Mheshimiwa Spika, Awali ya yote, naomba
nichukuwe nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu sub-hanahu wataalah kwa
kutujaalia afya njema na uwezo wa kutekeleza majukumu yetu kwa lengo la
kuwatumikia wananchi wetu, na mafanikio yake ni kuijenga nchi yetu ya Zanzibar
itakayowanufaisha wananchi wetu wa sasa na vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Spika, Naomba sasa niziwasilishe
shukurani zangu za dhati kwako wewe, kwa
kunipa fursa hii kusimama mbele ya Baraza lako tukufu kwa lengo la kuzungumzia
machache na ya muhimu, yanayohusu bajeti ya Wizara ya Habari, Utalii na Mambo
ya Kale kwa mwaka wa Fedha 2020/2021.
Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa maelekezo ya Kanuni ya 96 (1) ya
Kanuni za Kudumu za Baraza la Wawakilishi Toleo la 2016, naomba kulijuilisha
Baraza lako tukufu kwamba, Kamati ya Maendeleo ya Wanawake, Habari na Utalii ya
Baraza la Wawakilishi imepitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya kazi za kawaida na kazi za maendeleo kwa Mwaka
2020/2021 kwa Wizara ya Habari, Utalii
na Mambo ya Kale.
Mheshimiwa Spika, Kamati
ya Maendeleo ya Wanawake, Habari na
Utalii ya Baraza la Wawakilishi inaipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kwa kukipandisha hadhi Chuo cha Uandishi wa
Habari na Mawasiliano ya Umma Zanzibar na kukihamishia Chuo Kikuu cha
Zanzibar, ili kiweze kutoa Shahada ya
Kwanza ya Uandishi wa Habari hapa
nchini. Tunaamini kwamba kitendo hiki ni
miongoni mwa hatua muhimu ya kukuza na kuinua tasnia ya Habari hapa Zanzibar
ikiwa ni miongoni mwa mafanikio ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi
ya 2015- 2020.
MAPATO
Mheshimiwa Spika, Kamati
yetu inaipongeza Wizara kwa kusimamia vyema makusanyo hasa kwa Kamisheni ya
Utalii iliyofikia asilimia 71%. Hata hivyo,
juhudi zaidi bado zinahitajika kwa
taasisi nyengine za wizara hiyo zinazopeleka mapato yake katika mfuko mkuu wa
Hazina ikiwemo Idara ya Habari Maelezo, Tume ya Utangazaji, Idara ya Makumbusho
na Mambo ya Kale, Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu pamoja na Ofisi kuu Pemba,
ili nazo ziweze kufikia malengo ya makusanyo waliyopangiwa. Kwenye eneo la
Makusanyo ya taasisi zilizoruhusiwa kutumia hali haiko vizuri, kwani kwa tathmini ya jumla
taasisi hizo zimekusanya asilimia 42%
tu, ambapo Wakala wa Uchapaji alikusanya asilimia 27% na Shirika la Utangazaji
Zanzibar lilifikia asilimia 30% tu ya ukusanyaji. Ni mategemeo ya Kamati kuwa taasisi hizi
zilizoruhusiwa kutumia zingefanya juhudi za ukusanyaji ili zipate fungu kubwa
zaidi la matumizi na hivyo kufanikisha utendaji wa taasisi hizo.
PROGRAMU YA MAENDELEO YA HABARI,
UTANGAZAJI NA UPIGAJI CHAPA
Mheshimiwa Spika, Kamati
yetu imefurahishwa na inaunga mkono uamuzi wa serikali wa kuendelea kukuza misingi ya Demokrasia na Utawala Bora
hapa nchini na hatimae kuwa na jamii
iliyoimarika katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa kupitia habari. Kamati
Inazihimiza Shirika la Ungazaji Zanzibar
(ZBC), Idara ya Habari Maelezo na Shirika la Magazeti la Serikali kuimarisha
huduma za Urushaji wa Vipindi na matangazo pamoja na utoaji wa taarifa, picha
na sinema kwa ufanisi mzuri ili
kufanikisha viashiria na shabaha zilizokusudiwa katika Programu ya Maendeleo ya Habari, Utangazaji na Upigaji
Chapa.
Mheshimiwa Spika, Kamati
yetu inazidi kutoa wito kwa vyombo vyetu vya habari vya umma kuzidi kujitambua
kwamba ni mdomo wa Serikali na hivyo vinabeba dhima kubwa na nzito katika jamii,
napia vitambue kwamba bado vinaendelea kuaminiwa na kupendwa na wanajamii
walio wengi, hivyo havina budi kuwa mstari wa mbele katika kukuza mila, silka
na utamaduni wetu ikiwemo matumizi fasaha ya lugha ya Kiswahili. Mheshimiwa Spika , tumekuwa
tukishuhudia baadhi ya watangazaji wa shirika letu la ZBC wamekuwa na mbwembwe
nyingi tena katika vipindi muhimu kama vile taarifa za habari na vipindi maalum
suala ambalo wakati mwengine linaishushia hadhi Shirika hilo. Tunawaomba wale
wote waliopewa dhamana ya kuwasimamia sekta ya utangazaji watimize wajibu wao,
ili watangazaji wa ZBC wasiwakwaze wasikilizaji na watazamaji wao kwa kuwa na
uteuzi na matamshi mazuri ya maneno wanayoyatumia.
Katika
hatua nyengine, Kamati yetu inaipongeza sana Kampuni ya Uunganishaji wa Maudhui
(ZMUX), kwa kuweza kuvuka lengo la kukusanya asilimia hadi 184% ya mapato yake na kufikia hatua ya kuhudumia wateja 14,485 kutoka na ufanisi mzuri wa
utendaji na ubora ya king”amuzi cha ZMUX.
PROGRAMU YA MAENDELEO YA UTALII , MAKUMBUSHO, MAMBO YA
KALE NA UTUNZAJI WA NYARAKA NA KUMBUKUMBU
Mheshimiwa Spika, Katika
eneo ambalo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inapaswa kujivunia ni uendelezaji
wa Maeneo ya kihistoria na Mambo ya Kale kwa jitihada zake za kuyalinda na kuyahifadhi.
Kamati imetembelea takriban maeneo yote
yaliyofanyiwa ukarabati katika miaka ya hivi karibuni Unguja na Pemba na inaridhika na kazi
iliyofanyika na inayoendelea kufanyika katika maeneo hayo, na kupelekea kuongezeka kwa watalii wa nje na
ndani ya nchi katika maeneo hayo.
Kamati
imepokea kwa nia njema hatua ya ufungaji wa boya katika mji wa Kale uliozama wa
Mkumbuu uliopo Ndagoni Pemba. Hata hivyo, kwa kuwa “Mkono mmoja hauchinji Ng’ombe ”;
tunaziomba Mamlaka zote zinahuzosika kushirikiana kufufua miundombinu yote ya
kulifikia eneo hilo na kulitangaza zaidi kwa lengo la kuongeza idadi ya wageni
watakaotembelea mji huo.
Mheshimiwa Spika,
Kamati pia imefarajika na uamuzi wa
wizara kwa kuanza kufikiria kubuni vianzio vipya vya Mapato, ambapo kwa mwaka
ujao wa fedha Idara ya Nyaraka na
Kumbukumbu inakusudia kuanza kutoza ujira wa Kutengeneza Nyaraka. Huu ni mwanzo
mzuri, na tunaishauri wizara isichoke na kutumia wataalamu wake wa mipango na
uchumi kufikiria njia mbali mbali za kutunisha mifuko ya wizara hiyo na
serikali kwa ujumla.
PROGRAMU ZA UTANGAZAJI NA UHAMASISHAJI
WA UTALII
Mheshimiwa Spika, Kabla sijamaliza hotuba
hii naomba
tuiangalie Sekta ya Utalii, Sekta ambayo ndio tegemeo kuu la Mapato
ya Wizara hii na serikali kwa ujumla pamoja na Ajira kwa vijana wetu. Tunapata
matumaini kusikia kwamba Kamisheni ya Utalii kwa Kipindi hiki imeweza kusimamia
uanzishwaji wa Miradi ya wazalendo 100 na kutengeneza ajira za moja kwa moja
zipatazo 980. Hii ni hatua nzuri na tunaiomba
Kamisheni ya Utalii kuongeza juhudi na bidii ya kazi, ili kupiga hatua kubwa zaidi
katika sekta hii ya utalii. Tunawaomba waheshimiwa Wajumbe kuridhia maombi ya
Kamisheni na kuwaidhinishia shilingi 4,115,300,000
kwa ajili ya shughuli mbali mbali walizojipangia mwaka ujao wa Fedha, ikiwa ni pamoja na kuyaimarisha mashamba ya
viungo yanayotoa huduma kwa watalii na kuandaa vielelezo vya kutangaza utalii
kwa kushirikiana ipasavyo na Ofisi za Ubalozi za Tanzania zilioko nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Mwisho naomba kuchukua fursa hii kwa kuwashukuru Wajumbe wa Kamati kwa mashirikiano
yao waliyoyaonesha kuanzia mwanzo hadi mwisho wa tukipitia bajeti hii, kwa ruhusa
yako naomba niwatambue kwa majina kama ifuatavyo:
1.
Mhe. Mwantatu Mbarak Khamis - Mwenyekiti
2.
Mhe. Mussa Foum Mussa -
Makamu Mwenyekiti
3.
Mhe. Omar Seif Abedi -
Mjumbe
4.
Mhe. Zaina Abdalla Salum - Mjumbe
5.
Mhe. Saada Ramadha Mwendwa -
Mjumbe
6.
Mhe. Mwanaidi Kassim Mussa -
Mjumbe
7.
Mhe. Makame Saidi Juma - Mjumbe
8.
Ndg. Himid Haji Choko -
Katibu
9.
Ndg. Mussa Issa Mussa - Katibu
10.
Ndg. Amina
Abeid - Msaidizi
11.
Ndg. Azmina
Hamad - Msaidizi
Nimalizie
kwa kuwashukuru Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi kwa kunisikiliza kwa
umakini na kwa utulivu mkubwa.
Ahsante.
(Mhe. Omar Seif
Abeid)
Mjumbe,
Kamati ya Maendeleo
ya Wanawake Habari na Utalii,
Baraza la
Wawakilishi,
Zanzibar.
No comments:
Post a Comment