njia na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania ‘TAMWA’ ofisi ya Zanzibar.

Katibu wa ushirika wa ‘Tupate sote wa Mavungwa shehia ya Mbuzini Wilaya ya Chake Chake Meiye Hamad Juma, anasema kwao Corona imeathiri sana shughuli zao.

Kabla ya ujio wa janga hilo, walikuwa wakiiuza bidhaa zao na kujipatia wastani wa shilingi 250,000 hadi shilingi 300,000 kwa mwezi, kwa vile walikuwa na uhuru wa kuzitembeza watakavyo.

Bidhaa zao kama za mikoba ya kisasa ya ukili, inyoshonwa kwa cherehani, mafuta ya mti wa Mkaratusi, jiki na sabuni ya maji walikuwa wakiwafuta wateja hadi majumbani mwao.

“Wateja wetu ni wale wa nyumba kwa nyumba au mlango kwa mlango, ndio maana hapo ikifika mwezi tukifanya hesabu tunajikuta mpaka na shilingi 300,000 lakini sasa Corona imetupiga karantini ya kiuchumi,’’anasema.

Athari kubwa ya Corona ndani ya kikundi hichi cha wanawake, Katibu anasema ni kushuka kwa mauzo, hadi kujipatia shilingi 75,000 na zisizozidi shilingi 80,000 kwa mwezi.

Kwa hesabu za darasa la saba, utagundua kila mwezi wanawake hawa sasa wanapoteza kati ya shilingi 220,000 hadi shilingi 225,000 kutokana na kukosa kutembeza bidhaa zao.

Anasema Corona ikiendelea kung’ang’ania Tanzania, safari ya kurejea kwenye umaskini, ambao walishauwaga kwa miaka zaidi ya 10 sasa, itanukia.

Fatma Abdi wa kikundi cha Nyota njema cha kijiji cha Kiungoni wilaya ya Wete, anasema kabla ya Corona kwa mwaka 2019 pekee, walijipatia shilingi 1, 450,000 baada ya kuuza mikoba 45, sabuni ya maji dumu sita zenye ujazo wa lita tano tano, sabuni za miche 60 na vipochi 20 vya kisasa.

Anasema Corona kwa vile wataalamu wa afya wanataka kujiepusha na mikusanyiko, ambayo ndio waliyokuwa wakiitumia kutangaaza na kuuza bidhaa zao, sasa mambo ni magumu.

“Unajua sisi tukisikia pahala panamikusanyiko tushafika na bidhaa zetu, maana ndio tulivyofahamishwa na wawezeshaji kutoka TAMWA, lakini sasa Corona imeingilia kati,’’anafafanua.

Kwa sasa baada ya kukosa kutembeza bidhaa zo kutokana na uwepo wa Corona, wanazo bidhaa za shilingi 279,500 ambazo zimo ndani zikisubiri wateja.

Miongoni mwa bidhaa ambazo zimejiweka karantini kutokana na kuingia woga wa kuzitembeza kama zamani, ni pamoja na sabuni ya maji dumu tatu zinazojumuisha lita 15, dawa maalum ya kutolea madoa ‘Jik.

Lakini athari hii ya Corona ambayo pia kwa Tanzania imeshasababisha vifo 16 hadi Aprili 30 mwaka huu, imewakumba hata wajasiriamali wanawake mmoja mmoja, akiwemo Nassr Salum Mohamed.

Anasema katika eneo analoishi la Minungwini wilaya ya Wete, alikuwa na kawaida ya kutembeza bidhaa vile karafuu mchanganyiko kwa ajili ya kutolea nongo za mwili ‘singo’.

Lakini amekuwa akisambaaza kwa wateja wake pia bidhaa kama majani ya chai ya tiba, mikoba ya kisasa ya ukili ambapo fursa hiyo ilikuwa ikimtanulia soko lake.

Kabla ya Corona, alikuwa akipita kwenye vijiji vya Mchanga mdogo, Minungwini, Kwa bikirembo, Kigongoni, Kojani, Kangangani na Ole ili kuwafuata wateja wake.

Hilo analazimika kulifanya kutokana na uwepo wa wajasiriamali wengi zaidi sasa kisiwani Pemba, na kama engeamua kuwasubiri, engechelewa kufikia lengo.

“Mimi hakuna kijiji ambacho kwa wilaya ya Wete na Micheweni sijafika kuwafuta wateja tena kwa mguu, na huingia kila nyumba kwanza kuwasomesha na kisha kuwauzia, na narejea kwangu magharibi,’’anasema.

Anasema ujasiriamali mzuri, lazima uwe na sifa ya kuitangaaza bidhaa na kisha kuwafuata wateja walipo, ili kuwapunguzia usumbufu wa kukufuata ulipo.

Kazi hiyo za kuviandama vijiji kimoja baada ya chengine, alikwisha izoea na alikuwa akijipatia wastani wa shilingi 120,000 hadi shilingi 130,000 kwa mwezi hutegemeana na msimu.

“’aaa…!!!... katika mjasiriamali mwanamke aliyeathiriwa na Corona kiuchumi kwa hapa Tanzania basi ni mimi, maana sasa hakuna tena mpango wa kuwafuata wateja majumbani, ukipiga hodi waangaliwa kwa dirishani,’’anasema.

Anaeleza kuwa, tokea kuanza kwa karantini ya kuacha mikusanyiko isiyo ya lazima kwa hofu ya Corona, sasa biashara zake zinaelekea kupoteza mwelekeo.

“Sasa mimi tokea kuanza kwa Corona kwa mwezi mapato yangu yameshuka kutoka shilingi 130,000 za kabla na sasa nauza shilingi 70,000 tu,’’anasema.

Hivyo mjasiriamali huyo anasema, kama Corona ikiendelea kubakia Tanzania hadi visiwani, hana hakika kuwa ujasiriamali wake ambao aliwezeshwa na mradi wa uwezeshaji wa ‘WEZA II’ kuipitia TAMWA unaweza kuwa mkombozi.

Kadhia hii ya Corona pia, imebisha hodi ndani ya kikundi cha ‘Nguvu yetu ni umoja’ cha Minunwgini kinachotengeneza majani ya chai ya kileo na yenye tiba.

Kikundi hicho chenye wanachama 11 wanawake waliyojikusanya na kuamua kuukimbia umaskini, wanatengeneza mikoba ya kisasa ya ukili na pamoja na singo za karafuu.

Kupitia Mwenyekiti wake bibi Maulid Saleh Hamad, anasema walishajiandaa kwa bidhaa zenye thamani ya shilingi milioni 1, 260,000 tayari kwa safari ya mkoani Tanga, kwenye maonyesho waliyokwishaalikwa.

Wenyewe walikuwa na mikoba ya kisasa 40 kwa bei ya mmoja shilingi 30,000 inayotengenezwa kwa ukindu na kushonwa kwa cherehani na kutia kitambaa ndani, majani ya chai vikopo 100 sawa idadi kama hiyo ya vipochi.

“Lakini safari yetu ya Tanga, iliota mbawa baada ya mdudu  Corona kutia nanga Tanzania, na sasa bidhaa hizi tumelazimika kuzisambaaza katika maeneo ambayo, hatuna uhakika wa kununuliwa,’’analalamika.

Kikundi hichi cha ‘Nguvu yetu ni umoja’ ambacho kilianzishwa mika tisa iliyopoita, kutokana na dunia kutoingiliwa na ugonjwa huu wa Corona, mwaka 2018, waligawana faida na kila mwanachama alijipatia shilingi 60,000.

Ingawa faida hiyo ilipanda karibu mara mbili, maana mwaka 2019, waligawana kila mwanachama shilingi 110,000 baada ya kuzichana chana shilingi 1,210, 000 walizozipata kama faida kupitiza uzalishaji wa bidhaa zao.

“Unaona Corona ilivyotuvuruga, maana hata mwaka huu 2020 tunatarajia kugawa faida ndogo sana, isiyozidi shilingi 50,000 kila mmoja, maana ndio imetuendesha mchomo kwa kukosa kwenda kwenye maonyesho Tanga,’’anaeleza.

WATEJA WA WAJASIRIAMALI WAMEATHIRIWA NA CORONA?
Ashura Hassan Makame wa Mchanga mdogo, anasema ameshaacha kutumia sabuni ya maji na ya kipande ‘miche’ aliyokuwa akipitishiwa na mjasiriamali kutoka wilaya ya Mkoani.

Anasema, ilikuwa kila baada ya miezi miwili, alikuwa akigongewa mlango na mjasiriamali huyo na kumkopesha sabuni hizo, ingawa kwa sasa mwezi mmoja na nusu hajampitia.

“Nilimpigia simu siku moja akasema Corona imemzuia na hawezi kutoka, kiholela hivyo pesa zake amtumie kwa simu na sabuni hana mtu wa kumpa ili zimfikie,’’anasema.

Omar Khamis Haji wa Chake Chake, anasema alikuwa akiletewa majani ya chai ya asili kutoka Wete na mwanamke mmoja ambae anamfahamu kwa jina la Rukia, ingawa sasa anasiku 30 zaidi hajamuona.

“Baada yeye kutopita sasa nimerudia majani ya chai yale ya viwandani, ingawa moja hutumia siku nne, maana ni makali sana, na sio mazuri kiafya,’’anasema.

Hasnuu Ussi wa Mtambile anasema wiki moja ijayo atakuwa ameshamaliza majani ya chai na sabuni za mjasiriamali Arafa Mohamed wa Kangani, na anasema kwa sasa ameshaacha kutengeneza.

“Nilipomuuliza anasema, kwa vile biashara yake ni ya kutembeza na sasa uwepo wa Corona, ana hofu ikaganda ndani na kukosa wateja,’’anasema.

Mfanyabiashara Mohamed Hamad ‘ustadhi’ wa mjini Chake Chake anasema hata yeye Corona imemuathiri, maana alikuwa akipokea oda za sabuni ya maji kutoka kwa mjasiriamali wa mji wa Konde na sasa amerudia zile za viwandani.

“Nikimpigia simu anasema, kwanza ameamua kuacha maana baadhi ya malighafi huchukua mkoani Tanga, lakini kutokana na janga la Corona, anahofu kwenda huko,’aliniaeleza.

SERIKALI KUU
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiwasilisha bajeti ya ofisi yake ya mwaka 2020/2021, Baraza la Wawakilishi, alisema uchumi wa Zanzibar ulitarajiwa kukua kwa asiliamia 7 hadi 8 kwa mwaka 2020, lakini uwepo wa Corona sasa unatarajiwa kukua kwa asilimia 3.

Alisema hilo limesababishwa kutokana na kuyumba kwa sekta za uchumi ikiwemo utalii, biashara, uwekezaji na kupungua kwa mapato ya serikali.

TAMWA KINASEMA JE?
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania ‘TAMWA’ ofisi ya Zanzibar, chenyewe kinakereketwa na uwepo wa Corona, na hasa kuona ni adui wa uchumi kwa wajasiriamali wanawake.

Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar dk. Mzuri Issa wakati akiwasilisha mada ya athari za Corona na uhuru wa kujieleza hasa kwa wanawake, kupitia njia ya kielektroniki ya ‘zoom cloud meeting’ ilioyoandaliwa na shirika la Internews, anasema Corana ilisababisha serikali kufunga masoko kuanzia 10:00 jioni.

Anasema soko kama la wazi la Darajani mjini Unguja, kabla ya uwepo wa Corona, lilikuwa likianzia saa 11:00 jioni hadi saa 4:00 usiku, na kutoa fursa kwa wajasiriamali wengi wao wanawake kuuza bidhaa zao mbali mbali.

“Wapo wanawake, maskini na wajane wengi wanaofanyabiashara kama za mazao ya chakula na biashara wakiyatumia masoko ya Mwanakwerekwe na Darajani, lakini hawafaidiki nayo kiukamilifu na kuathiri uchumi wao,’’anasema.

Kwenye eneo jengine Mratibu wa TAMWA Ofisi ya Pemba Fat-hiya Mussa Said, anasema ‘TAMWA’ imeshandaa mpango wa kisasa wa kuhakikisha inawaunganisha wajasiriamali wanawake na wateja wao kwa njia ya kielektroniki.

Anasema, ingawa wazo hilo lipo kwa muda mrefu, lakini sasa wameamua kulifungia kazi, ili kuona Corona haiwi janga mara mbili, kwenye afya na uchumi wa wajasiriamalia wao.

“Corona ipo ulimwenguni kote na sasa hadi kisiwani Pemba, imeshaweka makaazi, na ni kweli wajasiriamali wetu walitegemea sana mikusanyiko ili kuuza bidhaa zao, lakini sasa ni marufuku,’’anafafanua.

Hivyo, anaona njia moja ya kuhakikisha wanazalisha na kuuza bidhaa zao, ni kuwatengenezea makundi ya ‘wasap’ kupitia simu zao na kisha kuwaunganisha na makampuni kama ya ndege, meli, hoteli na taasisi za serikali, ili kuhakikisha wanauza bidhaa zao,’’anafafanua.

Akawataka wasikate tamaa nawendelee kuzalisha, kwani moja ya changamoto za ujasiriamali ni uwepo wa magonjwa kama hayo, ambayo wakati mwengine hurejesha nyuma juhudi zao.

MAPENDEKEZO
Wenyewe wajasiriamali kisiwani Pemba, wamependekeza kuwa kama hali ya Corona itaendelea kuwepo, basi masoko ya Jumapili yafunguliwe kwa utaratibu unaokubalika wa wataalamu wa afya.
                                     Mwisho  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.